BENNY MWAIPAJA, DODOMA
SERIKALI imekubaliana na washirika wa maendeleo kurejesha uhusiano wa karibu na wenye tija ili kusaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III).
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa mazungumzo ya kimkakati baina ya Serikali na washirika wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali duniani mjini Dodoma mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema mwongozo wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Serikali na washirika wa maendeleo una malengo mbalimbali.
Alisema mwongozo huo wa miaka saba, 2017/2018 hadi 2014/2025, umelenga kuipa Serikali nafasi ya kuongoza mchakato wa maendeleo na kuijengea Serikali uwezo wa kukusanya mapato ya ndani, kuchambua fursa muhimu za uwekezaji na kutumia masoko ya kikanda na kimataifa kupata faida.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika hao, Alvaro Rodriguez aliahidi kushirikiana na Tanzania ili malengo yake ya maendeleo yaweze kufikiwa kwa kuboresha ushirikiano uliokuwa umeanza kulegalega.
Serikali na washirika wa maendeleo walifikia makubaliano ya kukutana mara mbili kwa mwaka. Kikao kingine kinatarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu.