David Kafulila |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema Rais Samia Suluhu Hassan amevunja rekodi ya utekelezaji bajeti ya maji ya miaka 20 ndani ya muda mfupi wa uongozi wake.
Kafulila aliyesema hayo hivi karibuni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alipokuwa akikabidhi ofisi kwa mrithi wake, Dk. Yahaya Esmail Nawanda.
Alisema utekelezaji wa bajeti ya miradi ya maji kwa sasa unaokoa Shilingi trilioni tatu ambazo zingetumika kutibu magonjwa yatokanayo na maji.
“Wakati nakuja Mkoa wa Simiyu kero kubwa kuliko zote ilikuwa maji lakini mwaka mmoja niliokaa hapa tumeshirikiana kusimamia mabilioni ya fedha za miradi ya maji, wote tunaona tatizo linapungua kwa kasi,” alisema Kafulila.
Alisema rekodi zilizopo sasa zinaonyesha kuwa upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 56 mwaka 2020 mpaka asilimia 73 kufikia mwezi Juni 2022 na kwamba hiyo ni mbali ya mradi mkubwa wa bomba lenye urefu wa km 190 wa kutoka Ziwa Victoria, wenye thamani ya Shilingi bilioni 400 utakaopita katika vijiji zaidi ya 200 ambao kazi za awali zimeanza.
“Niwambie ukweli. Nimesoma bajeti za miradi ya maji za miaka 20, kuanzia mwaka 2000 mpaka 2020, hakuna mwaka ambao fedha za miradi ya maji zilitolewa kwa asilimia 80. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita, mwaka 2021/22 fedha za miradi ya maji zilizotolewa ni Shilingi billioni 743 ambazo ni sawa na asilimia 95 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Hizi zilitolewa ndani ya miezi tisa, sio mwaka.
“Huu ni ushahidi kuwa Rais wetu anatekeleza kauli mbiu yake ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani kwa vitendo. Anaelewa kuwa maji ni uchumi, maji ni ustaarabu, maji ni afya.
“Ripoti ya Shirika la Afya duniani ya mwaka 2014 ilionesha kuwa kwenye kila Dola ya Marekni moja inayowekezwa kwenye maji, inaokoa Dola za Marekani 4.2 ambazo zingetumika kutibu magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama,” alisema Kafulila.
Aidha, Kafulila alisema Shilingi bilioni 743 zilitolewa kwa ajili ya miradi ya maji kwa mwaka mmoja wa 2021/22 ni sawa na kuokoa Shilingi trilioni 3.1 ambazo zingetumika kutibu magonjwa yatokanayo na maji.
Kafulila aligusia ripoti ya Taasisi ya SYNOVATE ya mwaka 2008 kwa kueleza kuwa utafiti uliofanywa na taasisi hiyo ulionesha kuwa kero namba moja kwa mtazania ni maji hivyo kasi ya utekelezaji wa bajeti ya maji kwa sasa ni kielelezo kuwa Rais Samia anatatua tatizo la maji kwa kuyagusa maisha ya watanzania walio wengi na hasa wa vijijini.
“Hivyo tunaposema Mama anaupiga mwingi sio sisi ni takwimu za kitafiti, tuendelee kuwasaidia wananchi kwa kuhakikisha wakandarasi wanatekeleza mikataba na tuendelee kuvunja mikataba ya wababaishaji kama tulivyofanya siku zote kuhakikisha kuwa fedha anazoleta Rais kukabili kero ya maji zinafanya kazi kweli kweli,” alisema.