RIPOTA PANORAMA
KAMATI ya Bunge ya Bajeti, imetembelea miradi ya kuzalisha umeme wa gesi ya Kinyerezi II na ule wa upanuzi wa Kinyerezi I unaoendeshwa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kueleza kuwa imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia pia ilitembelea kituo cha kupokea gesi asili inayotumika kuzalisha umeme kilichoko jirani na miradi hiyo.
Katika ziara hiyo, mwenyeji wa kamati hiyo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani aliwahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa miradi hiyo inaendelea kama ambavyo Serikali ilitarajia na kwamba watanzania wategemee ongezeko kubwa la upatikanaji wa umeme pindi miradi hiyo itakapokamilika.
“Mwenyekiti na wajumbe wote wa kamati, miradi hii kunzia ule wa Kinyerezi I unaopanuliwa ambapo kutakuwa na ongezeko la umeme megawati 35 na hivyo kufanya jumla ya megawati 185 zitakazozalishwa kutoka Kinyerezi I na huu wa Kinyerezi II utakapokamilika Agosti mwakani, 2018 utatupatia megawati 240 na ukijumlisha na miradi mingine itakayofuatia ya Kinyerezi III na VI, tutakuwa na jumla ya megawati 1175,” alifafanua Dk. Kalemani.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Kinyerezi II, Mhandisi Stephene Manda aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa mradi huo utakuwa na jumla ya mashine nane ambazo zitafua umeme na tayari ufungaji wa mashine hizo umeanza na unaendelea na kuongeza kuwa kuanzia Disemba Mosi mwaka huu, Tanesco itaingiza megawati 30 kwenye gridi ya Taifa na kufanya hivyo kila baada ya mwezi mmoja kadri kazi ya ufungaji wa mashine hizo utakavyokuwa unakamilika.
Alisema gharama za mradi wa Kinyerezi II ni Dola za Marekani, milioni 344.
Wajumbe wa kamati hiyo pia walipata fursa ya kujionea kazi ya utandazaji wa mabomba makubwa ya kupitisha gesi kutoka kituo cha kupokea gesi kuelekea kwenye eneo la miradi hiyo.
“Niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na haya ndio matarajio ya wabunge kuona kuwa miradi hii ambayo inagharimu fedha nyingi za walipa kodi inakamilika kwa wakati ili hatimaye Serikali iweze kutekeleza mipango yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kama ilivyoahidi wananchi,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia baada ya kumaliza ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme wa gesi asilia.