Ndimbo |
DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) kuwagawia hela waandishi wa habari kila linapowaita kuandika habari ni utaratibu wake wa kawaida.
Hayo yamesemwa na baadhi ya wanahabari waliojitokeza kueleza hisia zao baada ya kuripotiwa kuwa TFF imewamwagia mamilioni ya fedha wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali waliohudhuria mkutano wa rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wanahabari aliyehudhuria mkutano wa Rais Karia na kupata mgao huo, Asha Muhaji, akizungumza kwa hasira baada ya kutolewa kwa taarifa ya kuwepo kwa mgawo huo alisema amekasirika sana.
Akizungumza huku akitetemeka shingo, Muhaji amelaumu kuripotiwa kwa mgawo huo na kueleza kuwa ni utaratibu wa kawaida lakini haukupaswa kuwekwa hadharani.
“TFF kuwapa hela waandishi au wahariri bila kuwasainisha mahali popote ni utaratibu wao wa kawaida kwa zaidi ya miaka nane sasa. Hizo ni hela ndogo sana sema hujui kuwa inapokea Dola za Marekani nyingi kutoka FIFA na CAF na inaruhusiwa kuzitumia inavyoona inafaa.
“Kilichonikasirisha ni kusambazwa kwa taarifa ya wahariri kuhongwa. Hili jambo lilikuwa la siri sasa kwenda kuliweka public kuna maana gani kama siyo kuchafuana?
“Takukuru walishakagua sana hesabu za TFF, wanajua kuna pesa za waandishi ndiyo maana hujasikia kitu,” alisema Muhaji.
Kauli hiyo ya Muhaji iliungwa mkono na mwanahabari mwingine, Frolian Kaijage ambaye katika andiko lake kwenye group la wanamichezo la mtandaoni alieleza kuwa hizo ni fedha za mafuta.
“Hakika Asha, hizo ni fedha za ‘mafuta’ tulikuwa tukiziita hivyo nikiwa Afisa Habari pale Karume. Ni miaka takriban 8 tangu nitoke pale na ninafikiri kiwango tulichokua tunatoa wakati ule hakina tofauti na hiki cha sasa,” aliandika Kaijage.
Afisa Habari wa TFF, Clliford Mario Ndimbo alipoulizwa kuhusu uhalali wa utaratibu huo alisema suala hilo hawezi kulizungumzia.