RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
KATIBU wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Kijiji cha Sulu, Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, Daniel Jilala (43) amejinyonga hadi kufa kutokana na hofu ya rangi halisi ya Rais Samia Suluhu Hassan na ile ya Mkuu wa Mkoa (RC) wa Simiyu, David Kafulila.
Taarifa za kujinyonga kwa Jilala zimethibitishwa leo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simuyu, ACP Blastus Chitanda ambaye ameieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa marehemu alijinyonga hadi kufa kutokana na msongo wa mawazo.
Kamanda Chitanda alisema kabla ya kujinyonga, marehemu Jilala aliandika ujumbe ambao aliuacha sehemu alipojinyonga na ujumbe mwingine aliandika kwenye simu yake ya kiganjani na kuwatumia baadhi ya watu wake wa karibu na kwa mpelelezi wa kesi yake.
Alisema marehemu Jilala alikuwa akichunguzwa kwa makosa mbalimbali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambayo taasisi hiyo ndiyo inaweza kuyaongelea.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, ACP Blastus Chatanda |
“Ni kweli alijinyonga juzi kutokana na msongo wa mawazo, kabla ya kujinyonga aliandika ujumbe ukaaucha na ujumbe mwingine aliandika kwenye simu yake ya mkononi akautuma kwa baadhi ya watu wake wa karibu na kwa mpelelezi wake.
“Marehemu alijinyonga hadi kufa kwa kamba na ujumbe alioucha ulisomeka kuwa amechoshwa na kesi zinazoendelea TAKUKURU ambazo haziishi hivyo akifungwa hajui watoto wake wataishi vipi hivyo ni bora ajinyonge asiwepo kabisa duniani.
“Inavyoonekana kuna mtu alikuwa akimuomba pesa ili kumsaidia kumaliza hizo kesi zake lakini hilo halikufanikiwa. “Marehemu alikuwa anachunguzwa na TAKUKURU hivyo wanaoweza kuzungumzia tuhuma zake na uchunguzi wa tuhuma hizo ni TAKUKURU.
“Sisi polisi baada ya kujinyonga kwake tulikuwa tunachunguza chanzo cha kifo chake kama kuna mtu anaweza kuwa alisababisha lakini kwa sababu imethibitika kuwa alijinyonga kutokana na msongo wa mawazo basi sisi hatuna zaidi hayo mengine tunawaachia TAKUKURU,” alisema Kamanda Chitanda.
Alipoulizwa Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Simiyu ambaye alikataa kutaja jina lake kuhusu tuhuma ziilizokuwa zikimkabili marehemu Jilala, alisema suala hilo ni kubwa linalohitaji uchunguzi wa kina na mwenye mamlaka ya kulizungumzia ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
“Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu kwanza kujiua ni jinai hiyo, halafu hapo hapo kunakuwepo na tuhuma za rushwa. Kwa hiyo ni lazima lifanyiwe uchunguzi wa kina na kuna mamlaka za kutoa taarifa ambazo kwetu TAKUKURU mwenye mamlaka hayo ni Mkurugenzi Mkuu.
“Hata ukinitafuta badaaye siwezi kukupatia taarifa yoyote labda baada ya uchunguzi wa tukio zima mtafute Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ndiyo anayeweza kutoa taarifa kwa waandishi kwa ajili ya kuufahamisha umma,” alisema kamanda huyo wa TAKUKURU wa Mkoa wa Simiyu.
Taarifa zilizoifikia PANORAMA Blog awali zilieleza kuwa Jilala mwenye (43) ambaye alikuwa Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Kijiji cha Sulu alijinyonga hadi kufa kwa sababu ya kutishwa na rangi halisi za Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kilichopo Mkoa wa Simiyu, marehemu Jilala aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Sulu, Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu alikutwa amejinyonga kwa kamba kwenye mti jioni ya Mei 27, 2022 kwa kuhofia kufungwa jela kutokana na kesi zinazomkabili ambazo zilianza kumuandama baada ya Rais Samia kumuagiza RC Kufulila kuwashughulikia bila huruma viongozi wa vyama vya ushirika wanaotafuna fedha za ushirika.
“Marehemu aliacha ujumbe kwenye simu aliomtumia afisa mmoja wa TAKUKURU ulioshiria kuwa muhanga wa oparesheni inayoendeshwa na RC Kafulila katika Mkoa wa Simiyu ya kusafisha uozo ndani ya ushirika ambayo ina baraka za Rais Samia.
“Simu ya marehemu ilikutwa na ujumbe aliomtumia mmoja wa maofisa wa TAKUKURU wa Wilaya ya Maswa uliosomeka;
“Nimeamua kujiua kwa sababu sijasaidiwa , naombwa rushwa kila siku na afisa ushirika (alimtaja jina) kuwa anawapelekea TAKUKURU mkoa lakini sioni matumaini ya suala langu na inaelekea nitafungwa, sasa sioni sababu ya kuishi kwani sijui wanangu wataishije ikiwa nitafungwa.“
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila |
Akizungumza April 4, 2022 mkoani Dodoma, baada ya kugawa pikipiki kwa maofisa ugani nchi nzima, Rais Samia alimwelekeza RC Kafulila kuendelea kudhibiti wizi wa pembejeo za pamba na michezo michafu kwenye vyama vya ushirika na ushirika.
“Nakuagiza Kafulila, endelea kuwakaba, najua wapo ambao mliowafungulia mpaka kesi za uhujumu uchumi kwa wizi wa madawa ya pamba. Nasisitiza endelea kuwakaba wezi wa pembejeo na ushirika wote tena kwa hatua kali mpaka wazijue rangi zangu,” aliagiza Rais Samia.
Tayari RC Kafulila amekwishawaondoa maofisa ushirika wote wa ngazi ya wilaya na kuelekeza wapangiwe kazi zingine kwa kile alichokieleza kuwa maafisa hao ni sehemu ya udhaifu wa usimamizi wa ushirika na hujuma kwa wakulima wa pamba.