Friday, September 12, 2025
spot_img

POLISI WALIA UKATA DAR

 

NA MWANDISHI WETU

ASKARI Polisi wa Kituo Kidogo cha Polisi Mtongani kilichopo Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam wameeleza kuwa wanakabiliwa na ukata mkali unaokwamisha utekelezaji wa majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Wameeleza hayo baada ya Tanzania PANORAMA Blog kuhoji sababu za mafaili ya kesi zilizofunguliwa kituo kidogo cha Polisi Mtongani kushindwa kupelekwa Kituo cha Polisi Kawe kwa zaidi ya siku tano.

Akijibu swali la mmoja wa walalamikaji jana asubuhi lililohoji; kwanini mafaili ya kesi zilizofunguliwa hayajapelekwa Kawe kwa zaidi ya siku tano wakati siyo mbali, mmoja wa askari aliyekuwa kituo hapo alisema “muzee walishindwa tu kukwambia ukweli, hali ni mbaya, tuna hali mbaya hadi usafiri wa kupeleka mafaili hapo Kawe hatuna.”

Alipoambiwa kuwa mlalamikaji yupo tayari kuwasaidia polisi usafiri wa kubeba faili hizo kuzipeleka Kituo cha Polisi Kawe kwa sababu amesumbuka muda mrefu na anatumia gharama kuzunguka vituo vya polisi Kawe na Mtongani, polisi huyo alisema hilo haliruhusiwi ila atajitahidi kutafuta njia ya kuyapeleka mafaili hayo.

Dalili za kuwepo kwa ukata kwa polisi hao zilianza kuonekana Jumamosi ya Oktoba 10, 2020 baada ya Mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog kufika kituo kidogo cha Polisi Mtongani akiwa amejeruhiwa vibaya na wezi waliokuwa wamewateka abiria kwenye daladala na kuwashambulia kwa bisibisi na mapanga kabla ya kuwanyang’anya pesa, simu na vitu vingine vya thamani walivyokuwa navyo kisha kuwatupa pembezoni mwa barabara.

Mwandishi wetu aliwaeleza polisi hao kuwa alipanda daladala la wahalifu akiwa na abiria wenzake wawili katika kituo cha daladala cha njia panda ya kwenda Hotel ya Bahari Beach ambapo mmoja wa wahalifu alikuwa ametangaza kuwa linakwenda stendi ya Makumbusho.

“Hatukujua kama ndani ya daladala hilo kulikuwa na wahalifu, mmoja wao alitangaza kuwa linakwenda Makumbusho hivyo mimi na abiria wenzangu wawili tukapanda pale kituo cha kona ya kwenda Bahari Beach. Lakini lilipoondoka tu wale wezi ambao walikuwa zaidi ya 20 mle ndani wakaanza kupiga kelele kama washangiliaji wa mpira na dreva akawasha muziki kwa sauti ya juu ikawa kelele tu.

” Hapo wakaanza kutushambulia, walianza na mama tuliyepanda naye akawa anakataa kuachia pochi yake, wakamkata panga mkononi ukabaki unaning’inia, wakachukua kila kitu wakamsogeza mwisho kabisa wa gari na kijana mwingine niliyepanda naye yeye alikuwa amekatwa mapanga mawili kichwani na kuwapa kila kitu akabaki analia tu.

“Mimi nilijaribu kumwambia dreva apunguze sauti ya muziki ajabu alitoa upanga akanambia tulia kisha akaendelea kuendesha gari kwa kasi. Kwa sababu mlango wa gari ulikuwa umefungwa na taa zilikuwa zimezimwa niliiona hatari iliyokuwa mbele, sikuwa mbishi niliwapa pesa, simu nao walinisachi na kuchukua kila walichoona kinafaa.

” Walinishambulia kwa ngumi tu lakini walinijeruhi vibaya usoni na mdomoni nadhani kwa sababu sikuwa mbishi na walikwenda kunitupa Kona ya Mbuyuni wakawa wameondoka na mama ambaye wamemkata mkono, namba ya gari nimeikariri ina mstari wa njano ya wekundu wa damu ya mzee, tukiifukuza tunaikamata kwa sababu nimeona huko mbele kuna foleni,” alijieleza mwandishi wetu mbele ya kaunta ya polisi.

Polisi aliyekuwa akisikiliza maelezo yake alisema hawana uwezo wa kuifukuza daladala hiyo kwa sababu eneo hilo la kipolisi hadi Kawe lina gari moja tu bali anamfungulia RB na atampa PF 3 akatibiwe kwa sababu alikuwa akivuja damu nyingi.

“Hatuna jinsi ya kulifukuza mzee tuna gari moja tu nalo muda huu linasambaza askari kwenye malindo, we acha kumzungumzia mama aliyekatwa mkono naye watamtupa huko mbele atakwenda kutoa taarifa kituo chochote cha polisi kama ulivyofanya wewe.

” Nakufungulia faili nakupa PF 3 nenda Hospitali ukatibiwe angalia tisheti yote ulivyoloa damu, jihurumie umeumua sana acha kuhurumia wengine.

“Kwa sababu umetutajia namba na rangi za mstari wa hilo daladala Jumatatu tu tutalikamata.  Hao wahalifu wamekuwa tishio huwa wanaenda beach huko kila weekend kufanya uhalifu msiwe mnapanda daladala zao maana ndiyo mbinu yao mpya.

“Katibiwe nenda nyumbani kasikilizie hali yako Jumatatu asubuhi saa mbili uwe polisi Kawe utamkuta mpelelezi wa kesi yako, kesho jumapili hakuna kazi hivyo jumatatu litakamatwa hilo daladala,” alisema askari aliyekuwa kaunta.

Jumatatu, Oktoba 12, 2020, saa tano asubuhi mwandishi wetu alifika Kituo cha Polisi na kuonyesha RB namba KMT/RB/2428/2020 aliyopewa kituo kidogo cha Polisi Mtongani ili aonyeshwe mpelelezi wa kesi yake lakini polisi aliyekuwa kaunta alisema mafaili kutoka Mtongani hayajafika kituoni hapo wala hakuna kumbukumbu zake zilizorekodiwa kwenye rejista kituoni hapo na kuelekezwa arudi Mtongani kesi yake itashugulikiwa huko.

Alhamis, Oktoba 16, 2020 mwandishi wetu alirejea kituo cha Polisi Mtongani ambako baada ya polisi kukagua makaratasi mengi yaliyokuwa kaunta walisema faili lake bado lipo kituoni hapo likisuburi utaratibu wa kupelekwa Polisi Kawe.

“Siyo peke yako mzee, faili zote hizi hazijapelekwa hali mbaya, hakuna usafiri.  Wewe uwe unapitapita pale Polisi Kawe siku tukilipeleka utalikuta ataambiwa,” alisema askari aliyekuwa kaunta.

Alipoelezwa kuwa kwa sababu ya kupunguza usumbufu na gharama za usafiri na pia kuokoa muda anaweza kutoa msaada wa usafiri ili mafaili hayo yapelekwe Kawe aliambiwa hilo haliruhusiwi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, alipotafutwa jana kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia ukata huo alipokea msaidizi wake na kueleza kuwa yupo kwenye kikao atafutwe muda mwingine.

Alipotafutwa leo alipokea simu na kueleza kuwa hasikii vizuri anachoulizwa pengine yupo eneo baya hivyo atumiwe ujumbe na alipotumiwa ujumbe kwenye simu yake akiulizwa kuhusu kuwepo ukata katika eneo lake la utawala na kukwama kwa mafaili ya kesi kituo cha Polisi Mtongani kwa siku tano, hakujibu.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya