Sunday, June 22, 2025
spot_img

WALIMU 7, WAFANYABIASHARA WATATU KORTIN KWA MITIHANI YA TAIFA YA DARASA LA SABA

Washtakiwa wa kuvujisha mtihani wa Taifa wa darasa la saba wakiwa mahakamani Kisutu, leo



RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

WALIMU saba na wafanyabiashara watatu leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kuvujisha mtihani wa Taifa wa darasa la saba wa mwaka 2022.

Washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani majira ya saa nane mchana na kusomewa mashtaka yanayowakabili na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Katuga amewataja washtakiwa hao kuwa ni Patrick Chawawa, Theresia Chitanda, Elinami Sarakikya, Joyce Nkomola , Lloyd Mpande, Olomy Odongo, Docras Muro, Alcherous Malinzi, Johnson Ongeka na Gladius Roman.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo, Wakili Katuga amedai kuwa kati ya Oktoba 2 hadi 12, mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walisambaza mtihani huo kupitia mitandao ya kijamii ya Whatsapp na Telegram na kusababisha mtihani huo kuvuja kwa watu ambao hawakuwa na mamlaka ya kuusimamia.

Wakili Katuga ameendelea kudai mahakamani hapo kuwa shtaka la pili na la tatu yanamuhusu mshtakiwa wa kumi, Malinzi ambaye katika tarehe hizo hizo jijini Dar es Salaam alitengeneza nyaraka za uongo kuonesha kama ni mitihani ya Taifa ya darasa la saba ya masomo ya uraia, maadili na maarifa ya jamii; kuwa mitihani hiyo ni ya halali na imetolewa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), wakati akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, washtakiwa wote wamekana kutenda makosa hayo na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi la dhamana lakini ni mshtakiwa mmoja tu, Mpande ndiye amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana huku wengine wote wakipelekwa mahabusu.

Mahakama imewataka washtakiwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh. Milioni tano.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wameiomba mahakama kuipangia tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ambapo imeahirishwa hadi Novemba 2, mwaka huu.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya