TIMU PANORAMA
0711 46 49 84
TAIFA liko katika kampeni ya kukuza Sekta ya Kilimo na Viwanda. Serikali inafanya kila iwezalo kuimarisha ukuaji wa Sekta ya Kilimo na Viwanda kwa kuwajengea uwezo wakulima wadogo na wakubwa na vivyo hivyo kwa wafanyabiashara na kwa upande mwingine ikizishika mkono taasisi na mashirika yake na yale binafsi yenye uhusiano wa moja kwa moja na sekta hizo.
Timu ya waandishi wa Blogu ya PANORAMA na Jarida la PANORAMA ilikutana na kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbolea (TFC), Kanjel Simon Mloba; ambayo ina dhamana ya kuimarisha na kuchagiza kilimo bora na cha kisasa ili kuendeleza uwezo wa Taifa kujitegemea kwa chakula.
Katika mahojiano hayo, Kanjel anaelezea safari ya mafanikio na changamoto ilizonazo TFC huku biashara ya mbolea akiifananisha na msemo usemao ‘zimwi likujualo halitakula likakwisha.’
PANORAMA:
Watanzania wana kiu ya kuifahamu Kampuni ya Mbolea (TFC), na hii ni kwa sababu ni moja ya taasisi muhimu za Serikali zenye jukumu la kustawisha Sekta ya Kilimo nchini. Naomba uitambulishe TFC kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na shughuli zake.
KANJEL:
Kampuni ya Mbolea Tanzania ni chombo pekee cha Serikali chenye jukumu la kuingiza, kuuza na kusambaza mbolea na viuatilifu kwa wakulima wote nchini.
Unajua, zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wameajiliwa au wamejiajili kwenye kilimo, hivyo TFC ni chombo cha kimkakati cha Serikali chenye jukumu la kuleta tija ya kilimo kwa wakulima na Tanzania kwa ujumla. Kwa kuwahakikishia Watanzania upatikanaji wambolea bora kwa wakati na kwa bei shindani.
Nchi zote makini duniani zina chombo kama TFC, nenda Zambia, Rwanda nk; na hii ni kwa sababu huwezi kuacha sekta muhimu kama hii ikawa mikononi mwa sekta binafsi moja kwa moja.
Kilimo ndio kila kitu, maisha ya binadamu yamejikita katika kilimo. Chakula kinatokana na kilimo, malighafi za viwandani nk.
Nadhani sote tunajua kuwa usalama wa nchi uko katika chakula na ili kilimo kiweze kuwa na manufaa na upatikanaji wa chakula uwe wa uhakika ni muhimu kuwa na uhakika wa upatiakanaji wa mbolea bora, hivyo TFC imara maana yake kilimo chenye tija Tanzania.
Sasa umeuliza historia ya TFC. Iko hivi, TFC ina historia ndefu sana. Kampuni hii ilianzishwa mwaka 1968 kwa ubia kati ya Tanzania na Kampuni ya M\s Clokner INA ya Kijerumani.
Madhumuni ya TFC kulingana na Memorundum and Article of Association pamoja na mambo mengine yalikuwa ni kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza mbolea nchini. Kuagiza, kununua, kuuza ndani na nje ya nchi bidhaa za aina zote zinazozalishwa na kampuni au watengenezaji wengine.
Majukuu ya awali ya kampuni ilikuwa kuendesha kiwanda cha uzalishaji wa mbolea kilichokuwa mjini Tanga.
TFC ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya makampuni ambayo kwa sasa inajulikana kama sheria ya makampuni ya mwaka 2002 (campanies act 2002cap 12) na kuwekwa chini ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), lililokuwa chini ya Wizara ya Viwanda na mara moja ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha mbolea ulianza mjini Tanga na kukamilika mwaka 1972.
Kampuni mbia ya M\S Clokner INA ya Ujerumani ilipewa ukandarasi wa ujenzi wa kiwanda na menejimenti ya kiwanda kilichoanza kazi mwaka 1972 nakilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 105,000 za mbolea kwa mwaka.
Kiwanda hiki kilikuwa kikizalisha aina tatu za mbolea ambapo mbali ya Sulfur na ammonia zilizokuwa zikitoka nje ya nchi, malighafi nyingine zilipatikana kutoka Minjingu phosphate mkoani Manyara.
Mbolea aina ya NPK, TSP na SSP ndizo mbolea zilizozalishwa na Kiwanda cha TFC cha Tanga na kusambazwa kwa wakulima wa Tanzania.
Kwa takriban miongo miwili tangu kuanzishwa kwa TFC, kampuni ilifanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu ikifikisha mbolea kwa maelfu ya wakulima waliotapakaa nchi nzima.
Kanjel Mloba |
PANORAMA:
Ni nini kilitokea kwa Kiwanda cha Mbolea Tanga hadi kikafa? Na je, TFC ina mpango wa kukifufua na kwa sasa TFC ina miliki viwanda vingapi vya mbolea hapa nchini?
KANJEL:
Mabadiliko ya sera za kiuchumi duniani yaliikumba pia Tanzania na mara moja ukiritimba wa TFC kuhodhi soko la mbolea ukatakiwa kuondolewa kupisha soko huria.
Hali hii ilikuja miaka ya 1990. Kwa bahati mbaya, April 1991 mtambo wetu wa kuzalisha tindikali (sulfuric acid) kiwandani ulipata hitilafu na kuanguka hivyo kusababisha shughuli za uzalishaji kusimama na mwezi June 1991, Kampuni ya Clokner INA ilikabidhi hisa zote kwa Serikali na kuondoka nchini.
Huenda mwaka 1991 ndio utakaokumbukwa zaidi kwa TFC kwa kuwa mwezi Oktoba, uzalishaji wa mbolea ulisitishwa rasmi hivyo kulazimisha kupunguzwa kwa wafanyakazi wote waliokuwa wanajihusisha na uzalishaji kiwandani.
Pia wataalamu wakaja na hoja kwamba kiwanda kipo mjini kwenye makazi ya watu na Sulfur ni sumu. Kwa hiyo kiwanda kikafungwa. Kufungwa kwa kiwanda kilienda sambamba na uuzaji wa mali za TFC na wafanyakazi wengi kuondolewa.
Ni kitengo cha biashara cha TFC ndicho pekee kilichobaki baada ya kufungwa kwa kiwanda na kilipewa majukumu ya kununua na kuuza mbolea. Pia kutekeleza sera za kilimo zinazohusu mbolea ikiwemo usambazaji wa mbolea za ruzuku. Kitengo hiki ndicho pekee kilichopo mpaka sasa.
PANORAMA:
Zipo taarifa kuwa kiwanda hiki kiliuzwa kama chuma chakavu kwa mfanyabiashara mwenye asili ya Asia ambaye alikisafirisha chote na kukipeleka nje ya nchi alikokisimika na kuanza kuzalisha mbolea ambayo nyingine anatuuzia sasa hapa nchini.
PANORAMA inatambua kuwa wakati huo wewe hukuwa kwenye ofisi hii lakini historia huwa haifutiki hivyo uliikuta ofisini, kwa faida Watanzania, hili likoje? Tuambie, yako wapi mabaki ya kiwanda cha mbolea cha Tanga?
KANJEL:
Ninachojua ni kwamba kiliuzwa. Kumbukumbu zinaonyesha hivyo. Waraka namba 6 wa mwaka 1996 uliotolewa na Baraza la Mawaziri ulielekeza kuondolewa kwa kiwanda katika eneo kilipokuwa kwani lilikuwa eneo la makazi ya watu.
PANORAMA:
Hali ya upatikanaji wa mbolea nchini ipoje kwa sasa?
KANJEL:
Hili nadhani linapaswa kujibiwa na mamlaka za juu yangu. Hili nadhani ni la wizara.
PANORAMA:
Turejee nyuma kidogo, hebu elezea umuhimu wa TFC kwa nchi.
KANJEL:
TFC ni Kampuni kongwe hapa nchini hivyo ni kama achieve. Watu wengi wanaotaka kufanya biashara ya mbolea wanakuja kupata uzoefu TFC na pia kujua aina za mbolea zinazotumika nchini.
TFC imesaidia sana kuilisha TFRA ili iweze kupata ujuzi juu ya kukagua mbolea na kujifunza zaidi juu ya aina za mbolea zinazotumika nchini.
Umuhimu wake mwingine ni kusaidia kutekeleza sera za nchi katika kilimo, mfano kutumika katika kusimamia ruzuku. Kwa kifupi TFC ina mtandao mkubwa ambao hakuna kampuni binafsi yoyote hapa nchini inayoweza kuufikia. Mtandao wa TFC ni wa kimkakati, unawezesha kuwafikia wakulima walio wengi kama si wote nchini.
Lakini pia TFC ina umuhimu katika urekebishaji wa bei katika soko. Sasa hapa niseme kwamba TFC inapokuwa ina mbolea makampuni mengi yanayouza mbolea yanauza mbolea kwa bei za chini kwa wakulima, pale ambapo TFC haina mbolea inakuwa ni tatizo kwani inasababisha upandaji holela wa bei za mbolea.
Mara nyingi bei inayowekwa na TFC imekuwa ikitumika kama reference ya bei kwa makampuni mengi. Mara nyingi ambapo inathibitika kuwa TFC imeishiwa mbolea, bei zawapinzani hupanda ghafla.
Mfano 2017, kampuni binafsi Songea ziliuza mbolea kwa Shilingi 75,000 lakini baada ya TFC kuanza kuuza, zilipunguza bei ya mbolea hadi kufikia Shilingi 60,000. Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa Tabora , Mbeya na mikoa mingine hapa nchini.
Kingine ni kutekeleza sera za kilimo pale ambapo wadau wengine wanakuwa wamezigomea; mfano msimu wa 2014/2015, utaratibu ulikuwa makampuni yakopeshe vyama vya ushirika na vikundi. Kampuni binafsi zote ziligoma, ni TFC tu iliyotekeleza utaratibu huo wa Serikali.
Pia kuhakikisha uwepo wa Serikali katika mfumo mzima wa uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa mbolea nchini.
Tumeona wakati wa janga la Uviko 19, ni Serikali pekee iliyokuwa kazini hivyo ukiachia kampuni binafsi kusimamia mbolea utakwamisha kilimo wakati wa majanga kama huna chombo cha kukituma na kukitumia.
Pia TFC ikisaidiana na wadau wengine inashiriki katika uhamasishaji wa matumizi bora ya mbolea.
Kanjel Mloba |
PANORAMA:
Kulingana na mwenendo wa mambo ulivyo sasa? TFC ni imara kiasi gani kuweza kutekeleza majukumu yake?
KANJEL:
Hapa labda nianze kwa kusema kinachohitajika ni kuiimarisha TFC. Unajua kila mwekezaji anakuwa comfortable akifanya kazi na Serikali.
Hivyo TFC inajiuza na ni chombo muhimu sana katika mustakabali mzima wa usalama wa chakula na ukuaji wa kilimo kwa ujumla.
Sasa kwa TFC changamoto kubwa inayokabiliana nayo ni kupata mtaji wa kutosha kuingiza mbolea wakati wa low season na kuwa na reserve (akiba) ya kutosha ya mbolea.
Ukipatikana wa mtaji na changamoto zingine zote zinazoikabili TFC zitaisha, mfano madeni. Tuna reschedule na kuyalipa yote n.k
Mimi naamini pamoja na misukosuko ya hapa na pale lakini TFC bado ipo imara na bado ni tishio kwa makampuni binafsi. TFC ni chombo muhimu kwa Taifa, nasisitiza tena na hii ni kwa sababu katika kipindi cha uhai wake wote, TFC ilijiimarisha kimiundombinu ikiwa na ofisi namaghala yenye uwezo wa kuhifadhi kiasi kikubwa cha mbolea, karibu kila kanda nchini.
Na huo ndio uimara wetu. Hakuna kampuni ya mbolea yenye maghala mengi na makubwa kama TFC, ndio maana wengine wanatuogopa sana. Kuwapo kwa TFC ni faraja kwa wakulima kwa kuwa wakulima wana matumaini makubwa na TFC, wanafahamu kuwa sisi ni sehemu ya Serikali na Serikali ipo kwa ajili ya wananchi.
Wananchi wengi wanaifahamu TFC na wanaipenda sana, wana imani kuwa mbolea bora na ujazo sahihi ni ile inayouzwa na TFC na pia wanamini hupatikana kwa bei nafuu.
PANORAMA:
Hivi sasa TFC inajiendeshaje?
KANJEL:
Kwa sasa Serikali inaangalia jinsi ya kuiwezesha TFC iweze kufanya majukumu yake ya msingi ipasavyo. Kampuni inafanya biashara kama kampuni nyingine binafsi zinavyofanya. Na kwa kuwa biashara ya mbolea ni ya msimu huwa pia tunapangisha maghala yetu na kujiingizia kipato pale msimu wa mbolea unapoisha.
TFC inahangaika kupata mtaji ili iweze kupata mbolea kwa bei nafuu zaidi ili iweze kumuuzia mkulima kwa bei rahisi zaidi na hatimaye kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
PANORAMA:
Nini chanzo cha hali ya TFC kukosa mtaji?
KANJEL:
Baada ya kitengo cha biashara kuanzishwa, mali zote ziliuzwa na PSRC. TFC ikapewa jukumu la kulipa wafanyakazi waliopunguzwa kiwandani.
Mwanzo TFC iliwekwa PSRC hivyo ilikuwa sokoni kwa kifupi. Lakini mwaka 2005 ikatolewa PSRC baada ya kuona umuhimu wake ikawa recategorized. Kutoka hapo TFC ikaanza kufanya biashara ikikopa toka mabenki ya biashara na ikijiendesha katika ushindani na(equal treatment) na makampunibinafsi. TFC iliweza kufanya vizuri hadi mwaka 2008.
Mwaka 2008, bei ya bidhaa za petrol ilipanda sana duniani na kusababisha bei za mbolea duniani kupanda sana kuliko wakati wowote katika historia. Kwa mfano bei ya Urea ilifika Dola za Marekani 820 FOB kwa tani ikilinganishwa na 350 msimu 2007\2008 na DAP iliuzwa kwa Dola za Marekani 1,300fob kwa tani ukulingansha na Dola za Marekani 500 msimu wa 2007\2008.
Serikali kwa kuliona hili na kwa kutambua uwezo mdogo wa makampuni yanayoagiza nakusambaza mbolea nchini na kuogopa nchi kukumbwa na baa la njaa kutokana na usalamamdogo wa chakula, iliamua kutoa dhamana kwa Kampuni ya Mbolea Tanzania – TFC ili iweze kununua na kusambaza mbolea nchini.
Dhamana hiyo ilikuwa ya kuiwezesha TFC kununua Mbolea yote ya Minjingu phosphate (MRP) inayozalishawa na Kiwanda cha Minjingu Mines and Fertilizer Limited (MMFL) ambayo ni ya kupandia, Mbolea ya DAP kwa ajili ya kupandia maeneo ambayombolea ya MRP haitumiki (eneo ambalo udongo wake sio wa tindikali) na mbolea ya kukuzia aina ya Urea.
Mbolea iliagizwa kutoka nje mwezi wa Agosti na Septemba, 2008 ambapo bei zilikuwa juu sana. Kufika mwezi Oktoba na Novemba 2008, bei za UREA na DAP katika Soko la Dunia zilishuka ghafla kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani uliofikia kilele mwezi Novemba ambapo tayari TFC ilikuwa imekwisha ingia mikataba na wasambazaji wakati bei ikiwa kubwa kabla ya mtikisiko bei hizo hazikubadilika baada ya mtikisiko wa bei kushuka kutokana na mikataba hiyo ya ununuzi.
Wanunuzi binafsi walinunua mbolea za bei nafuu kwa haraka na kuanza kuuza. Kushuka kwa bei kuliathiri sana TFC na kwa bahati mbaya, kutokana na mtikisiko wa uchumi (economic crisis) tukalazimika kuuza mbolea kwa bei ya chini kabisa tofauti na tuliyonunulia baada ya kukopa. Huu ukawa ndio mwanzo wa TFC kutetereka sana.
Kwa bahati mbaya zaidi, wakati Serikali ikiweka mikakati ya kusaidia kampuni zilizokumbwa na mdororo wa uchumi (rescue package), TFC haikuingia kwenye mpango huo wa kusisimua hivyo TFC iliendelea kuwa na madeni yasiyolipika na hivyo kushindwa kukopesheka na kuwa miongoni mwa kampuni ambazo hazikopesheki.
TFC ikaendelea kujikongoja kwa kufanya kazi sawa na za udalali kwa kutumia miundombinu imara tunayomiliki kusambaza na kuuza mbolea za kampuni nyingine binafsi kwa kupewa faida kidogo sana.
Tulifanya hivyo kama njia mojawapo ya kujiendesha wakati tunapambana kulipa madeni yaliyokuwa yakitukabiri.
Ilifika wakati ili kuweza kushiriki katika kutekeleza sera za nchi na kuweza kujikimu, TFC ililazimika kukopa mbolea toka kwa washindani na kuuza kwa faidandogo sana.
Aidha, TFC iliweza kukopa kwa washindani na kuingiza mbolea kwenye ruzuku na pesa za ruzuku zimekuwa mara nyingi hazilipwi kwa wakati na hii imesababisha mikopo hiyo kuattaract interest kubwa na kuiletea mzigo kampuni.
Hivyo kwa mtindo huu TFC imekuwa na madeni yasiyolipika ambayo mengi yametokana na kutokulipwa kwa ruzuku.
TFC inaidai Serikali na mawakala zaidi ya Shilingi bilioni 5 za ruzuku ya mbolea iliyosambaza wakati wa sera ya ruzuku ya mbolea kwa wakulima tangu mwaka 2015.
Sasa msimu wa 2017/18 tulishindwa kabisa kufanya biashara kutokana na ukata. Januari, 2019 TFC ilihamishwa rasmi toka Wizara ya Viwanda na Biashara na kuhamia Wizara yaKilimo.
Kuna juhudi za Serikali zilizofanyika katika kuinusuru TFC mfano mwaka 2018, Serikali ilitoa bilioni 10 ili TFC iingize madawa ya Surphur ya unga ili iuzie Bodi ya Korosho.
Historia yake ni ndefu kidogo kwani TFC imepata changamoto sana katika mpango huo kwani haukuenda ulivyotarajiwa.
Kanjle Mloba |
PANORAMA:
Ni lini umeanza kukalia hiki kiti na nini mafanikio yako
KANJEL:
Ha ha mafanikio, labda naweza kusema nikuweza kuweka amani na matumaini kwa wafanyakazi waliokuwa wamekufa moyo kabisa kwani nilipokabidhiwa ofisi hali ilikuwa ngumu sana.
Tulikuwa hatujafanya biashara kwa muda na TFC ni Kampuni ya Serikali inayojitegemea hivyo wafanyakazi walikuwa hawapati mishahara, tulikuwa hatuna pesa za kujikimu kabisa.
Duniani kuna viongozi lakini namkumbuka Msajili wa Hazina wa wakati huo, Mtuka nilipata wasaa wa kumuelezea matatizo yetu kwa kweli aliyabeba kwa moyo wote na kuunda kamati ya kutathimini hayo matatizo yetu.
Pia Wizara ya Kilimo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo wakati huo, Kusaya alitubeba na matatizo yetu na kutupa moyo sana na tulipokwama alitusikiliza na kututatulia matatizo yaliyokuwa ndani ya uwezo wake. Kwa ujumla uongozi wote wa Wizara ya Kilimo walitusikiliza na kutujali sana.
Siwezi kusahau tulivyoshirikiana kutoa shehena ya madawa ya Salfa yaliyokuwa yamekwama bandarini. Najivunia kuwa katika hiyo timu nikiongoza utoaji wa hiyo shehena; pili naweza kusema kwa kushirikiana na viongozi wa tuliweza kufanikisha kuhamishia mishahara ya watumishi kuingia serikalini
Aidha, kwa kushirikiana na wizara kufuatia changamoto ya upatikanakji wa mbolea za kupandia DAP na za kukuzia Urea tuliweza kufanikiwa kupata vyanzo vya kupata mbolea hizo kwa bei shindani. pia kuweza kupata makampuni wazalishaji duniani ambao wapo tayari kufanya kazi na TFC na hasa kutuuzia mbolea kwa bei ya Cooparate.
Jambo moja hapa ambalo kwa uzoefu wangu katika ofisi hii naweza kulisema kwa uhakika kabisa ni kwamba Serikali inapaswa kuhakikisha kila muwekezaji anayetaka kuanzisha kiwanda, TFC iwe na hisa ili asije aka – monopolize na hatimaye kututawala maana mtu akimonopolize udongo tayari amewamaliza. Atakuwa anawapangia bei anazotaka. Serikali iimarishe chombo chakeTFC kiwe na nguvu ili kulinda kilimo cha Tanzania.
PANORAMA:
Umesema Rais alitoa Shilingi bilioni 10 lakini hamkupata hizo pesa, hapo ulimaanisha nini?
KANJEL:
Pesa hizo zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa madawa ya Salfa ya Unga ili kuwauzia Bodi korosho. Maana yangu ni kwamba hazikuja moja kwa moja TFC na hii imeleta usumbufu sana hata kusababisha kukwama kwa shehena ya Salfa ya unga bandarini.
PANORAMA:
Hiyo mbolea iliyokwama bandarini ilikwama kwa muda gani?
KANJEL:
Ilikaa miaka miwili bandarini.
PANORAMA:
Kuna wakati tulisikia kampuni binafsi ilipewa pesa hizo za Serikali ambazo zilitolewa na Raiskwa TFC?
KANJEL:
Kwa kweli hilo siwezi kujua.
PANORAMA:
Umesema pia kuwa mmekuwa na tatizo la kutopata mishahara kwa sasa hali ikoje?
KANJEL:
Kama nilivyoongea mwanzo tulilazimika kufanya vikao na Serikali kupitia kwa Msajili waHazina (TR). Kampuni hii ipo chini ya TR.
Tulienda kwa TR bila miadi akatupokea na nikamweleza shida tunazopambana nazo, akashangaa sana na siku hiyo hiyo akaunda timu kuja kufuatilia hali ya TFC ilivyo.
Nashukuru sana TR alielewa na hata wizara walielewa na kutusaidia kufanikisha hilo, sasa wafanyakazi wote tunalipwa mishahara kutoka Serikali Kuu, hivyo hatuna tena tatizo la mishahara kama awali.
PANORAMA:
Msimu huu wa kilimo kumekuwa na malalamiko ya kupanda kwa bei ya mbolea. Unadhani hali hii ingewezaje kudhibitiwa na kumpa nafuu mkulima?
KANJEL:
Kabisa. Hali hii ingeweza kudhibitiwa kwa TFC kuwa na mbolea. Pamoja na kwamba kupanda kwa mbolea kumetokana na madhara ya uviko 19 lakini nahisi kama TFC tungekuwa na mbolea bei isingefika huko.
Kwa kawaidaTFC ikiwa na mbolea bei haipandi! Tatizo ni pale sisi tusipokuwa na mbolea wafanyabishara wanapandisha bei watakavyo wao. Kwa hiyo ni muhimu Serikali isimame na kampuni yake hii ya mbolea ili kumsaidia mkulima.
Wafanyabiashara binafsi wa mbolea nchini wana nguvu sana hivyo ni lazima Serikali iamuekwa dhati kuwadhibiti kupitia TFC kwa manufaa ya Mtanzania na Kilimo cha TANZANIA.
Wanaofanya biashara hii wanajua kabisa mkulima anahitaji mbolea. Hivyo kama TFC haina Mbolea ni rahisi wao kuungana kwa makusudi na kupandisha bei kwa kujinufaisha zaidi. Ni jukumu la Serikali kusimama na wakulima kuwasaidia katika hali hii.
Biashara ya mbolea ni kama zimwi likujualo halikuli likakwisha. Biashara hii ina hitaji mtaji mkubwa na wafanyabiashara wa mbolea wana mtandao mpana.
Mbolea kama mafuta tunahitaji kuwa na reserve ya Taifa hivyo Serikali ifanye juhudi za makusudi kukiwezesha hiki chombo chake ili kiweze kutumika ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania.
Uzuri ni kwamba chombo kipo na niimara kabisa na kina mtandao mpana na brand name ambayo inapendwa sana na Watanzania wengi.
Jamani nawashukuruni sana naomba nikatekeleze majukumu mengine na karibuni siku nyingine tuzungumze mambo haya ya nchi yetu.