Saturday, August 23, 2025
spot_img

KIKWETE ANAOGOPA, TUMTIE MOYO


Jakaya Kikwete

RAFIKI yangu Rais Jakaya Kikwete amekumbwa na woga mkuu kiasi kwamba sasa anajiogopa hata yeye mwenyewe.
Anaogopa kufanya mambo yaliyo ndani ya uwezo wake. Hali hii si nzuri, tunapaswa kumsaidia kuondoka nayo. Kwa pamoja tunapaswa kumtia moyo.
Tukimuacha, ataendelea kuogopa kwa kipindi kirefu. Atakuwa anaogopa kukutana na mimi rafiki yake, kisa, kiherehere changu cha kumwandama kili ahudhurie mdahalo wa wagombea urais. 
Atakuwa anaogopa kukutana na watu wanaomtaka sana kwenye mdahalo, na hasa atakuwa anaogopa kukutana na watu wenye akili. Sitaki jambo hili litokee. Sitaki tuwe na rais mwoga.
Ili kumsaidia kuondokana na hali hiyo ya woga, sote kwa pamoja tunapaswa kuungana, tuwe na kauli moja ambayo itamshinikiza kutusikiliza. 
Na kwa sauti hiyo moja tumkataze kuwasikiliza watu wawili, Yusuph Makamba na Abdurahaman Kinana kwa sababu wanampotosha. Wanamshauri ajiweke katika hali ya kipindi cha ujima. 
Wala hakuna haja ya kuwajadili kwa undani Makamba na Kinana kwa sababu tumekwishabaini kuwa hamtakii mema, wanataka aonekane ni wa kisoma cha watu wazima hivyo hata wadhfa wa urais aliupata kiujanja ujanja tu lakini hakustahili na hastahili. Kwamba licha ya kuhudhuria masomo pale mlimani, haieleweki kama alielimika kweli au vipi!
Makamba na Kinana wanataka Kikwete awaone ndiyo tegemeo la pekee la yeye kuingia Ikulu, eti bila wao Ikulu hawezi kuiona hivyo chochote wanachomshauri hata kama wengine tunakiona cha kipuuzi, ni lazima akikubali kama anataka msaada wao wa kumuwezesha kuendelea kukaa magogoni. 
Hili ni lazima tulikatae kwa sababu sisi ndiyo wenye uwezo wa kumbakiza hapo kwa kura zetu. Tukikataa, tutamfukuza Ikulu kwa kutompigia kura.
Tukimwacha akubaliane nao tutakuwa tunampoteza, tumpigie kelele awafukuze. Akishawafukuza kwa sababu tayari amekwishajawa na woga tumtie moyo kwa kumwelekeze kufanya haya hata kama yatamgharimu kiasi cha kukosa ukubwa anaoutafuta, lakini atabaki na heshima yake tofauti na kuendelea kuwa mtawala asiye heshimiwa na watu wake. 
Wakimuona wanamcheka na kumkashfu kuwa rais asiyekuwa na chochote kichwani ! Ikiwa hivyo, itakuwa aibu!
Ingawa jambo hili limezungumzwa mara nyingi na watu wengi mimi nikiwa mmoja wao. Kwa ni njema kabisa narudia tena kulizungumza ili kuulainisha moyo wa rafiki yangu uliopondeka pondeka kwa woga ambao hapaswi kuwa nao kwa sababu ninaamini kuwa anao ubavu wa kujenga hoja zenye mashiko kwenye mdahalo wa aina yoyote kulingana na historia yake kielimu na hata katika utumishi wa taifa letu na kimataifa.
Jambo la kwanza na la msingi tunalopaswa kufanya ni kumuombea kwa Mungu amjalie afya njema na kamwe asiwe na mawazo ya kutegemea nguvu za giza kumlinda. 
Akatae kwa nguvu zake zote kulindwa na mashetani hata kama anayemfikishia ujumbe huo wa kulindwa na mashetani awe ametumwa kutoka mbinguni. Katika hilo awe tayari kutofautiana na malaika kama ndiye atakayemfikishia ujumbe huo na mimi nitamuunga mkono.
Katika maombi yetu hayo tusisahau kusali ile sala ya kuomba asiwahofie washindani wake wa kiti cha urais. Awaone ni watu wa kawaida tu kama yeye ambao anaweza kukutana nao mahali popote katika tukio la aina yoyote.
Ajiamini kuwa anaweza kwani kipindi cha miaka mitano ya urais na kile cha miaka kumi cha uwaziri wa mambo ya nje si haba, kimemjengea uwezo wa kutosha kwa kushiriki midahalo ya kila aina ndani na nje ya nchi.
Inawezekana anawaza kama mimi kwamba kwenye mdahalo huo anaougopa viherehere wataibua hoja za serikali yake kushindwa vibaya kutekeleza ahadi zake, jambo ambalo ni kweli na yeye hana majibu yake. 
Issue za ufisadi na kila aina ya uchafu unaoelekezwa katika serikali iliyoko madarakani. Anaogopa kwenda mbele ya jukwaa la mdahalo kwa sababu hapo hakuna ujanja ujanja kama kwenye majukwaa ya kampeni, hivyo anaweza kujikuta akiumbuka.
Mimi napenda kumtia moyo kuwa hao jamaa wakiibuka na issue hizo, asiwe na haraka ya kuzijibu. Awaache watoe tuhuma na mashambulizi yote kisha yeye akubali, aseme, ndiyo serikali yake kwa kipindi cha miaka mitano imeshindwa kabisa kutekeleza ahazi zake, imeshindwa kumaliza tatizo la rushwa na hata kupambana na mafisadi. 
Aende mbele zaidi kwa kueleza kwamba kwa kutambua kuwa ameshindwa alikuwa na mpango wa kukaa kando baada ya kumaliza muhula wake wa uongozi wa miaka mitano. Lakini pamoja na kushindwa huko, ni yupi wa kumuachia ulaji alionao kwa sababu wote waliopo wanaonekana wana tamaa?
Maelezo haya hayatakuwa yanajibu maswali ya msingi bali yatakuwa yanahamisha kabisa mada nzima kwa kuwachanganya washiriki wote wa mdahalo. 
Rafiki yangu Kikwete, hii ni siri ninakupa na nakuomba uniamini. Watu wote wenye akili waliozoe kufikiri mambo magumu huwa wanachanganywa kwa mambo rahisi na mapesi kabisa. Profesa na Daktari wamezoe kufikiri vitu vigumu sasa ukiwapa vya huku uswahili, walah utawaacha tu! 
Na mimi siku zote ninapokutana na watu wa aina hiyo huwa nawachanganya kwa namna hiyo niliyoeleza, huwa nawasikiliza kwa umakini, nikiona wanaanza kuniacha, nawachanganyia mada, wanachanganyikiwa na kubaki wanabishana wenyewe kwa wenyewe bila kupata jibu sahihi. Hii ndiyo siri ya mchokonozi kuwa rafiki kipenzi wa wakubwa, wewe mwenyewe ukiwemo.     
Ili kuhalalisha ulichokisema, unaweza kutoa mfano mwepesi unaoeleweka vizuri kwa wapiga kura wa uswahilini waliochoka sana kimaisha kwa kusema kuwa, ni kweli unatambua serikali yako haikufanya vizuri, ukakiri kushindwa na kwamba unastahili kufukuzwa na wapiga kura. Lakini wakikufukuza, mbadala wako ni nani?
Ndani ya chama chetu hakuna, wote ni kama kondoo. Hakuna aliyejitokeza kuwania kiti chako ingawa wanajua ni kweli umeshindwa. Na walipopotoshwa na yule mfuga majini unayemsaidia vijisenti kidogo anapoumwa kuwa atakayekupinga atakufa, ndiyo kabisa wakaanza kuimba mapambio ya kukusafishia njia ya kuendelea kutawala kwa miaka mingine mitano. Huko wote hawana sifa.
Kwa wapinzani, sawa kuna Profesa na Daktari. Profesa anakubalika maeneo fulani na Daktari naye anakubalika katika maeneo fulani ingawa yeye anaonekana kutikisa zaidi. Lakini wote wanagombea utukufu mmoja hivyo lazima watagawana kura.
Zako ziko pale pale na kama zitapungua basi ni kidogo. Kwanini hawa kama nia ni kukuondosha madarakani wasiungane wakakung’oa kiurahisi badala ya sasa wanapopigana vikumbo wenyewe kwa wenyewe kutaka kupanga kwenye nyumba uliyopanga.  
Wote wanahubiri ubaya wa ufisadi, wote wana nia ya kuwaletea watanzania mabadiliko ya maisha, wote wanajua wewe umeshindwa ingawa unang’ang’ania kuendelea nadhani kwa sababu ya mapochopocho ya hapo Ikulu, sasa wameshindwa nini kuungana wakatekeleza nia yao moja kwa pamoja?
Hawa wana tamaa, hawafai. Mpaka hapo mbadala wako hajapatikana ndiyo maana heri uendelee kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano labda baada ya hapo atapatikana mbadala wako. 
Baada ya maelezo hayo mapesi kabisa naamini Profesa na Daktari watatoana macho kwa sababu ni hakika kwamba muungano kwa wapinzani ni ndoto na wewe rafiki yangu Rais Kikwete unajua. 
Hivyo ukishawamwangia upupu huo wewe utabaki ukipumua taratibu na kuwaacha wao wakishambuliana kwa maneno makali ya kwanini mmoja hataki kumuunga mkono mwingine hata kama amegombea na kushindwa kwa kipindi cha miaka 15 mfululizo. Hilo utakuwa umemaliza.  
Hussein Bashe
   
Ikitokea likaibuka swala la ubaguzi ambalo naamini litaingizwa kwa mgongo wa kuenguliwa kwa yule kijana wetu Hussien Bashe kwa sababu baadhi ya watu makini hapa nchini wameanzisha tabia nzuri ya kupinga maamuzi ya uonevu yanayotolewa na wakubwa dhidi ya wanyonge ambayo najua wewe haikupendezi ingawa wao wanaonekana hawajali hata kama itawagharimu aidha ajira zao au uraia wao, hapa napo inafaa kueleza ukweli kuwa jina lake lilikatwa kwa sababu hakuwa mwenzetu.
Kwamba ingawa ili mtu awe huru anapaswa kuwa mkweli, lakini ni muhimu ieleweke kwamba ukweli una mipaka yake ndani ya chama chetu. Tumefundishwa kuishi kikondoo, kukubali kila jambo tunaloambiwa na wakubwa hata kama ni la kipuuzi kupindukia pasipo kuhoji chochote. 
Ndani ya  chama chetu historia inaonyesha baadhi ya waliosimamia haki na ukweli dhidi ya uonevu na uongo wa wakubwa wamekuwa wakiishia pabaya ingawa watu wa aina hii hawaishi. Jambo linaloshangaza kweli!
Hivyo suala la Bashe kuvuliwa uraia kibabe na chama chetu kinachotawala kibabe liliamuliwa kibabe ili kumkomesha kutokana na tabia yake ya kusumbua wakubwa.
Kwamba wewe mwenyekiti ndiye uliyewaambia wakubwa wenzako katika mkutano ule kuwa bwana mdogo Bashe hafai kupitishwa kuwa mgombea ubunge kwa sababu ni msumbufu. Alikusumbua sana, yeye na wenzake kwenye mkutano wa kutatua mgogoro wa umoja wa vijana wa chama tawala huko Iringa.
Kwa sababu ya usumbufu wake na kwa sababu hakuwa tayari kuimba kale ka wimbo ka zidumu na kuvuma fikra sahihi za mwenyekiti wa chama Tanzania bara na visiwani, ulimchukia kuanzia Iringa hadi Dodoma ulipoongoza kukata jina lake kwa kumsingizia kuwa si raia! 
Ni vema watu wakaelewa kuwa mkubwa ni mkubwa, hata akikosea hairuhusiwi kushinda naye bali kukubali hata hayo makosa yake, hivyo Bashe alipaswa kukubali yote ya kipuuzi na yasiyo kuwa ya kipuuzi aliyokuwa akielekezwa na wakubwa. 
Sasa alipojifanya kujua kibaya ni kipi na kizuri ni kipi hapo ndipo alipoharibu. Na hiyo ndiyo sababu ya kumnyima nafasi ya kugombea ulaji kwa kisingizio cha uraia.
Inawezekana pia suala la Salma likaibuka manake waswahili wameshaanza kushapalia matanuzi yake. Kwa mtizamo wangu hapa napo ni rahisi kupangua hoja hii. 
Salma Kikwete
Likiibuka jambo hili ili kuondoa swali lolote la nyongeza, kwanza ni kukanusha maneno yote ya Kinana kuwa Salma analipiwa gharama na chama chetu kwani taarifa zilizopo zinadai kuwepo utata katika hayo malipo yaliyoelezwa na Kinana.
Halafu ni kuwaelewesha wanaohoji raha za Salma kuwa dunia inabadilika na kila mtawala ana staili yake ya kula nchi. Kama wakubwa wa zamani walikuwa wanawazibia ‘mawife’ zao kufaidi matunda yao ya ukubwa, kwako haiko hivyo.
Ni ruksa kwa Salma kujirusha kwa pesa za walalahoi hata kama baadaye atakuja kufikishwa mahakamani kwa kufaidi asivyostahili. Hayo ni matokeo.
Hapo jambo la kuweka wazi ni kuwa Salma baada ya kuingia Ikulu maisha yake yalibadilika kulingana na hali ya jengo lenyewe. Alibadilika kuanzia mwili, mavazi, usafiri wake na kila kitu. 
Hivyo mambo yote ya kuanzisha taasisi hata kama pesa inayopatikana anaibugia yote ni sawa kwani hayo ndiyo matunda ya ukubwa. Majuto yatakuja baadaye na hasa akiingia mpinzani madarakani jambo ambalo si rahisi hata kidogo kwa sababu ambazo ziko wazi kabisa na kila mmoja anazijua. Wakati mwingine ni bora kuweka mambo wazi ili kuondoa vijimaneno maneno. 
Na hawa viherehere walio kwenye ofisi za umma wanaomfuata fuata Salma kwenye matembezi yake eti kwenda kumpokea, hao ni kuwakana mapema kwa sababu hawakutumwa na mtu kumfuatafuata bali viherehere vyao na adhabu yao waweza itangaza hapo hapo kuwa katika serikali yako ijayo kama utafanikiwa kushinda uchaguzi, hawatakuwa na kazi kwa sababu kwanza wanamnyima uhuru wa kujitanua. 
Jambo lenye utata hapo ni hili la Salma naye kuanza kutoa maagizo kwa wakuu wa mikoa. Hapo sijui utajibuje? Katika hili atakuwa amekuangusha kwa sababu huwezi kusema ulimtuma amuagize yule jamaa hivyo alivyomuagiza, nadhani inabidi kumrekebisha kidogo. Ale tu raha za wavuja jasho la damu lakini asiingilie kazi zako.
Mambo ya kipuuzi kwenye mdahalo, eti nyumba ndogo ziko!? Na upuuzi mwingine hayatakuwa na nafasi, hilo naomba ulielewe mapema na lisikunyime usingizi. Atayeibuka nayo huyo hatutamsikiliza na tutamuweka katika kundi la wapuuzi.
Ikiwa hivi, kwa namna yoyote mdahalo utakuwa mzuri sana kwa upande wako. Ni juu yako kutafakari na kuchukua hatua.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya