RIPOTA PANORAMA – 0711 46 49 84
LEO asubuhi, Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Wallace Karia amefanya mkutano na wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali vya habari na kueleza mikakati yake mingi pasipo kujibu ‘mashtaka’ ambayo ameelekezwa katika taasisi hiyo anayoiongoza.
Katika mkutano huo, Karia hakujibu ‘mashtaka’ iliyoelekezwa TFF likiwemo lile la Wambura kama Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya TFF kuhoji matumizi ya Sh. bilioni 3 zilizotumika ndani ya miezi sita.
Pia, Karia hakujibu wala kulitolewa ufafanuzi shtaka la kukiukwa kwa kanuni/taratibu za ajira ndani ya shirikisho katika utoaji nafasi za kazi na hakuzungumza chochote kuhusu wafanyakazi wa kujitolea wanaoelezwa kupewa kipaumbele cha kuajiriwa kwa sasa ndani ya shirikisho huku wale wenye sifa wakiwekwa kando kwa sababu siyo washirika wa kakribu wa viongozi wakuu wa shirikisho hilo.
Aidha, katika hali ya kushangaza Karia hakusema chochote kuhusu kile kinachodaiwa kuwa taratibu za shirikisho zinaelekeza nafasi za ajira ndani ya shirikisho zinapaswa kutangazwa, waombaji wa ajira wanapaswa kufanyiwa usaili na kigezo cha elimu katika nafasi muhimu za kiutendaji ndani ya shirikisho kinapaswa kuzingatiwa, mambo ambayo utawala wa Rais Karia unadaiwa kuyakiuka.
Wataalamu wa mambo ya soka wameeleza kuwa inawezekana Karia ameamua kuyaweka kiporo ‘mashtaka’ hayo ili ukweli wake uje kudhihirishwa na vyombo vingine ndani ya TFF lakini kwa hatua yake ya kutangaza kwenye mkutano huo kuwa hayuko tayari kukaa meza moja na ‘mdhalimu’ katika kipindi ambacho anasuguana na msaidizi wake, atalazimika sasa au huko tuendako kusimama tena mbele ya wana habari kutoa majibu ya ‘mashtaka’ haya na hata yale yatakayoongezeka.
Katika mkutano huo, Karia amesema mtu yeyote aliyechezea fedha za TFF hatasalimika bila kujali kama ni rafiki yake na ametoa wito kwa yeyote anayejua kuwa ana pesa za TFF kinyume cha utaratibu ajisalimishe mwenyewe.
Karia amewaambia wahariri kuwa anafanya kazi ya kuisafisha TFF na kazi hiyo ina gharama zake hivyo anahitaji kuungwa mkono kwa hatua madhubuti anazochukua za kupambana na udhalimu katika soka.
Amesisitiza kuwa atapambana bila woga pasipo kumdhulumu, kumuonea au kumpendelea mtu yeyote na kwamba hayuko tayari kukaa meza moja na mdhalimu.
Amekwenda mbali kidogo kwa kujifananisha na Rais Dk. John Magufuli kwa kile alichoeleza kuwa katika kupambana na ufisadi yeye ni Magufuli mwingine ndani ya TFF.
Ametaja baadhi ya hatua ambazo TFF inachukua kujisafisha kuwa ni pamoja na kupambana na wizi wa mapato ya milangoni na kwamba tayari baadhi ya viongozi wamefungiwa.
Pamoja na hayo, Karia ameutumia pia mkutano huo kuzungumzia juu juu baadhi ya ‘mashtaka’ yaliyoelekezewa shirikisho kwa kueleza kuwa wakati anaingia madarakani TFF ilikuwa na wafanyakazi 44 waliokuwa wanalipwa mshahara Sh. mil 85. Kwamba yeye amewapunguza hadi 21 ambao mishahara yao ni Sh. mil 50.
Amesema upunguzaji wafanyakazi haujiegemezi kwenye kufukuza bali wafanyakazi wasiokuwa na tija wanapomaliza muda wao, mikataba yao haiongezwi.