NA MWANDISHI WETU, HONG KONG
JE, wewe ni mwekezaji unayetafuta tasnia yenye fursa kubwa ya kukuza utajiri wako nchini Tanzania?
Usitafute tena, tabaka la kati la kijamii barani Asia linalokuwa kwa kasi likiwa na mchango wa asilimia 54 ya mahitaji ya kimataifa linahitaji mazao sita ya ‘horticulture’ ya Tanzania.
Mazao hayo ni tikitimaji, pilipili, parachichi, macadamia, matunda aina ya berries na mboga mboga mchanganyiko.
Mnyororo huu wa thamani unazidi kushika kasi katika masoko ya Asia, kama ilivyoangaziwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAHA, Dk. Jacqueline Mkindi, aliyeongoza makampuni 19 ya wauzaji wa mazao ya horticulture katika masoko ya nje ya nchi kwenda katika maonesho ya juu ya biashara ya mazao barani Asia, maarufu kama Asia Fruit Logistica 2025.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Dk. Mkindi anasema mahitaji haya makubwa kutoka barani Asia yanavunja rekodi na yanapandisha hadhi ya mazao haya ya Tanzania katika viwango vipya.
Anasema wakati ni huu kwa wakulima na wawekezaji kuongeza uzalishaji na kunufaika na fursa kubwa zinazotokana na tabaka la kati linalokuwa kwa kasi barani Asia.

Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dk Jacqueline Mkindi (katikati) akiwa na baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya horticulture wanaoshiriki maonesho ya biashara ya mazao barani Asia, maarufu kama Asia Fruit Logistica 2025.
Anatoa mfano kuwa zao la parachichi limepanda kwa kasi kiumaarufu katika Bara la Asia na linatumiwa zaidi na watu wa tabaka la kati.
Takwimu za World Economic Forum zinaonyesha kuwa tabaka la watu wa kati la Asia lilikuwa na watu bilioni mbili mwaka 2020 na linatarajiwa kufikia watu bilioni 3.5 ifikapo 2030, likiwakilisha karibu theluthi mbili ya tabaka la kati duniani.
Ushiriki wa TAHA kama taasisi pekee ya sekta binafsi kutoka Afrika kwenye Asia Fruit Logistica 2025 unathibitisha dhamira ya Tanzania kuweka alama yake katika masoko ya kimataifa ya mazao ya horticulture.
“Ushiriki wetu wa kimkakati katika maonesho haya ya kifahari unaonyesha dhamira ya Tanzania ya kushika na kutawala masoko mapya, tukishukuru ufadhili kutoka Trade Mark Africa (TMA), SIDA na World Food Programme (WFP),” alisisitiza Dk. Mkindi.
Anasema wanunuzi wa kikanda wa Asia walivutiwa zaidi na bidhaa za Tanzania huku wakishangazwa zaidi na ubora wake.
Dk. Mkindi anasema ujumbe wa Tanzania katika maonyesho hayo umepata maarifa muhimu kuhusu teknolojia za kisasa za uchakataji na vifungashio kutoka kwa wabunifu nchini China, Marekani, Japani, na Italia.
Ujumbe wa waandaaji wa maonesho ya Fruit Logistica wa Berlin na Asia waliotembelea banda la TAHA, walitoa pongezi kwa wauzaji wa nje ya Tanzania kwa ushiriki wao na mchango wao katika tasnia horticulture kimataifa.
Dk. Mkindi anasema pongezi zilizotolewa kwa TAHA zinathibitisha uwezo wa Tanzania kuzalisha mazao ya horticulture.