MACHI 2, 2018
NDEGE ZA SERIKALI ZATENGEWA BILIONI 11
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akiteremka baada ya kukagua mojawapo ya ndege za Wakala wa Ndege za Serikali alipotembelea wakala hiyo leo.
DAR ES SALAAM
Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) imetengewa Shilingi Bilioni 11.4 kwa ajili ya kuboresha huduma zake.
Akizungumza na Menejimenti ya TGFA jana, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa majukumu ya wakala hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye alisema Serikali inakusudia kuboresha huduma za TGFA.
“Serikali imetenga Shilingi Bilioni 11.4 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wakala ikiwemo matengenezo ya ndege, mafunzo kwa wanahewa na ukarabati wa karakana.
“Serikali inatambua umuhimu wa wakala hii na ina imani kubwa nanyi katika kuhakikisha kuwa mnafanya kazi zenu za kusafirisha viongozi kwa usalama na kwa uhakika ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi,” amesema Mhandisi Nditiye.
Mhandisi Nditiye aliieleza Menejimenti na wafanyakazi wa TGFA kuwa wizara na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), wamekubaliana kuwapatia nafasi za kozi na mafunzo mbalimbali marubani wa ndege za wakala hiyo.
Aidha, alisema marubani hao pia watapatiwa nafasi ya kurusha ndege za ATCL mara kwa mara ili kuendana na matakwa ya taaluma zao.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa TGFA, Tito Kasambala alimueleza Mhandisi Nditiye kuwa taasisi hiyo ina ndege nne zinazosafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali.
Wakati huo huo, wafanyakazi wa TGFA walimuomba Mhandisi Nditiye kuwasilisha Serikali ombi lao la kuongezwa mishahara kulingana na hali ya soko la ajira ya marubani lilivyo nchini kwa sasa.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akiongea na wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo. Anayemsikiliza ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Tito Kasambala.