Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), umewatoa hofu wanachama wake na wananchi kwa ujumla kuhusu hali ya mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antipas Lissu, ukisema yuko salama.
Taarifa ya chama hicho inakuja kufuatia taarifa zilizokuwa zikienea tangu ijumaa April 18 2025 kupitia mitandao ya kijamii zikibainisha kutokuonekana kwa mwenyekiti huyo katika gereza ambalo amekuwa akishikiliwa la Keko.
Kupitia ukurasa rasmi wa instagram wa CHADEMA, wameandika wakisema kwamba viongozi wakuu wa chama chao walikutana na uongozi wa Jeshi la Magereza na kufahamishwa kwamba Tundu Lissu amehamishiwa katika gereza la Ukonga.
Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, imeeleza kwamba kufuatia taarifa hizo, sasa wanachama na wapenzi wa chama chao wanaweza kumtembelea mwenyekiti Lissu katika gereza la Ukonga badala ya Keko alikokuwa awali
Aidha makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara John Heche anatarajiwa kufika Gereza la ukonga mapema leo kwa ajili ya kumuona Tundu Lissu na kuzungumza nae kuhusu hali yake.
