Friday, September 12, 2025
spot_img

RAIS SAMIA KUWAKILISHWA NA RAIS MWINYI NI DHAMBI?

 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

NA ABBAS MWALIMU

0719258484

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tumepokea maswali mengi kutoka kwa wadau wetu wakitaka kufahamu itifaki imekaaje kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa SADC nchini Msumbiji.

Tukumbuke kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliondoka Zanzibar Jumatano Aprili 7, kuelekea nchini Msumbuji kumuwakilisha Rais Samia katika mkutano wa SADC,  kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ukanda huo na  hasa masuala ya ulinzi na usalama na hatua za kukabiliana na vitendo vya ugaidi katika nchi za SADC.  

Ili kufahamu itifaki imekaaje katika hili la Rais Dk. Mwinyi kumuwakilisha Rais Samia ni vema kwanza tufahamu kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna mambo ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano. Fedha, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ni mambo ya Muungano.

Sasa tutazame katiba inasemaje?

Tukisoma ibara ya 34 (3) inaeleza kama ifuatavyo:

‘Mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara yatakuwa mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.’

Hapa tunaona kuwa masuala ya Fedha, Uhusiano wa Kimataifa, Ulinzi na Usalama yapo mikononi mwa Rais Samia.

Lakini je, Rais anawajibika kuyatekeleza peke yake masuala ya Muungano hata pale ambapo atahitaji kupata mwakilishi? Katiba inasemaje katika hili?

Ibara hiyo hiyo ya 34 ibara ndogo ya  4 inafafanua kama ifuatavyo: ‘Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, madaraka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa watu wengine wenye madaraka katika  utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.’

Sasa hapa tujiulize Rais Dk. Hussein hahusiki na Mambo ya Muungano, mfano hili la Uhusiano wa Kimataifa? 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi


Ibara ya 54, ibara ndogo ya kwanza tunaona kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametajwa kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri. Ibara hii inasomeka kama ifuatavyo:

54.-(1) Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote.

Kwa mantiki ya hapo juu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni kiongozi katika Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia masuala yahusuyo Jamhuri ya Muungano yakiwemo Uhusiano wa Kimataifa, Ulinzi na Usalama ambayo ameenda kumuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia kwayo.

Hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile ya Zanzibar ya mwaka 1984 sambamba na marekebisho mbalimbali, Rais wa Zanzibar anahusika moja kwa moja katika masuala ya Muungano kama haya ya Kimataifa, Ulinzi na Usalama ambayo amehudhuria nchini Msumbuji kumuwakilisha Rais Samia.

Na haya yamewekwa wazi pia katika ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo inasomeka kama ifuatavyo: 102.-(1) Kutakuwa na Serikali ya Zanzibar itakayojulikana

kama “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar” ambayo itakuwa na mamlaka katika Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Kwa mujibu wa ibara hii, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni msimamizi wa masuala yote yasiyo ya Muungano lakini pia anahusika katika mashauriano kwa mambo yote ya Muungano.

Na ibara hiyo hiyo ya 102  inakazia kama ifuatavyo:

(2) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii na katika ibara zifuatazo katika sura hii ya Katiba hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaundwa na itatekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na Katiba ya Zanzibar, 1984. Hivyo katiba ya Zanzibar pia imekazia mambo ya Muungano.

Lakini pia ni vema tukafahamu kuwa viongozi wa juu kabisa kitaifa (the top cream four) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapo wanne na hawa ni:

(1) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(2) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(3) Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

(4) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo basi, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar ni kiongozi wa juu kabisa kwa masuala yahusuyo Muungano na kikanuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania angeweza kumteua yeyote kati ya hao watatu lakini naamini kutokana na kwamba Rais Dk. Mwinyi aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na tukizingatia mkutano ule ulikuwa unajadili masuala ya Ulinzi na  Usalama basi imempendeza Mheshimiwa Rais kupeleka mwakilishi ambae anayajua vema masuala ambayo alihudumu kwayo kwa miaka mingi.

Bendera za nchi wanachama wa SADC


Hivyo basi, hakuna shida yoyote kwenye uwakilishi wa Rais Dk. Mwinyi nchini Msumbiji kwa kuwa kikao kile cha SADC kinahusu Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Ulinzi na Usalama ambayo ni mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba zetu zote mbili.

Zaidi, Rais Samia amefanya vema kupeleka mwakilishi ambaye alipata kuhudumu katika eneo hilo la Ulinzi na Usalama kabla ya kuwa Rais wa Zanzibar.

Kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

Uwanja wa Diplomasia- (Facebook|WhatsApp).

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya