RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WATU 20 jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakishtakiwa kwa kosa la mauaji.
Washtakiwa hao walisomewa shtaka la kumuua kwa kukusudia Askari Polisi Garlus Mwita Garlus (36) huko Loliondo.
Garlus aliuawawa Juni 10, 2022 kwa kuchomwa mkuki na watu wasiojulikana wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi ya kulinda usalama kwenye kazi ya uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 ambalo limetengwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi, vyanzo vya maji na mazalia ya wanyama.
Washtakiwa hao ambao taarifa zinaeleza kuwa walifikishwa mahakamani katika hali ya usiri mkubwa ni Malongo Daniel Paschal (21) mkazi wa Ololosokwani, Albert Kiseya Selembo (37) mkazi wa Soitisambu, Sineli Parmwati Korongoi (19) ambaye ni mwanafunzi na mkazi wa Ololosokwani, Lekayoko Parmwati Sirikoti (21) mkazi wa Ololosokwani na Sapati Parmwat Sirikoti mkazi wa Ololosokwani.
Wengine ni Ingoi Olkedenyi Kanjwel (21) mkazi wa Soitisambu, Sangau Morongoti Ngiminisi ambaye umri wake haufahamiki na mkazi wa Soitisimbu, Marijoi Ngoisa Parmati (20) mkazi wa Ololosokwan, Morongeti Meeki Masako ambaye umri wake haufamiki na mkazi wa Ololosokwani, Kambatai Lulu (40) mkazi wa Ololosokwani na Moloimeti Yohana Saingeu (37) mkazi wa Ololosokwani.
Watuhumiwa wengine ni Ndirango Senge Laiza (52) mkazi wa Orgosorok na Joel Clemes Lessonu (54) mkazi wa Malambo
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani na baada ya kusomewa mashtaka walipelekwa Gereza Kuu la Kisonga kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.