DAR ES SALAAM
TAASISI ya Saratani ya Ocean Road inatibu watu zaidi 2000 kila mwaka kwa kutumia mionzi ya Nyuklia.Hayo yameelezwa leo na Daktari Bingwa na Mtaalamu wa Uchunguzi na Tiba ya Mionzi wa taasisi hiyo, Tausi Maftah.
Maftah aliisifu teknolojia hiyo kwa kueleza kuwa ni ya hali ya juu katika uchunguzi na tiba dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Alisema ingawa Ocean Road ni taasisi ya saratani lakini kwa kutumia teknolojia hiyo ina uwezo wa kuchunguza na kutibu magonjwa mengine yakiwamo ya moyo na figo.
Alisema huduma hiyo imeanzishwa pia katika Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.
Dk. Maftah alisema Ocean Road inaagiza mionzi ya Nyuklia kutoka Afrika Kusini na Bugando inaagiza kutoka Uturuki.