RIPOTA PANORAMA
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameitupia ‘mzigo’ Ofisi ya Msajili wa Hazina skandari kuhusu kuporwa kwa ardhi na mali za umma na kutumika kuchukua mkopo wa mabilioni benki.
Skandari hiyo inayoihusu kampuni binafsi ya SISI Construction Company Limited (SISICOL) yenye hisa asilimia 75 kwenye kampuni ya umma ya Mwananchi Engeenering and Contracting Company Limited (MECCO).
Awali SISICOL ilimega kipande kikubwa cha hisa za Serikali, asilimia 25 ilizokuwa ikimiliki kwenye Kampuni ya MECCO na kubakiza hisa asilimia 2.6 tu kabla ya kuhamisha umiliki wa baadhi ya mali za MECCO.
Madai ya SISICOL ni kwamba hisa hizo walizichukua kama sehemu ya malipo ya deni la fedha zake lililoingizwa kwenye vitabu mwaka 2008.
Kampuni hiyo ilihamisha umiliki wa hati hizo na kuwa mali yake bila ya kuihusisha Serikali na kuchukua mkopo wa mabilioni ya shilingi katika benki mbili tofauti, ikiwemo mkopo unaoonyesha kiwango kisicho na ukomo (unlimited amount.)
Akijibu kuhusu hatua iliyofikiwa na Serikali kuzikomboa hisa zake hizo pamoja na mambo mengine, Waziri Mbarawa amesema skandari hiyo anayeweza kuizungumzia ni Msajili wa Hazina, ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mashirika ya umma.
Waziri Mbarawa aliulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa kunusuru hisa hizo za Serikali inazomiliki kwenye Kampuni ya MECCO baada ya kuporwa na SISICOL na kubakishiwa hisa asilimia 2.6 pekee.
Aidha, Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Waziri Mbarawa kuhusu hatma ya viwanja viwili ambavyo ni mali ya MECCO; kiwanja namba 2 na namba 3B vilivyopo Barabara ya Nyerere katika Manispaa ya Temeke kubadilishwa umiliki wake kinyemele kwenda kwenye umiliki wa Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited.
Tanzania PANORAMA Blog ilitaka kupata kauli ya Waziri Mbarawa kuhusu hati za viwanja hivyo, namba 2 namba 3B mali ya MECCO kutumiwa na Kampuni ya Mas Holding Depot Limited kuchukua mkopo wa mabilioni ya Shilingi kwenye benki mbili kubwa hapa nchini bila Serikali ambaye ni mwanahisa kuwa na taarifa zozote kuhusu mkopo huo.
Swali jingine aliloulizwa Waziri Mbarawa lilihusu Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited kupewa leseni ya kufanya biashara ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha makontena katika eneo la viwanja namba 2 na 3B bila kufanyiwa ukaguzi wowote na mamlaka za udhibiti na usalama ambapo moja ya mamlaka zilizopaswa kufanya ukaguzi na kutoa leseni hiyo ni TASAC iliyo chini ya Waziri Mbarawa.
Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza zaidi Waziri Mbarawa kuwa; ‘inadaiwa TASAC huku ikujua kuwa katika maeneo ya viwanja hivyo kulikuwa na biashara nyingine inayofanyika ilifumba macho na kuacha kutekeleza wajibu wake wa kukagua maeneo hayo ambako kuna biashara nyingine inayoendelea ili kutoa mwanya kwa Kampuni ya Mas Holding and Container Depot Limited kufanya biashara katika maeneo hayo kinyume cha taratibu. Tunaomba kupata kauli yako kuhusu madai hayo.’
Akijibu, Waziri Mbarawa aliandika; ‘Ninaomba uongee na Msajili wa Hazina. Yeye ndiyo anayesimamia mali zote za mashirika ya umma.’
Tanzania PANORAMA Blog ilimtumia maswali matatu Msajili wa Hazina, Benedicto Mgonya kwenye simu yake ya kiganjani ambayo aliyasoma kisha akakaa kimya lakini baadaye Tanzania PANORAMA Blog ilimtumia ujumbe wa kumkumbusha kujibu maswali iliyomuuliza ndipo naye akaandika ‘utapigiwa simu na wahusika, nipo kikaoni.’
Mgonya ametoa kauli hiyo huku rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania PANORAMA Blog imekwishawasilisha ofisini kwake maswali kuhusu skandari hiyo zaidi ya miezi sita iliyopita na mara zote ofisi yake imekuwa ikipiga chenga kutoa majibu au ufafanuzi.
KESHO USIKOSE KUSOMA TANZANIA PANORAMA BLOG ILI KUJUA ZAIDI UNDANI WA SAKATA HILI.