Sunday, November 23, 2025
spot_img

MWELEKEO SAHIHI TRC

MAKALA YA MTANGAZAJI

UKURASA mpya wa Tanzania kuelekea mafanikio ya kibiashara na kuwa na miundombinu ya uhakika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, umefunguliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

TRC limechukua mwelekeo sahihi wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuzindua mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge (SGR), ya Uvinza – Musongati.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye wakiwa pamoja na viongozi wengine wa Tanzania na Burundi katika uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa reli ya Musongati.

Mtandao wa Reli hii inayojulikana zaidi kwa jina la mradi wa reli ya Musongati, utaunganisha Mji wa Uvinza uliopo Mkoa wa Kigoma, Tanzania na Mji wa Musongati uliopo Burundi. Mji wa Musongati una utajiri mkubwa wa madini ya nikeli, shaba, kolbati, platinamu na dhahabu.

Ramani inayoonyesha Mji wa Musongati.

Mji wa Musongati.

Kwa TRC, chini ya Serikali ya Tanzania; kujenga mtandao huo wa reli kunaiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa lango kuu la madini hayo kufika kwenye masoko ya kimataifa.

Sambamba na hilo, mradi wa reli ya Musongati utaondoa changamoto ya msongamano wa maroli ya kusafirisha mizigo, utaondoa gharama kubwa za matengenezo ya barabara zinazoharibiwa na uzito wa magari ya kusafirisha mizigo, utatatua changamoto ya uchafuzi wa mazingira na utapunguza ajali za barabarani zinazogharimu maisha ya watu wengi.

Reli ya Musongati itaondoa changamoto ya msongamano wa maroli ya kusafirisha mizigo kama yanavyoonekana kwenye picha.

Reli ya Musongati itakuwa na urefu wa kilomita 282 na ujenzi wake utagharimu Dola za Marekani bilioni 2.15. Wakandarasi wake ni Kampuni ya China Railway Engineering Group (CREGC) na China Railway Design and Consulting Group (CREDC), zote kutoka China. Muda wa ujenzi unatarajiwa kuwa miaka sita.

Ni reli ya umeme na itajengwa kwa viwango vya kimataifa ikiwa na kasi ya hadi kilomita 160 kwa saa na pia ujenzi wake utajumuisha daraja la mpakani la Mto Malagarasi litakalokuwa na urefu wa kilomita moja na vituo saba vya abiria na mizigo.

Mchanganyiko wa madini yanayopatikana Musongati.

Itakuwa na uwezo wa kusafirisha zaidi ya tani milioni tatu za madini kwa mwaka na itazidi kuchechemua shughuli za Bandari ya Dar es Salaam na biashara zaidi kwa watoa huduma wa ndani.

TRC YA KWANZA EAC

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limekuwa la kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuanza kutekeleza mradi mkubwa unaoziunganisha moja kwa moja nchi mbili kwa reli ya kisasa.

Mji wa Uvinza

Hatua hii ya TRC itachochea ukuaji wa uchumi wa Burundi ambayo itapata njia nafuu na ya uhakika ya kufikia masoko ya kimataifa ya madini yake yaliyopo Musongati na pia itaimarisha uhusiano wake na Tanzania.

Kwa upande wa Tanzania, mradi wa reli ya Musongati utawezesha upatikanaji wa ajira, biashara na ukuaji wa uchumi kwa sehemu ambazo utapita na aidha; kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu kutachochea kasi ya mazungumzo ya kuongeza mtandao wa reli hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hilo likapokamilika, Tanzania itakuwa kitovu cha ukanda wa kati (Central Corridor) unaoanzia Dar es Salaam kupitia Dodoma, Tabora, Kigoma na kuvuka mpaka hadi nchini Burundi, Rwanda na DRC.

RELI YA MATUMAINI

Reli ya Musongati inahusu watu, fursa na ndoto. Kwa TRC kutekeleza mradi huu inachora ndoto ya maisha ya matumaini ya watanzania na warundi, huko tuendako.

Mtandao wa Reli ya Umeme uliopo Tanzania.

Serikali ya Tanzania inapojikita kwenye uwekezaji wa miundombinu na lojistiki, inaweka nguzo imara za sera za uchumi kwa watu wake.

Safari za treni za abiria na mizigo, kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na kwa upande mwingine hadi mkoani Kigoma kisha kuvuka mpaka kuelekea Burundi, Rwanda hadi DRC ni tumani jipya la mabadiliko ya kiuchumi na biashara kwa watu wa Afrika Mashariki.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya