Sunday, November 23, 2025
spot_img

RSA TANZANIA, MADEREVA NA WCF WAADHIMISHA SIKU YA WAATHIRIKA WA AJALI DUNIANI

Madereva wa vyombo vya moto wameaswa kutambua wajibu na nafasi yao katika kuhakikisha usalama barabarani nchini unaimarika, ili kuifanya Tanzania kuwa katika uelekeo sahihi wa utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa la kupunguza madhara ya ajali za barabarani kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Wito huo umetolewa leo wakati wa semina kwa madereva iliyokuwa imeandaliwa na asasi ya kiraia ya Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA Tanzania), kwa kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukizi kwa Waathirika wa Ajali za Barabarani Duniani, ambayo huadhimishwa wikiendi ya tatu ya mwezi novemba kila mwaka.

Katika nasaha zake kwa washiriki wa semina, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam aliyewakilishwa na Mkuu wa Oparesheni wa Kikosi Kanda hiyo, Afande Msigwa, alisisitiza kuwa madereva ni nguzo muhimu katika kulinda maisha ya watumiaji wa barabara. hivyo, mafunzo kama hayo yana faida kubwa sana kwakuwa yanawakumbusha wajibu walionao katika kuhakikisha vifo na majeruhi watokanao na ajali vinapungua.

Lengo la tukio hili ni kuongeza uelewa wa madereva juu ya nafasi yao katika kupunguza ajali na madhara yake, ikizingatia kwamba madereva ndio kundi linalobeba jukumu kubwa katika kuhakikisha safari na barabara kwa ujumla zinakuwa salama kwa kila mtumia barabara. Kupitia mafunzo haya, washiriki waliweza kupata maarifa mapya kuhusu mienendo salama barabarani, wajibu wao kisheria, na athari za uzembe au kutokufuata taratibu za usalama..

Semina hii ilijikita zaidi katika nguzo tatu kati ya tano za usalama barabarani ambazo ni zile za magari salama, watumiaji salama wa barabara, na huduma za dharura baada ya ajali (post-crash care) ambapo washiriki walifundishwa umuhimu wa kuhakikisha magari yao yako katika hali bora kila wakati, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara, kufuata ratiba za matengenezo, na kutambua viashiria vya hitilafu zinazoweza kusababisha ajali.

Nguzo ya watumiaji salama wa barabara pia ilisisitizwa ambapo madereva walikumbushwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kuheshimu watembea kwa miguu, kujiandaa na safari, na kujiepusha na tabia hatarishi kama kutumia simu wakati wa kuendesha gari. Washiriki walihimizwa kuwa mabalozi wa usalama popote wanapokuwa, kwani tabia binafsi za madereva zina athari ya moja kwa moja kwa maisha ya watu wengine.

Katika upande wa huduma za dharura baada ya ajali, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liliwasilisha mada muhimu kuhusu namna ya kutoa msaada wa awali pale ajali inapojitokeza. Walifundisha madereva hatua za msingi za kuokoa maisha kama kuweka eneo salama, kutoa msaada wa haraka kwa majeruhi bila kuongeza madhara, na njia sahihi za kuwasiliana na vyombo vya huduma za dharura. Maarifa haya ni muhimu kwani mara nyingi hatua za kwanza ndizo huamua uwezekano wa kuokoa maisha.

Kwa upande mwingine, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) walitoa elimu kuhusu uhusiano kati ya ajali, usalama kazini, na fidia. Walibainisha kuwa madereva ni sehemu kubwa ya wafanyakazi waliopo katika mazingira hatarishi, hivyo uelewa kuhusu fidia unawasaidia kutambua haki zao na wajibu wa waajiri katika kulinda usalama kazini. Aidha, WCF ilieleza jinsi fidia inavyoweza kupunguza mzigo wa kifedha kwa waathirika na familia zao pindi ajali zinapotokea.

Tukio hili pia liliangazia umuhimu wa mashirikiano kati ya taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau binafsi katika kupunguza ajali za barabarani. Kupitia ushirikiano huu, kila chombo huleta ujuzi wake maalum—iwe ni ujenzi wa uwezo, utafiti, uokoaji, au utekelezaji wa sheria—na kwa pamoja kuhakikisha malengo ya kupunguza vifo na majeraha barabarani yanatimia.

Madereva walipata fursa ya kuuliza maswali, kujadili changamoto wanazokutana nazo barabarani, na kubadilishana uzoefu. Mazungumzo hayo yameongeza uelewa kuhusu vikwazo vinavyowakabili na pia kutoa mwanga juu ya maeneo yanayohitaji maboresho zaidi katika mfumo mzima wa usalama barabarani nchini.

Kupitia tukio hili, mabalozi wa usalama barabarani, madereva wa vyombo vya moto na wadau washirika wameonesha kwa vitendo kuwa elimu, ushirikiano na uwajibikaji ndiyo nguzo kuu za kujenga mfumo salama wa usafiri. Semina kama hizi zinaendelea kuwa nyenzo muhimu katika juhudi za kitaifa za kuokoa maisha na kutengeneza mazingira salama kwa wote.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya