RIPOTA PANORAMA
SAKATA linalotokota chini kwa chini kwa muda mrefu sasa linalohusu Kampuni ya Symbion Power LLC kulipwa na Serikali, Shilingi bilioni 350 huku ikiwa na malimbikizo ya madeni ya kodi na gharama nyinginezo limeibuliwa bungeni.
Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ndiye aliyeliibua alipokuwa akichangia mjadala wa taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya malipo yaliyofanywa kwa Kampuni ya Symbion Power LLC.
Katika mchango wake huo uliokuwa na hoja tatu, alihoji uhalali wa malipo hayo akizingatia ripoti (CAG) ya mwaka 2021/22 ambayo imeonyesha kuwa yalifanyika pasipo kuzingatia kodi na gharama nyingine ambazo Serikali inaidai kampuni hiyo.
Katika mchango wake huo, Mpina ambaye kwa sehemu kubwa alikuwa akinukuu ripoti ya CAG, alihoji udharura wa malipo hayo ya mabilioni ya fedha kwa kile alichosema yalifanyika haraka haraka, aliyeidhinisha malipo kufanyika na aliyeisababisha Serikali hasara kwa kuingia mkataba mbaya na Symbion.
āSerikali imelipa Sh. bilioni 350 kwa hii kampuni lakini pia kwa maana ya Dola za Marekani milioni 153.43.
āMkaguzi anatuambia kuwa, na kamati inatueleza kuwa makubaliano haya yalifanyika bila kujumuisha kodi wala gharama zingine.
āSasa maswali ya kujiuliza ni kwanini Serikali ilipe Sh. bilioni 350 kwa Kampuni ya Symbion bila kuangalia Symbion inadaiwa kodi kiasi gani na Serikali, bila kuangalia gharama ambazo Symbion anahusika kuilipa Serikali?ā
Mpina alisema makubaliano ya kulipwa kwa fedha hizo yalifanyika Mei, 2021 na zililipwa haraka baada tu ya kufanyika kwa makuliano hayo huku Bunge likiwa limekwishaidhinisha bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2020/2021.
āNa je, kulikuwa na udharura gani, haraka tu baada ya makubaliano, Mei 2021 baada ya makubaliano ya kulipa hizi fedha, kwanini zililipwa haraka pale pale na kama zililipwa kwa dharura namna hiyo nani aliidhinisha fedha hizi kwa maana Bunge lilikuwa tayari limeishaidhinisha bajeti ya mwaka 2020/2021.
āSasa ilipofika Mei zimelipwa bilioni 350 kwa Kampuni ya Symbion, hizi fedha zilitoka wapi? Nani aliziruhusu wakati Bunge hili lilikuwa limeishapitisha bajeti tayari?
āKatika mwaka huo wa fedha tulikuwa tuna miradi mingi ya maendeleo iliyokuwa inatakiwa kutekelezwa. Serikali iliwezaje kulipa fedha hizo wakati bajeti ya Serikali ilikuwa imeishapitishwa.
āLakini mkaguzi hapa anatuambia hapa kulikuwa na usimamizi mbaya wa mkataba, hao waliousimamia mkataba vibaya mpaka wameisababisha nchi yetu kulipa bilioni 350 ni akina nani? mbona hawajatajwa? ni nani aliusimamia mkataba huu mbaya? Kwanini huyo mtu hatajwi na aliusimamia vipi huo mkataba vibaya?ā
Mpina aliendelea kulieleza Bunge kuwa mkataba wa kampuni hiyo kuzalisha umeme hapa nchini ulikuwa unaishia Septemba 18, 2015 na Bunge lilitaarifiwa kuwa hautahuishwa lakini ulihuishwa ghafla siku tatu kabla ya kuisha.
āMkataba huu ulikuwa unaisha 18 Septemba, 2015 ulikuwa unaisha kabisa lakini baadaye ulifufuliwa. Ulikuja kuhuishwa na makubaliano ya Septemba 15, 2015 siku tatu kabla ya mkataba kufika mwisho.
Mkataba huu ulihuishwa kwa dharura hivyo kulikuwa na udharura kiasi gani kwa sababu wakati huo Bunge lilikuwa limeishaambiwa kuwa mkataba huo umefika mwisho na hautaendelea.
Mkataba baina ya TANESCO na Symbion wa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Ubungo, Dar es Salaam kwa mara ya kwanza uliingiwa Julai 2001 na kumalizika Septemba 2013. Baada ya hapo uliongezwa kwa miaka miwili hadi Septemba 2015, na kuibua utata na maswali kuhusu nyongeza hiyo.
āHizi kodi za Serikali huyu Symbion analipwaje kwa sababu cha kwanza huyu Symbion wakati analipwa bilioni 350 sisi tulikuwa tunamdai kiasi gani?ā alihoji Mpina.
Mpina ameliibua sakata hili bungeni ikiwa ni miezi michache baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii ikimhusisha mwanamke mmoja Mtanzania anayeishi nje ya nchi ambaye pia ana undugu wa kuzaliwa wa mmoja wa viongozi waandamizi wa Serikali kuwa kiungo muhimu aliyewezesha kampuni hiyo kulipwa mabilioni hayo.
Katika video hiyo, inadaiwa mwanamke huyo ambaye alipewa mgao wa mabilioni ya Shilingi baada ya kufanikisha malipo hayo, alikwenda kununua nyumba Dubai.
Video hiyo ilifutwa muda mfupi baadaye huku kukiwa na madai kuwa mfanyabiashara Mtanzania mwenye uwezo mkubwa wa kiuchumi ambaye ana mkono wake katika kampuni ya Symbion ndiye aliyefanikisha kufutwa kwa video hiyo.
Inadaiwa mfanyabiashara huyo ambaye ana uhusiano binafsi na mwanamke aliyefanikisha kampuni hiyo kulipwa mabilioni hayo na Serikali ni mnufaika wa moja kwa moja wa mabilioni ambayo Symbion imelipwa na kwamba yupo kwenye mkakati mahususi wa kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
TANZANIA PANORAMA BLOG INAFANYA UCHUNGUZI WA KINA WA SINTOFAHAMU HII NA ITAANDAA RIPOTI MAALUMU ITAKAYOGUSA MAENEO YOTE YANAYODAIWA KUWA NA SHAKA KUHUSU MALIPO HAYO NA WATU WANAODAIWA KUYAFANIKISHA.