UONGOZI wa Klabu ya Simba, umepanga kufanya usajili wa wachezaji wapya kwa kimkakati ili waweze kutimiza ndoto yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu uliopita, Simba walifika hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini walishindwa kutwaa ubingwa baada ya kufungwa na timu ya Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1 katika michezo miwili iliyochezwa ugenini na nyumbani.
Katika mchezo wa fainali ya kwanza, Simba walipoteza kwenye Uwanja wa Manispaa wa Berkane, baada ya kufungwa mabao 2-0 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 waliporudiana kwenye Uwanja wa Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Kwa kuhakikisha ndoto yao inatimia, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa HNAeshima wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’, amesema watahakikisha wanafanya usajili wa wachezaji wenye tija ili kuona wanatimiza malengo waliyojiwekea yakiwamo ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Dewji alisema watafanya usajili huo kwa umakini na kuliongezea nguvu benchi la ufundi ambalo kwa sasa lipo chini ya kocha mkuu, Fadlu Davies, lengo kubwa ni kuifanya timu ya Simba kuwa bora katika michuano ya ndani na kimataifa.
Msimu uliopita wa 2024/2025 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba walimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, huku watani wao wa jadi Yanga wakitwaa ubingwa kwa misimu minne mfululizo.