Tuesday, July 1, 2025
spot_img

MAAJABU YA KASA HIFADHI YA SAADANI

ARODIA PETER

KASA ni aina ya mnyama kobe. Ni mkubwa kwa umbo lakini anaishi baharini. Hutaga mayai yake katika mchanga wa fukwe za kanda za tropiki na nusu tropiki.

Kasa ni miongoni mwa samaki au viumbe wa baharini ambao wamepungua kwa zaidi ya asilimia 80 duniani.

Wanasayansi wanasema kuna aina saba za kasa duniani, miongoni mwake, tano zinapatikana Tanzania.

Baadhi ya jamii zinazoishi maeneo ya Pwani ya Kusini na Zanzibar zinamtumia kasa kama kitoweo. Hata hivyo, kasa wanatajwa kuwa na sumu kali ambayo inaweza kusababisha kifo kwa binadamu.

Akitoa ufafanuzi juu ya mnyama huyo, mwongoza watalii upande wa fukwe ya bahari katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani hivi karibuni, Hamis Mwanakombo maarufu ‘Mr. kasa au Hamisi kasa’ anasema walianza kuhifadhi mazalia ya kasa tangu mwaka 2004.

Hamisi Mwinyikombo, mwongoza watalii kwenye fukwe ya Bahari ya Hindi katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Anasema hifadhi hiyo ilianza na viota vinne, lakini hivi sasa vimefikia 35 mpaka 40 kwa mwaka, jambo ambalo linaashiria kuongezeka kwa viumbe hao adimu duniani.

Anasema kasa ni kivutio kinachoifanya Hifadhi ya Saadani kuwa ya kipekee kati ya hifadhi 21 nchini kwakuwa na kasa wa bahari lakini pia kasa wa kijani, na kasa huyo anakuwa wa kijani kwa sababu anakula majani.

“Kasa wana tofauti sana. Kasa anayepatikana Saadani ni mkubwa namba mbili duniani, anazaliwa akiwa na ukubwa wa milimita 25 na anazeeka akiwa na urefu wa mita 1.30 na uzito wa kilogram 400.

“Kasa wa Tanzania ana gamba gumu lililochongoka tumboni na mgongoni, ana vipande kama vigae (tiles) 13 mgongoni na mbili baina ya jicho na jicho.” anasema Hamisi Kasa na kuongeza.

“Kasa wa pili ni mdogo, anapatikana katika kisiwa cha Mafia, mdomo wake umejikunja kama ndege tai (egle), magamba yake yamepandiana na chakula chake kikuu ni sponji.

“Kasa wa tatu anapatikana nchini Kenya, ana magamba kama 15 mgongoni na matano kichwani na chakula chake ni dagaa wadogo wadogo.

“Lakini kuna kasa aina ya nne ambaye ni mdogo kuliko wote lakini ana kichwa kikubwa kuliko wote, anapatikana visiwa vya Shelisheli. Huyu anataga mayai kati ya 80 mpaka 200 ambayo ni mengi kuliko kasa wote duniani huku mgongoni akiwa na magamba 19 yanayofana na tailes na chakula chake kikuu ni dagaa kamba.

Aina ya tano na ya mwisho aliitaja kwa jina la kitaalam ‘lather burke’, anakula jelly fish pekee, ana ngozi laini, ana rangi nyeupe na nyeusi na ana matuta mgongoni.

Kasa wa Kijani

Kwa mujibu wa Hamis, Kasa huyo anaongoza kuwa na sumu nyingi baharini na ni mkubwa kuliko wote ambapo anazaliwa akiwa na milimita 40 na kuzeeka akiwa na urefu wa mita mbili na uzito wa tani moja huku akiwa na sifa ya kutaga mayai kati ya 60 hadi 65 pekee.

Faida za kasa

Kuna faida mbalimbali za kasa, zaidi kasa wanasaidia kuongeza mapato ya serikali kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni kupitia watalii na watafiti mbalimbali.

Kwa mujibu wa Hamisi, mbali ya fedha za kigeni, kuwepo kwa Kasa wa kijani katika eneo hilo kunasaidia utunzaji wa mazingira na kuimarisha mazalia ya samaki.

Anasema kasa hao wanapokula nyasi zilizopo baharini samaki wanapokwenda kuzaliana katika maeneo hayo mayai yao yanarutubishwa kupitia mionzi ya jua ambayo inapenya kwa urahisi kwenye maji.

“Kwa hiyo katika yale maisha ya kutegemeana, kasa wana faida kubwa kwa maana ya kuweza kusaidia viumbe wengine kuzaliana kwa kasi, na bahari yoyote ambayo inapatikana kasa ina urahisi wa samaki wa biashara na uhifadhi kuweza kuongezeka vizuri.

Kupotea vifaranga wa kasa.

Kwa mujibu Hamisi, Mara baada ya mayai kuenguliwa, vifaranga huwa na siku maalum ya kurudi baharini kuendelea na naisha yao.

Hata hivyo hatua yao ya kurudi baharini hukumbana na hatari ya kuliwa na viumbe wengine kama kenge, nyoka na kadhalika.

Kupotea kwa vifaranga hao wakati wanarudi baharini wakitokea ardhini walikozaliwa, inajulikana kama ‘Eco system’, kwa maana afe mmoja, amsaidie mwingine kuishi.

Hamisi anasema vifaranga hao hupotea kwa kuliwa na kenge, nyoka na viumbe na wanaoweza kuruka kiunzi hicho ni wachache zaidi na hiyo ndiyo sababu kubwa ya kasa kuwa miongoni mwa viumbe wachache duniani.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya