NA MWANDISHI WETU
MWELEKEO mpya wa siasa za majukwaani za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 wa kujitenga na siasa za mipasho na matusi dhidi ya wapinzani unaonekana kupokewa vema na watanzania wengi wakiwemo wafuasi na mashabiki na vyama vya upinzani.
Hayo yamethibitika katika tathimini ya awali ya mwenendo wa kampeni za uchaguzi mkuu, siku kumi za mwanzo, ambapo maelfu ya watanzania wamekuwa wakifurika katika mikutano ya kampeni ya makada wa chama hicho wa ngazi mbalimbali, huku wengine wakilazimika kusimama juani kwa saa nyingi kusubiri kusikiliza hotuba za wagombea.
Tangu kuzinduliwa kwa kampeni za chama hicho na Mwenyekiti, Rais John Pombe Magufuli, Septemba 29, 2020 katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, ambaye hotuba yake ilijikita kunadi ilani na kuomba kura, wafuatiliaji wa mambo ya siasa na wananchi wa kawaida walionekana kuvutiwa na staili ya Rais Pombe kupuuza mashambulizi ya maneno machafu na matusi ambayo amekuwa akielekezewa na baadhi ya washindani wake.
Hotuba hiyo ya Septemba 29 ya Rais Dk. Pombe ambayo ilikuwa ikifuatiliwa na mamilioni ya watanzania kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi ulimwenguni kote, imeacha taswira ya kile ambacho wagombea wa chama hicho wanapaswa kujikita katika kampeni zao.
Ni kwa kufuata taswira hiyo, wagombea wa CCM sasa wanaonekana kuwa na mvuto zaidi kwa wananchi wanaovutiwa na utamaduni mpya wa CCM wa kujitenga na laana ya mdomo na kujikita kuhubiri ilani ya chama chao na kuomba kura huku kibwagizo chao kikiwa kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Alfred Dimoso, mmoja wa mashabiki wa CCM aliyefanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog mapema wiki hii jijini Dodoma, alisema CCM ambacho hapo awali baadhi ya makada wake walikuwa na sifa mbaya ya kupiga vijembe na kutoa maneno machafu dhidi ya wanasiasa wanaoshindana nacho, sasa wanaonekana kuzaliwa upya au kubatizwa upya.
“Yule mzee Yusuf Makamba alisema kweli ujue. Rais Pombe amewabatiza wana CCM kwa moto, sasa ni watakatifu, kila mtanzania ana hamu ya kuwasikiliza. Yaani ni mwendo wa sera, kunadi ilani yao na kuomba kura. Hakuna matusi wala vijembe. Hata ukiwa na mwanao unakwenda kwenye mikutano yao bila wasiwasi.
“Zamani makada wa chama hicho walikuwa wanashambuliana wenyewe kwa maneno ya kashfa na kejeli na hivyo kuwapa nafasi washandani wao kuwang’ong’a kwa kukosa sera na kushindwa kuinadi ilani yao ya uchaguzi kwa wapiga kura na wananchi, hayo yote sasa yanaonekana kuwa historia.
“We hushangai hivi sasa hata wagombea ubunge na udiwani ni magwiji wa kuinadi ilani ya chama chao tena kwa kumwanga takwimu za utekelezaji wa ilani inayokwisha na nini kitafanyika katika ilani mpya. Lakini zaidi ni mahubiri ya wagombea wa chama hicho ya amani, umoja, mshikamano, maendeleo hayana chama, yanayotolewa kwa lugha ya upole na unyenyekevu yamewafanya wao na chama chao kuwa na mvuto mkubwa wa kisiasa dhidi ya washindani nao,” alisema Dimoso.
Mwingine aliyehojiwa na kutoa maoni yake kuhusu CCM na makada wake kujiumba upya ni Jumanne Abdul, mkazi wa Muheza mkoani Tanga anayejishughulisha na biashara ndogo ndogo aliyesema uzinduzi wa kampeni za CCM katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma pia umekuja na neema kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la machinga.
“Mimi ni mpiga picha wa kujitegemea, ni machinga. Nimetokea Tanga kuja kwenye huu uzinduzi wa kampeni kwa sababu hizi kampeni za wana CCM zina mambo ya ziada, ni fursa ya biashara kwetu.
“Kwanza ni kampeni ambazo zimeratibiwa vizuri sana, hakuna fujo, kuna burudani ya wasanii wote maarufu nchini na viongozi wote wakiwemo wastaafu wapo hapa.
“Mkutano huu ni tofauti kabisa na ya wanasiasa wengine. Hapa wapiga kura wanaondoka wakiwa wameelewa somo siyo matusi na kejeli,” alisema Abdul.
Tanzania PANORAMA Blog itaanza kufanya uchambuzi wa ilani za uchaguzi za vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 wiki hii. Karibu twende pamoja.)