KWA kawaida fungate hudumu kwa muda wa siku saba. Hili ni fungate la kawaida baina ya wanandoa ambao ni mume na mke.
Kwa wachokonozi fungate ni mapumziko rasmi ya muda usiojulikana yanayolazimishwa na wakubwa ambao hushinikiza pande mbili zinazopingana kwa hoja na kutofautiana kimtizamo kuwa kimya kwa sababu ya woga wa kuumbuliwa na wakati mwingine kuepusha shari.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Mchokonoz.
Kabla ya fungate, Mchokonozi alikuwa daraja muhimu kati ya watawala na watawaliwa na zaidi alikuwa na kazi ya kuwachokonoa watawala kwa wakati muafaka na kwa staili nzuri inayofurahisha kuisoma lakini inayoumiza na kukasirisha wale wanaochokonolewa.
Fungate la Mchokonozi na watawala limedumu kwa takribani mwaka mmoja sasa. Limemalizika huku kila upande ukiutumia muda huo wa mapumziko kujipanga sawasawa kwa ajili ya kujishughulisha; na hii ni kwa sababu hakuna aliyekuwa tayari kwenda kwenye fungate hilo bali manguvu ya wakubwa ndiyo yaliyolazimisha liwepo.
Kumalizika kwa fungate hili ni mwanzo mpya wa shughuli za kichokonozi ambazo ndiyo msingi wa mapinduzi ya kweli ya kilimo, uchumi, utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, tiba, utawala, starehe na hata uhusiano binafsi baina ya mtu na mtu ambao kwa nyakati za sasa unapaswa kujengwa katika misingi ya kisasa zaidi kuliko ilivyokuwa miaka kadhaa nyuma kabla ya kuvumbuliwa kwa simu za mkononi zilizorahisisha zaidi mfumo wa mawasiliano.
Mwisho wa fungate ni mwanzo wa utekelezaji wa talaka baina ya Mchokonozi na watawala ambayo baada ya kuhalalisha utengano wao, itatoa uhuru mpana kwa watalaka kuishi maisha yao halisi wakisimama katika kile ambacho kila mmoja anakiamini.
Huu utakuwa muda muhimu sana kwa watanzania kwa sababu watapata fursa ya kusoma na kujifunza mambo mengi kutoka pande hizi mbili ambayo waliyakosa kwa muda mrefu.
Ni kawaida kwa talaka ya aina yoyote kutolewa ikiwa na sababu za msingi. Kwa hii inayotolewa na Mchokonozi inazo sababu kadhaa ambazo ninazitaja hapa chini bila mpangilio maalumu kwa sababu ndiyo utamaduni wa safu hii. Unaeleweka.
Ya kwanza ni kukithiri kwa kile kinachoitwa madudu yanayofanywa na baadhi ya wakubwa walioko serikalini. Katika kipindi cha fungate la Mchokonozi, wakubwa hawa wamekuwa wakitajwa kufanya mambo mengi ya ovyo ovyo ambayo lazima waliowachagua wajue ukweli wake ili wakasirike na hivyo wawanyime ulaji katika uchaguzi wa mwakani.
Moja kubwa ni hili la wizi wa mabilioni ya IPTL. Ni lazima wakubwa waumbuke kwa sababu kwa jinsi sakata lenyewe lilivyo inaonekana hawana pa kutokea.
Sakata la IPTL litaihalalisha talaka ya Mchokonozi kwa wakubwa kwa kuangalia jinsi wizi ulivyofanyika. Kama kweli Waziri msomi na Katibu Mkuu mfyatukaji nao walimeza mate.
Hawa watakuwa wa kwanza kufanyiwa kazi kwa sababu kauli zao katika sakata hili zina kila dalili za kutiliwa shaka.
Waziri msomi atachokonolewa kwa kushindwa kutoa majibu ya kuwaridhisha wachokonozi kuhusu wizi huo kulingana na kiwango cha usomi wake na badala yake kugeuka kuwa msema ovyo akiwa mahali ambako wengine hawawezi kusimama kumjibu ama kumuumbua kwa kauli zake.
Safu hii itashughulika naye kwa kumtendea haki kwa kadri ya maneno na matendo yake kulingana na wadhifa alionao.
Hana ubavu wa kuinyamazisha wala kupambana nayo na ikitokea akathubutu, kitumbua chake kitamwagiwa mchanga na usomi wake utapata doa.
Katibu Mkuu naye ataangaliwa kwa staili hiyo hiyo. Maneno yake ya hovyo hovyo yasiyoendena na wadhifa wake dhidi ya vijana wa kizazi cha kuhoji yataangaliwa kwa macho matatu ili kujua kiburi cha kipuuzi alichokionyesha mbele ya waandishi wa habari kinatokea wapi!
Siyo dhambi kumchunguza kwa sababu naye anadaiwa kuhusika na ukwapuaji huo. Kumchokonoa huyu ni rahisi kwa sababu anaonekana hana busara za kikubwa, ni mropokaji.
Ili kumlazimisha aseme ukweli, intelejensia ya kichokonozi itamuanzia mbali kwenye sakata alilohusishwa na ukware kisha ugawaji posho bila mpangilio kwa walionazo.
Bwana Sheria anayeamini katika ukale wa kuchapana makonde kavu kavu naye ataguswa katika uchunguzi huu.
Utakuwa ni uchunguzi huru utakaoangalia ni kwanini anapenda kusema maneno ya kuudhi dhidi ya wengine na kwanini akiudhiwa yeye anatishia kumkata mtu kichwa. Akikasirika na kukunja ngumu tena, atajiumiza mwenyewe kwa sababu atakuwa anapambana na upepo.
Sababu ya pili ni kuota mbawa kwa Katiba Mpya. Mchokonozi hawezi kuwa na ushirika na watu wanaohubiri kupatikana kwa Katiba mpya huku wakijua kuwa haitapatikana.
Rasimu ya Katiba mpya |
Atakachokifanya ni kuwaeleza walalahoi jinsi sheria ya mabadiliko ya Katiba ilivyofinyangwafinyangwa na Bunge la Katiba na wasiwasi walionao baadhi ya wana CCM wa kujadili rasimu ya pili ya Katiba kama ilivyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.
Tetesi zilizosambaa sasa kuwa kuna wakubwa wanaojipanga kupeleka kesi mahakamani kupinga mwenendo wa Bunge la Katiba unaosigina sheria ya mabadiliko ya Katiba zitashughulikiwa.
Mwenendo wa Mwenyekiti wa Bunge hilo, mwanasiasa mkongwe ambaye Mchokonozi hajapata kumuunga mkono utafuatiliwa kwa karibu na ukweli kuhusu Hati ya Muungano nao utawekwa bayana ili kuhalalisha talaka hii.
Sitajishughulisha hata kidogo na vijana fukufuku wenye tabia za ukitatange wa aina ya Ridhiwan kwa sababu hawana sifa za kujadiliwa katika safu hii isipokuwa kwa kumalizia nitashughulika kwa karibu na kiporo nilichokiacha mwaka jana cha mwenendo wa Idara ya Habari Maelezo.
Hapo nitachunguza kwa kina sababu za mkubwa wa idara hiyo kuniogopa kuliko mwajiri wake kiasi cha kusita kunipa karatasi ngumu ya serikali inayotolewa kwa wachokonozi.
Na kwa faida ya watanzania wote, nitachunguza na kuripoti neno kwa neno mradi wa mabilioni ya shilingi ambao mkubwa huyo anauwinda kutoka kwenye chama chetu ili kujua kama anastahili kuupata au lah!
Kwa umakini uliopitiliza na usioacha kivuli cha kushughulikiwa nitaangalia kama kuna harufu yoyote ya ufisadi kwenye mradi mzima na makandokando mengine yote yanayopaswa kuchunguzwa kwa mtu mkubwa serikalini lakini anayemuogopa mno Mchokonozi ili kuhalalisha mwisho wa fungate na mwanzo wa utekelezaji wa talaka.