RIPOTA PANORAMA
TIMU ya soka ya wanawake wa Simba, Sinba Queens jana ilifanikiwa kutinga nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika baada ya kuichakaza bila huruma mabao 2-0 timu ya wanawake ya Green Buffalloes ya Zambia.
Ikitandaza kandanda la kukata na shoka katika uwanja wa Marrakech, Simba Queens ilikosa windo lake la kwanza dakika ya 43 ya kipindi cha kwanza baada shuti la mshambuliaji wake, Djafar kutoka nje kidogo ya lango.
Kipindi cha pili Simba Queens waliingia kwa kasi ya ajabu na kuanza kuwakimbiza nyati wa kike wa kijani za Zambia kona zote za uwanja na ilipofika dakika ya 64, nyati hao walikandikwa goli la kwanza na Djafar alilolitupia kwa kichwa, akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Fatuma Issa, maarufu zaidi kwa jina la Fetty Densa.
Baada ya kupatikana kwa goli hilo, Simba Queens waliongeza kasi na kuwa kama waliofungulia turbo zilizo kwenye mapafu yao hivyo kuwafunika kabisa nyati jike wa kijani wa Zambia ambapo mnamo dakika 79 nahodha, Opa Clement alitupatia bao la pili baada ya kupokea pasi ndefu ya mpira wa kutengwa iliyopigwa na mlinzi wa kati, Daniela Kanyanya.
Katika mtanange huo, mchezaji Agnes Musase wa Green Buffaloes alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya mwisho ya mchezo baada ya kumfanyia madhambi Opa.
Kwa ushindi huo wa jana, Simba Queens imemaliza mechi zake ikiwa na alama sita na kushika nafasi ya pili nyuma na wenyeji ASFAR FC.