Timu ya Tanzania ya Wanawake ‘Twiga Stars’ leo inatarajia kushuka uwanjani kumenyana na Mali ukiwa ni mchezo wa kwanza wa kuwania ubingwa Afrika (WAFCON) utakaochezwa mjini Morocco.
Twiga Stars ambayo ipo Kundi C, pamoja timu ya Afrika Kusini ‘Banyama Banyama’, Ghana na Mali. Katika mchezo wa leo, Twiga Stars watahitaji ushindi ili iweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa kombe hilo.
Baada ya mchezo huo, Twiga Stars ambayo ni timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki (CECAFA), itavaana na Afrika Kusini na baadaye Ghana.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), bingwa wa michuano hiyo ataondoka na kitita cha Dola za Kimarekani 1000000 sawa na Sh bilioni 2.7 za Tanzania. Mshindi wa pili atavuna Dola 500,000 sawa na Sh.Bilioni 1.035 za Tanzania, wakati mshindi wa tatu ataondoka na Dola 350,000 sawa na Sh. Milioni 945.