MACHI 6, 2018
DAR ES SALAAM
Ombi lililowasilishwa na Hospitali ya Kairuki katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa kesi ya madai inayoikabili isikilizwe kwa siri limetupiliwa mbali.
Hospitali ya Kairuki iliiomba mahakama isikilize kesi hiyo dhidi yake bila waandishi wa habari kuruhusiwa kuiripoti.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba jana alitupilia mbali ombi hilo kwa kueleza kuwa vifungu vya sheria vilivyowasilishwa katika maombi hayo haviendani na shauri lililopo mahakamani.
Hakimu Simba alisema sheria inaruhusu kesi zote za madai kuendeshwa katika mahakama ya wazi isipokuwa kesi za watoto na talaka.
Alisema ni ruksa kwa waandishi wa habari kuripoti nwenendo wa kesi hiyo na kuielekeza hospitali hiyo iwabane iwapo watafanya makosa kuiripoti.
Hospitali ya Kairuki inatuhumiwa kusababisha madhara ya kiafya kwa Khairat Omary, mkazi wa Dar es Salaam aliyekuwa akipatiwa tiba katika hospitali hiyo. Hata hivyo imekanusha madai hayo.
Khairat amefungua kesi ya madai namba 384, ya mwaka jana akidai matibabu aliyopatiwa katika hospitali hiyo yamemsababishai madhara ya kiafya.
Hospitali ya Kairuki imekiri mahakakani kuwa, Khairat alikuwa mteja wao akipatiwa tiba katika hospitali hiyo iliyoko Mikocheni, Wilaya Kinondoni, Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, alipokuwa mjauzito na baada ya kufanyiwa upasuaji Desemba 15, mwaka jana.
Kwamba, Khairat alikuwa na matatizo alipokuwa na ujauzito, hivyo asingeweza kujifungua kwa njia ya kawaida isipokuwa kufanyiwa upasuaji na yeye mwenyewe aliridhia kwa kutia saini kiapo cha kukubali kufanyiwa upasuaji Disemba 15, mwaka jana.
Katika malalamiko yake, Khairat anadai kuna vifaa vya kujifungulia ambavyo viliachwa kwenye mfuko wake wa uzazi alipofanyiwa upasuaji Disemba 21, 2017 jambo ambalo linapingwa na Hospitali ya Kairuki.

Khairat anaiomba mahakama iiamuru hospitali hiyo kumlipa Sh. Milioni 20 kama gharama za tiba na matibabu na gharama za dharura alizotumia, Sh. Milioni 25 kwa ajili ya kupoteza kipato, Sh. Milioni 80 kama gharama za adhabu na Sh. Milioni 30 za kuvunja kwa wajibu wake.