Friday, September 12, 2025
spot_img

KAMATI: WALIOMTOROSHA MWANAFUNZI ST. MARY’S WAKAMATWE, WAHOJIWE, WASHTAKIWE

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC) Daniel Chongolo

RIPOTI (3)

MWANDISHI WA PANORAMA

Novemba 6, 2020, mwanafunzi Lubna Salim Said wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari St. Marys iliyopo eneo la Mbezi, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam aliripotiwa na wazazi wake kutoweka shuleni katika mazingira ya kutatanisha huku uongozi wa shule hiyo ukiwa umeficha siri ya tukio hilo.

Wazazi wa Lubna waliripoti tukio hilo Kituo cha Polisi Stakishari na Novemba 18, 2020, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Daniel Chongolo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni aliunda Kamati Maalumu ya kuchunguza tukio hilo lililoghubikwa na usiri mkubwa na kunyamaziwa na vyombo vya habari na katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog, DC Chongolo alisema Serikali haitalala mpaka mwanafunzi huyo atakapopatikana na itatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu sakata hilo.

Tanzania PANORAMA Blog ambayo ndiyo pekee iliripoti tukio hilo na kuendelea kulifuatilia kwa karibu ilielezwa na wajumbe wa Kamati ya DC Chongolo kuwa wakati wa uchunguzi wao walibaini mambo mazito ikiwemo nyumba ya kamanda wa juu wa Jeshi la Magereza iliyozungushiwa ua, ndani ya ua huo kulikuwa kukifanyika kilimo cha bangi na vijana waliokuwa wakiishi humo walikuwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Aidha, Tanzania PANORAMA Blog lilielezwa kuwa mwanafunzi Lubna alitoroshwa shuleni na mtoto wa kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Magereaza na kupelekwa katika nyumba hiyo ambako alivutishwa bangi, kufanyishwa kazi za ndani na kuingiliwa kimwili.

Ikiwa ni takribani miezi sita sasa tangu tukio hilo lilipotokea na DC Chongolo kuunda Kamati Maalumu ya kulichunguza, haijapata kutolewa taarifa yoyote ya uchunguzi huo na ripoti hiyo haijawasilishwa kwake licha ya kamati kukamilisha uchunguzi wake Disemba 15, 2020, ambao ulifungiwa kabatini.

Tanzania PANORAMA Blog limefanikiwa kuiona ripoti hiyo ya uchunguzi na hapa linaichapisha neno kwa neno. Hii ni sehemu ya tatu na nne. 

TAARIFA YA KAMATI MAALUM YA MKUU WA WILAYA YA KINONDONI KUCHUNGUZA TUKIO LA KUPOTEA KWA MWANAFUNZI LUBNA SALIM SAID WA SHULE YA SEKONDARI ST. MARY’S HIGH SCHOOL, MANISPAA YA KINONDONI – DAR ES SALAAM

Mwanafunzi Lubna Said


SEHEMU YA TATU 

3.0      HITIMISHO

Baada ya kufanya uchunguzi kwa kina, kukagua eneo la tukio, kufanya mahojiano na watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi na wanafunzi wa shule hiyo, kamati hii imebaini na kuthibitisha kwamba.

i.Chanzo cha tutio la kutoroka kwa mwanafunzi LUBNA SALIM SAID katika Shule ya Sekondari St. Mary’s High School ni kutokana na usimamizi usioridhisha wa mlezi wao (Matron).

ii. Kiwango cha usalama katika shule hiyo siyo cha kuridhisha kutokana na kuwa na mwingiliano wa watu wasio wanafunzi wanaoingia na kutoka bila sababu ya msingi.

iii.Ukiukwaji wa sheria za uendeshaji na usimamizi wa shule hiyo kwa kulaza wanafunzi katika vyumba visivyo na hadhi ya kuwa bweni, malazi ya namna hiyo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi. 

 

 SEHEMU YA NNE

 4.0 4.0 MAONI/ MAPENDEKEZO YA KAMATI


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo


Uendeshaji wa taasisi zinazotoa huduma kujumuisha watu wengi kama vile shule, vyuo na ofisi zina wajibu wa kuzingatia taratibu, miongozo na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Kufanya kinyume cha sheria zilizowekwa ni kuhatarisha usalama wa maisha, mali na afya za wahitaji na watoa huduma katika eneo husika, jambo ambalo pia ni kosa linalohitaji kuchukuliwa hatua.

Aidha mbali na ukiukwaji huo, kuna tishio la kiusalama na kiafya, lakini pia unafanya mamlaka zinazohusika na umiliki wa taasisi husika kupata hasara za mali na vifaa mbalimbali.

Kwa hiyo ili kuepuka athari zitokanazo na ukiukaji wa taratibu, miongozo, kanuni na sheria kamati inapendekeza yafuatayo;

i.Kamati inashauri shule zitakiwe kuweka utaratibu madhubuti wa usimamizi na uratibu wa shughuli zinazohusisha muingiliano wa wanafunzi na jamii inayotoka nje shule kwa lengo la kiusalama.

ii.Kamati imependekeza wanafunzi wote waliojihusisha kwa namna moja au nyingine katika kumtorosha LUBNA SALIM SAID wachukuliwe hatua za kinidhamu ili iwe fundisho.

iii.Kamati inashauri kufungwa kwa kamera katika maeneo ya shule ili kufanya utambuzi na kufuatilia mienendo ya watu wanaoingia na kutoka katika shule hiyo ili kuimarisha usalama.

Kutokana na ushahidi uliotolewa na ukaguzi uliofanyika hasa maeneo ya tukio (shuleni na nyumbani), kamati imejiridhisha kuwa tukio hilo limesababishwa na malezi duni na usimamizi usioridhisha kwa wadau wote (wazazi, walimu, na walezi).  Hivyo basi kamati inashauri vyombo vya usalama kufuatilia kwa kina ili kuweza kukamatwa, kuhojiwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na tukio hilo.


 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya