RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
TANZANIA ina viwango cha chini vya bei ya umeme kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Simiyu, David Kafulila alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa mapokezi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo katikia Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu.
Alisema takwimu za ulinganisho wa bei ya umeme kwa nchi za Afrika Mashariki zinaonesha kwa wastani Watanzania wanatozwa bei chini ya umeme kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.
Kafulila alisisitiza kuwa nafuu hiyo ya bei ni kielelezo kuwa Serikali iliyoko madarakani inawajali wananchi wake.
“Jana serikali imetoa bei mpya za mafuta zenye punguzo la takribani shilingi 300 kwa lita kama mkakati wa kupunguza makali ya bei za bidhaa. Serikali itaendelea kuchukua hatua ili kupunguza makali ya gharama za maisha nchini.
“Tuelewe tu kwamba mbali ya mkakati huo kwenye mafuta, pia ni sera ya Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati ya umeme kwa bei nafuu zaidi.
“Takwimu za ulinganisho wa bei ya nishati ya umeme duniani zinaonesha kwamba wakati bei ya umeme Tanzania, wastani ni Dola za Marekani senti 10, Kenya ni Dola za Marekani senti 21, Uganda Dola za Marekani senti 18 na Rwanda ni Dola za Marekani senti 26.
“Hii maana yake wananchi wa Kenya wananunua umeme kwa bei kubwa mara mbili ya wananchi wa Tanzania. Na zaidi tunafahamu sera ya Serikali kuhakikisha watu wa kipato cha chini wanapata nishati ya umeme.
“Kwamba wananchi wanaotumia sio zaidi ya unit 75 kwa mwezi wanalipia unit 1 ya umeme kwa shilingi100. Yote hii ni namna ya kujenga maendeleo yanayobeba watu wengi,” alisema Kafulila.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa awalitaka Watanzania kutambua juhudi za Serikali katika maisha yao hata kama bado kuna changamoto kwani Serikali inazitambua na inaendelea kukabiliana nazo kwa vitendo.