Tuesday, December 24, 2024
spot_img

CHONDE CHONDE MPENZI SPIKA MAKINDA

 
Makinda
 
SIKUPATA kufiriki hata siku moja kukujadili kwa heri au kwa shari kiongozi wangu mpenzi wa Bunge, Spika Anne Makinda kwa sababu ya kuhofia kukutia doa, wewe mwenyewe na kiti chako cha uspika.

Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana sikuwa na mpango wa kuhudhuria mkutano wa pili wa bunge la kumi ingawa ninawajibika kufanya hivyo.
Kwa wasiofahamu sababu ya mimi kuhudhuria vikao hivi bila kukosa, niwafahamishe kuwa mimi ni mbunge wa kulazimisha niliyejiteua mwenyewe kuwawakilishi wachokonozi wote wa Tanzania katika chombo chao hiki cha kutunga sheria.

Hata hivyo, nililazimika kufunga safari kuja hapa mjengoni Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kusikia kuwa wabunge fulani wamekuandikia barua wewe mpenzi Spika Makinda wakikuomba uangalie uwezekano wa kubadili kanuni za bunge ili nao wajumuishwe kwenye kambi rasmi ya upinzani bungeni ambayo walikuwa hawamo kwa sababu za msingi kabisa.

Sababu hizo sitazijadili hapa leo, lakini ninakuahidi kwa upendo mkubwa kuwa nitaziweka bayana sababu zangu za kutounga mkono ushirikiano huo wa wapinzani bungeni kwa sasa. Nakuomba vuta subira kwa sababu sasa utakuwa ukinisoma kila mara.

Niliposikia kwamba baadhi ya wabunge hasa wa chama chetu wanashabikia sana mabadiliko hayo, nilipagawa kwa hasira. Nilitamani niwepo mjengoni ili nitumie nguvu yangu ya ushawishi kubadili mwelekeo wa upepo huo wa mabadiliko ya kanuni lakini kabla hata sijaanza maandalizi ya safari yenyewe, kanuni zikawa zimebadilishwa.

Kubadilishwa kwa kanuni kulinifanya niamini kuwa kuna mengi yatakayotokea yanayohitaji uwepo wangu mjengoni. Na hasa nilijua kuwa katika kipindi hiki wewe mpenzi Spika Makinda utakuwa unahitaji sana msaada wa mawazo yangu ili uendelee kutekeleze majukumu yako vema.

Ninatambua kuwa wewe ni gwiji wa shughuli za bunge lakini ninaamini kuwa unaamini katika imani yangu kuwa huwezi kuwa unajua kila kitu, hivyo pamoja na ugwiji wako bado unahitaji msaada wa mawazo na ushauri kutoka kwa watu wengine, mimi nikiwa mmoja wa watu hao.

Mpenzi Spika, niharakishe kueleze mapema kuwa neno mpenzi ninalolitumia hapa halina maana yoyote mbaya, bali lina maana moja tu ambayo haina tofauti na ile ambayo huwa ninaimaanisha ninapomtaja mpenzi marehemu mama yangu, Agnes Batendi Simba.

Nadhani hapo umenielewa vema na kama kuna mpuuzi yoyote hasa kutoka chama chetu atayekuja kukuletea umbea eti unihoji kwanini ninakuita mpenzi! Naomba unijuze jina lake ili nikutane naye nikiwa na kamusi sanifu ya Kiswahili cha kisasa inayoeleza kwa mapana na marefu maana ya neno mpenzi. Nakusihi usinifiche kwa sababu najua tunao wapuuzi wengi ndani ya chama chetu!

Sasa tuendelee; kwa masikitiko makubwa mpenzi Spika Makinda, naomba nikueleze kuwa sijafurahishwa hata kidogo na staili yako ya ukali na kukoroga mambo mara kadhaa, tena nadhani umekuwa ukifanya hivyo kwa makusudi katika kipindi hiki kifupi ambacho umekuwa katika kiti hicho cha uspika.

Umekwenda kinyume na matarajio yangu na kwa staili hii sina shaka hata kidogo kuwa utayumba na ni mtizamo wangu kuwa utaliyumbisha bunge.

Nakusihi usikasirike kwa maandishi yangu haya yaliyojaa ukweli na hekima kubwa kwa sababu binafsi huwa ninakuelewa hivyo kutokana na staili ya uzungumzaji wako na jinsi unavyowashushua wenzako hata kama ni mbele ya kadamnasi.

Ulianza kunichanganya siku ya uchaguzi wa wawakilishi wa bunge katika bunge  la SADCC kwa makusudi tu uliamua Sophia Simba asijieleze kama walivyofanya wabunge wenzake.

Sophie Simba

Hata John Mnyika, Mbunge wa Ubungo aliposimama na kuomba mwongozo wako kuhusu jambo hilo hakuwa tayari kukubali ukweli kwa maelezo kuwa amechelewa kueleza jambo hilo.

Nikueleze jambo baya kabisa ambalo sikutaka kulieleza hapa kuwa kwa kitendo chako hicho, wapo wapuuzi fulani ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiamini kuwa ung’eng’e unampiga chenga Simba, siku hiyo walijua kuwa ni kweli na ndiyo sababu ukaamua kumnusuru kwa sababu lugha iliyokuwa ikitumika kujieleza ni kimombo.

Kwa tunaofuatiliaji shughuli za bunge tulijua fika kuwa hapo ulicheza faulo lakini kwa sababu ya imani yetu kwako tulikaa kimya kwa kudhani kuwa huenda ulipitiwa au kwa makusudi uliamua kumuokoa na aibu ya kutojua kuongea vema kiingereza Mbunge Simba kama ambavyo imekuwa ikivuma huko uswahilini kwetu wachokonozi.

Mnyika

Baada ya hilo, limekuja hili la kubadili kanuni ambalo wewe juzi ulisema si kubadili bali kutoa ufafanuzi ili tu wapinzani wetu ambao kwa sasa wanatofautiana kwa mambo kadha wa kadha wakae sehemu moja bila kujali kuwa jambo hilo litazidi kudhoofisha nguvu zao na hivyo kushindwa kabisa kuisimamia serikali yetu vizuri hasa katika kipindi hiki inaponuka kwa tuhuma mbalimbali.

Mpenzi Spika Makinda, binafsi kama wachambuzi wengine walivyokwishaeleza, sioni sababu iliyolazimisha sana watu hawa kuunganishwa kwa ulazima sasa. Kama ndiyo taratibu za mabunge yote ina maana hapo zamani mlikuwa hamjui? Kwa nini iwe sasa ambapo chama kilichotutikisa sana kwenye kampeni ndiyo kimepata fursa ya maulaji katika kambi hiyo?

Na ni kwanini wabunge wa CCM walikuwa wakishabikia sana mabadiliko hayo? hivi kama kweli mabadiliko yalikuwa na umihumu kiasi hicho ili hata wabunge wengine wa upinzani waweze kugombea nafasi za uenyekiti wa kamati za maulaji za bunge. Kwanini sio lazima na hailazimishwi kama ilivyolazimishwa kwenye uenyekiti wa kamati za bunge kuteuliwa pia wabunge wa vyama vingine vya upinzani kwenye baraza la mawaziri kivuli?

Katika akili ya kawaida, hata kama unayo mamlaka ya kubadili kanuni kadiri unavyotaka, hapa ni rahisi mtu kuamini kuwa uliridhia jambo hili kwa maslahi ya chama chako!
   
Mpenzi Spika Makinda, hayo yote tisa, jambo lililonichefua zaidi ni hili la juzi ulipokuwa ukizungumzia makala ya uchambuzi iliyochapishwa katika gazeti la mwananchi ambapo mwandishi alikuwa akielezea maoni yake kuhusu staili yako ya uongozi katika chombo hiki.

Kwa waliokusikia na kukutizama wakati ukitoa tamko kuhusu makala ile nadhani watakubaliana na mimi kuwa hasira zako hazina simile na kwamba huna uelewa wa uandishi wa habari.

Ni mapema mno kuanza kukuingiza darasani kukufundisha maana ya habari, maoni ya mhariri, makala za mahojiano, uchambuzi wa magwiji wa nyanja mbalimbali, habari za michezo na burudani, mashairi na hata barua za wasomaji kwa sababu sitaki kukushushia heshima yako.
Lakini ningependa uelewe kuwa uandishi wa habari ni fani pana sana tofauti na inavyofikiriwa na wengi wakiwemo baadhi ya wabunge na nadhani hata wewe mwenyewe. Uandishi wa habari ni fani iliyotukuka na yenye heshima kubwa ingawa imekuwa ikichafuliwa na wapuuzi wachache.

Nikudokeze kwa maneno mapesi kabisa ambayo ninaamini itakuwa rahisi kwako kuelewa kuwa mchambuzi yule aliyekuchambua katika uchambuzi wake ule, alikuwa akielezea maoni yake kuhusu namna unavyoliendesha bunge, ule haukuwa msimamo wa gazeti la mwananchi. Jambo hili linaruhusiwa katika taaluma ya habari. Nakueleza kwa ufupi kwa sababu ya ufinyu wa ukurasa huu.

Mpenzi Spika Makinda, wewe bila kujua kuwa gazeti la mwananchi halikukiuka taratibu zozote za kiuandishi, ulipaza sauti kwa watanzania wote ukitaka wawe wanalisoma gazeti hilo kama wanavyosoma barua!

Hii ni dharau! na nikuonye mapema kuwa kwa staili hii, wachambuzi mbalimbali wa mambo kupitia vyombo mbalimbali vya habari hawatakuacha, watakuchambua ili uendelee kukasirika. Na ukikasirika sana utaharibu kazi na ukiharibu kazi utaonekana hufai. Kama unabisha endelea na utaratibu wako wa sasa hakimu wako atakuwa muda kadiri unavyosonga mbele.

Ni muhimu pia uelewe kuwa kama wewe una hasira au hutishwi na yeyote katika kueleza jambo linalokukera, wapo pia waandishi wenye hasira kukuzidi wewe na wasiotishwa na mtu yeyote ukiwemo wewe Mpenzi Spika Makinda wanapokuwa wamekerwa na jambo ambao kwa hakika ni la kipuuzi.

Hawa huwa wanaandika maandishi makali ya kuonya na kukosoa kama ninavyofanya hapa. Wala hawaji bungeni kwa hisani ya Spika au wabunge bali ni sehemu ya kazi yao hivyo hawalazimishwi na yoyote kuandika kulingana na utashi wa Spika au washirika wake, bali kulingana na sheria na taratibu za kazi zao.

Ninachotaka kukuaminisha mpenzi Spika Makinda ni kwamba ingawa mimi si mwandishi wa gazeti la mwananchi, lakini kwa maoni yangu, nina uhakika usio na mashaka kabisa kuwa gazeti hilo ni moja ya magazeti makini katika kazi zake hivyo si rahisi kwalo kuandika makala na hata habari yoyote yenye lengo la kukuchafua wewe mpenzi Spika na hata wabunge wenzako.

Umakini wa gazeti hilo, ndiyo unaolilazimisha kuchapisha hata makala za uchambuzi zisizo kiuka maadili bila kujali kama zitakufurahisha au kukukasirisha wewe au mtu mwingine yoyote yule.

Mpenzi Spika Makinda, baada ya kukueleza hayo tena kwa mfumo wa barua kama unavyotaka wewe mwenyewe ili uweze kusoma, nimalizie kwa kukueleza kuwa haya ni maoni yangu binafsi kama mwanahabari, hayahusiani kwa namna yoyote na timu nzima ya mwananchi.

Ukipenda, yatafakari, usipopenda yatupe kapuni na yakakiudhi yatolee tamko bungeni kwa hasira, lakini ukifanya hivyo tambua sitakuacha, nami nitakujibu kwa hasira za kichokonozi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya