RIPOTA MAALUMU
MAWAKILI wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) na Katibu wa Kanda ya Nyasa, Emmanueli Masonga wamekamilisha taratibu za ukataji wa rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya.
Mmoja wa mawakili wa Sugu, Faraji Mangula jana aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa kuwa tayari wameshakamilisha taratibu zote muhimu za kukata rufaa hiyo wanachosubiri ni kupangiwa tarehe na Mahakama Kuu.
Wakili Mangula alieleza kuwa anatumaini mahakama itapanga haraka tarehe ya kuanza kusikiliza kesi ya Sugu.
Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walihukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani bila faini baada ya kukutwa na hatia ya kutamka maneno ya fedheha yaliyomlenga Rais Dk. John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Disemba 30, mwaka 2017 katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Mwenge ya jijini Mbeya.