Tuesday, July 1, 2025
spot_img

FAHAMU ULIPO MBUYU WENYE TASWIRA YA BIKIRA MARIA

ARODIA PETER

KATIKA kitabu Kitakatifu cha Biblia, inaelezwa kwamba Mwenyezi Mungu aliumba dunia na vitu vyote vilivyomo. Na kamwe hakuwahi kukosea katika uumbaji wake.

Vitabu vya dini ya kikristo vinamtambua Bikira Maria kuwa mama yake Yesu Kristo na Kitabu cha Qur’an Tukufu kwa Waislam, ikimtambua kuwa mama yake Issa bin Mariam, huku akiheshimika kuwa Mama Bora.

Maeneo mengi duniani, hasa miongoni mwa wakristo, Bikira Maria ni mmoja wa watakatifu wanaoheshimika sana.

Ili kukamilisha ibada kwa mama huyo, wakristo wamekuwa wakitengeneza vitu mbalimbali ikiwa ishara ya kutegemea maombezi yake. Picha na taswira za Bikira Maria ni jambo lililozoeleka sana.

Lakini, katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni maajabu, taswira ya picha ya Bikira Maria, inayofanana na sanamu ambazo hutumika na wakristo kufanya ibada kwa bikira huyo, imegunduliwa kwenye mti wa mbuyu uliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Saadan wilayani Pangani, Tanga.

Taswira hiyo ambayo iligundulika mwaka 2019 ndani ya hifadhi hiyo, imetajwa kuwa ni maajabu mapya yanayoongeza upekee wa hifadhi hiyo kwa macho na masikio ya kawaida ya watalii wa ndani na nje ya Tanzania.

Taswira hiyo iliyokita katikati ya mti mkubwa wa mbuyu, inaonekana vizuri ukiwa umbali wa mita 100 mpaka 50, lakini kadri una- vyousogelea mbuyu huo, ndivyo inavyopoteza mwonekano wake.

Kwa wanaofahamu sanamu ya Bikira Maria, akiwa na mavazi yake yanayoanzia kichwani na kufika chini ya miguu, ndivyo sanamu hiyo inavyoonekana kwa uwazi.

Picha ya Bikira Maria

Ofisa Muhifadhi Idara ya Utalii, Hifadhi ya Saadani iliyo chini ya Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa), Daud Gordon, anaeleza kuwa taswira hiyo ya Bikira Maria, imekuwa kivutio kipya na inafaa kutumika kuwa nyenzo muhimu katika kukuza utalii wa kiimani na hata kuwa sehemu ya hija kwa waamini wa kikristo hususan, wanaomheshimu mama huyo kadiri ya mapokeo ya imani zao.

Gordon anaeleza kuwa taswira hiyo inaweza kuwapa wageni fursa ya kutafakari juu ya ukuu wa Mungu, uumbaji wake na imani wanazozishikilia, huku wakiwa katikati ya maajabu ya asili.

“Sanamu (taswira) hiyo inayoonekana katikati ya mti wa mbuyu, imeshuhudiwa na watalii mbalimbali wanaofika hapa. Hakika hili ni jambo la kipekee…”

“Siyo hadithi, bali ni uhalisia, niwaombe na kuwakaribisha watanzania waje kujionea maajabu haya ambayo yameonekana na kutambuliwa miaka ya karibuni,” anasema Gordon.

Hifadhi ya Saadani inapatikana katika mikoa ya Pwani Wilaya ya Bagamoyo na Tanga, wilaya za Pangani na Handeni, ni pekee nchini inayopakana moja kwa moja na Bahari ya Hindi, ambapo wanyama na binadamu hukutana kwenye ufukwe wa bahari kupunga upepo na kupumzika.

Saadani

Kwa mujibu wa mwongoza watalii katika eneo hilo, Fredy Nesto, taswira hiyo ya Bikira Maria iligundulika mwaka 2019, ikiwa katika mbuyu wenye zaidi ya miaka 100 na ambao historia inaonyesha ni kati ya miti ya mibuyu iliyo – tumika kunyongea watumwa.

Nesto alisema, tayari watalii kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufika kwenye eneo hilo na kulitumia kwa maombi mbalimbali na baadhi wanarudi kueleza, kushukuru kwa mafanikio waliyoyapata kulingana na imani zao baada ya kuufikia mbuyu huo.

Aidha, hifadhi hiyo pia inajumuisha historia mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara ya utumwa, makaburi saba ya wamisionari waliokuja kueneza ukristo katika ukanda wa Pwani wakiongozwa na mjerumani, James Lebman ambaye alifariki Februari 28 mwaka 1882 akiwa na miaka 45.

Maeneo ya Pwani mwanzoni yalitawaliwa na utawala wa kisultani ambao ulieneza Dini ya Kiislam kabla ya miaka ya 1880, walipoanza kuingia wamisionari wa kijerumani ambao hata hivyo hawakufanikiwa kueneza ukristo katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, mwili wa Lebman ulishindwa kusafirishwa kwenda kuzikwa kwao Ujerumani kutokana na ukosefu wa usafiri, kwani wakati huo hakukuwepo na ndege wala miundombinu rahisi kwa safari ya masafa.

MAKALA HAYA YALICHAPISHWA KWANZA KWENYE GAZETI LA PAMBAZUKO

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya