Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mei 6, 2025 amemteua Lazaro Jacob Twange kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Marehemu Gissima Nyamo-Hanga, aliyefariki dunia katika ajali ya gari mapema mwaka huu.
Kabla ya uteuzi huu, Twange alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo. Uteuzi wake unakuja wakati muhimu ambapo TANESCO, chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati, ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa nchi nzima.
Aidha, Shirika hilo pia lina jukumu kubwa la kupanua mtandao wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia miradi kama ya REA (Rural Energy Agency), pamoja na kusimamia uwekezaji katika vyanzo vya nishati mbadala kama vile umeme wa jua, upepo, na majimoto, ili kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati ya mafuta na kulinda mazingira.
Kupitia nafasi hii mpya, Twange anatarajiwa kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za umeme zaidi, kuongeza uzalishaji kupitia miradi mikubwa kama ule wa Julius Nyerere (JNHPP – Rufiji), na kuwezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 pamoja na Ajenda ya Mageuzi ya Sekta ya Nishati.