Tuesday, December 24, 2024
spot_img

‘POSTMORTEM’ YA KICHOKONOZI YA AKILI MBILI

 
Afande Barlow
 
AKILI mbili za binadamu wawili zimeuchanganya ulimwengu. Zimefanya uchunguzi wa maiti kwa kupeleleza sababu ya kufo na kutoa majibu tofauti.

Akili hizi mbili, zote zinasadikika kuwa zina akili, zinaaminiwa na walimwengu ndiyo maana wakazipa kazi hiyo nyeti ya kufanya uchunguzi wa maiti kwa kupeleleza sababu za kufa kwake.

Kwa maana nyingine, akili hizi mbili zinaaminiwa sanakwa sababu kufanya uchunguzi wa jambo kama hilo sio suala la mzaha.

Dosari iliyojitokeza ni kutoa majibu mawili tofauti katika uchunguzi wa maiti moja. Na katika uchunguzi huo hapo awali, akili hizi zilishirikiana kuifanya kazi hiyo na kuibuka na majibu yanayofanana lakini muda mfupi baadaye akili moja ikaibuka na majibu mengine tofauti.

Ni kwa sababu hiyo, Mchokonozi nimeamua kuzifanyia uchunguzi wa kupeleleza sababu ya akili hizo kutofautiana, kwa lugha ya kichokonozi ‘Postmortem.’ Naamini akili moja kati hizi haiko sawasawa, haina akili na inawezekana imekufa, ndiyo maana inatoa majibu mfu.

Nimeamua kufanya hivi ili kubaini ni akili ipi mfu na ipi iliyo hai na kwa watakaopenda watasoma matokeo ya uchunguzi huo ambayo nitayatangaza hadharani ili walimwengu wajue kuwa kuna akili mfu zinazoishi.

Kwa sababu hapa sio mahali pa majungu, nazitaja akili mbili ninazozichunguza; Ya kwanza ni ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, anaitwa Afande Liberatus Barlow na akili ya pili ni ya Daktari mwenye akili anayefanya kazi Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Daktari huyu mwenye akili nasikia anaitwa Kahigi, mimi simfahamu lakini sifa zake ninazisikia. Sasa asitokee punguani yoyote wa kuhoji inakuwaje ninafanya uchunguzi wa akili ya mtu ambaye simfahamu.

Ni jambo la kawaida kwa sababu akili ya mtu inaweza kuchunguzwa kutokana na matendo, kauli na hata kwa kudhani tu. Sasa kauli na matendo ya Daktari Kahigi viko mbele ya uso wangu, hali kadhalika Barlow, tayari kuvichunguza. Naanza:

Kwanza, ieleweke kuwa uchunguzi huu ninaufanya kwa mujibu wa taratibu za uchunguzi wa kichokonozi. Kwamba linapotekea jambo ambalo wachokonozi wana shaka nalo wana uhuru wa kulichunguza, kuhoji na kutoa maoni yao.

Mtu halazimishwi kuamini uchunguzi huu, ni maoni ya Mchokonozi ingawa ni uchunguzi makini mno unaofanywa kwa utaalamu wa hali ya juu kiasi kwamba hakuna sehemu itakayoachwa kuangaliwa na kutolewa majibu.

Pia, msingi wa kufanya uchunguzi huu ni baada ya kubaini kuwa wenye dhamana za kufanya uchunguzi kama huo sasa wanatofautiana. Kwamba inawezekana wameshindwa kazi au pengine walipewa kazi hiyo wakati hawastahili.

Kwamba labda bongo zao zina pumba zisizowawezesha kufanya kazi zinazohitaji utalaamu mkubwa lakini kwa sababu ni watoto wa shemeji au ni wakataji wazuri, basi walipewa kazi hiyo yenye maulaji ya kutosha inayowastahili wenye akili tu kwa upendeleo.

Jambo la kwanza ninaloliangalia katika uchunguzi huu ni uwezo wa akili ya kawaida  katika kupima mambo baina ya Afande Barlow na Daktari Kahigi.

Hapa ninachunguza akili zao kwa kuangalia jinsi walivyopokea tukio la mauaji lililopewa jina la ajali ya gari la mwandishi wa habari, Richard Masatu. Ninachochunguza ni kauli zao za awali kama zilikuwa zikikubaliana na ukweli kulingana na mazingira ya ajali au lah!

Tuanze na Afande Barlow; huyu baada tu ya mazishi ya Masatu, nilisikia kupitia kwa wachokonozi akieleza kuwa hawezi kuzungumza lolote kuhusu uchunguzi wa kikachero wa tukio hilo kwa sababu ni zito na la kusikitisha linalohitaji uchunguzi wa kina.

Hapa alikuwa sahihi, akili yake ilikuwa na akili nzuri tu tena ya kawaida ya kutambua tukio kubwa ambalo ili kulitolea maelezo ni lazima kwanza kufanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kuhusu kile ambacho kachero wa ngazi kama yake anapaswa kuutangazia ulimwengu. Hapa Barlow alikuwa na akili sana. Kamani maksi, basi alipata za kutosha.

Kwa upande wa Daktari Kahigi hapo hana maksi kwa sababu mpaka taarifa hizo zinanifikia nilikuwa sijapewa uchokonozi wowote kuhusu matokeo ya uchunguzi alioufanya kwenye mwili wa Masatu.

Sasa twende kwenye chumba cha uchunguzi, mahali ambako Daktari Kahigi alifanya kazi yake ya kuchunguza maiti ya Masatu na kueleza alichobaini na pia ofisini kwa Afande Barlow ambako alisoma ripoti yake ya kipelelezi kuhusu uchunguzi wa maiti ya Masatu.

Kutoka chumba cha uchunguzi Hospitali ya Bugando, taarifa zinaeleza kuwa Daktari Kahigi akiwa na polisi na watu wengine kadhaa, akifanya kazi yake ya kitalaamu kwa uwazi, alibaini kuwa maiti ya Marehemu Masatu ilikuwa imevunjwa vunjwa mifupa ya kifuani na kusagika. Hivyo haina shaka alipigwa pigo zito kifuani kisha akawa anakandamizwa na kitu kizito kifuani jambo lililosababisha damu nyingi kuvuja ndani ya kifua chake na kuganda.

Sina tatizo kabisa na taarifa hii kwa sababu kwanza ilifanywa kitaalamu tena mbele ya mashuhuda wakiwemo polisi. Daktari huyu anaonyesha jinsi alivyo mkweli na anavyojua kuchungza hata mifupa iliyosagika. Akili yake ina akili.

Kutoka ofisini kwa Afande Barlow, taarifa zinasema uchunguzi wake haukubaini jereha lolote sehemu za kifuani za maiti hiyo, isipokuwa katika ripoti hiyo, kuna kipengele kinachoeleza kuwa polisi walibaini michubuko katika mkono wa kulia na kushoto wa maiti.

Huu ni upuuzi. Mtu aliyefundishwa ukachero hadi akakubuhu. Aliyeahidi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kifo chenye utata, aliyetuma mwakilishi wake wakati maiti husika ikichunguzwa na mtaalamu wa miili ya binadamu mwenye akili na kuletewa matokeo yake, kushindwa kueleza ukweli kuhusu majeraha iliyokutwa nayo maiti kifuani ni upuuzi.

Hapa akili ya Afande huyu inadhihirisha kuwa haina akili kwa sababu inaficha ukweli wa kitabibu. Inashusha hadhi ya cheo cha Kamanda wa Polisi. Kwetu sisi wachokonozi, kwa hilo tunajiuliza kama kweli Barlow ni kachero au ‘mtoa taarifa tu.’

Tuendelee, turudi Bugando kwa Daktari Kahigi. Kutoka huko, taarifa zilieleza kuwa uchunguzi wa kitabibu uligundua kuwa maiti ilitobolewa jicho moja na kitu chenye ncha kali.

Taarifa hii wala haiwezi kutiliwa shaka kwa sababu hata mashuhuda waliomuona marehemu akiwa mahututi katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure nao walishakaririwa na vyombo vya habari wakieleza kuwa macho ya marehemu yalikuwa hayafunguki. Yalikuwa yamepakazwa gundi.

Hili Afande Barlow katika upelelezi wake hakuliona. Halimo katika ripoti yake. Akili yake inajaribu kumtuma kuficha ukweli ambao haufichiki. Hapa anadhihirisha jinsi akili yake isivyokuwa na akili kwa sababu ni akili mfu pekee ambazo haziwezi kuona ukweli au kufikiri ni kipi cha kuficha.

Daktari Kahigi pia alibaini kuwa maiti ya Masatu ilikuwa imepasuliwa bandama na mapafu. Hili hata kachero Barlow naye amelikiri katika ripoti yake ingawa kwa mashaka kwa sababu sentensi inayoeleza hilo imeongezwa katikati ya mistari, tena kwa mwandiko wa mkono. Hapa Barlow hakujiandaa kudanganya, hajui kudanganya. Kachero asiyejua kwamba hajui!

Uchunguzi wa kichokonozi wa akili ya Daktari Kahigi umebaini kuwa jamaa huyo ni miongoni mwa wasomi wachache ambao kwao kuuchambua mwili wa binadamu kulingana na utalaamu aliona ni jambo la kawaida mno na kwamba katika kazi hiyo kusema uongo kwa lengo la kupindisha ukweli ni mwiko.

Kuthibitisha hilo. Kutoka chumba cha uchunguzi huko huko Bugando Mwanza, anakaririwa akieleza kuwa uchunguzi wake ulibaini kuwa kichwa cha maiti ya Masatu kilipigwa pigo zito na kusababisha damu nyingi kuvujia ndani na kuathiri ubongo na sehemu nyinginezo baada ya kuganda.

Wakati Daktari Kahigi akithibitisha ubora wa akili yake kutokana na ripoti ya uchunguzi wake, Barlow naye aliendelea kuthibitisha kwa wachokonozi uhamnazo wake kwa kuwatangazia waandishi wa habari waoga wasio kuwa na uwezo wa kuhoji matamko tata na yenye kutia kinyaa kama hili alilokuwa akilitoa.

Huku akiamini unyonge wenye kudumaza akili wa waandishi waliokuwa wakimsikiliza. Akiwa katika mavazi ya ukamanda ninayoamini kuwa anayatia aibu, alisema upelelezi wake umebaini kuwa maiti ilikuwa na majereha na michubuko upande wa kulia wa paji la uso.

Kwa maelezo haya, haina shaka ninaweza kuwasilisha ripoti inayojitosheleza kwa wachokonozi kuwa kati ya akili hizi mbili, ya polisi Barlow na Daktari Kahigi, ya Barlow imeganda, haifai na kwangu mimi sio kosa kuiita mfu kwa sababu inafikiri na kutangaza mambo ambayo hayapo ingawa yanafanana kwa mbali na ukweli kwa lengo ambalo watu wenye akili hawalijui.

Hivyo kama uchunguzi huu ungekuwa unanitaka kuandika ripoti, ningehitimisha kwa sentensi moja tu ambayo ingesomeka hivi; Uchunguzi wa kichokonozi umebaini kuwa akili ya Daktari Kahigi iko makini na inafaa kuendelea kutumika. Lakini akili ya Afande Barlow haina akili, haifai na inapaswa kupumzishwa haraka kwa manufaa ya umma. Nimemaliza.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya