Saturday, April 19, 2025
spot_img

DK. CHANA AWAASA MAKETE KUTOVAMIA MAENEO YA HIFADHI

ZERUBABEL CHUMA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amewaasa wananchi wa Makete, mkoani Njombe kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa na badala yake wayatumie kujiongezea kipato.

Ameyasema hayo jana alipokuwa akifungua semina ya kuwajengea uwezo wadau wa uhifadhi kuhusu uanzishaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) na mikakati ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu, inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete.

“Wilaya hii inapakana na maeneo yaliyohifadhiwa kama vile Hifadhi ya Taifa Kitulo, Pori la Akiba la Mpanga- Kipengele na misitu ya hifadhi ya Chimala, Maguli inasimamiwa na TFS na Msitu wa Living Stone na Ipuji unaosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Makete.

“Pia inapitiwa na ushoroba wa Ndukunduku unaounganisha Hifadhi ya Taifa Kitulo na Pori la Akiba Mpanga Kipengele hivyo ni muhimu kuyatunza na kuyalinda, tusiweke mashamba au makazi kwenye maeneo haya,” amesema Chana.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo amesema yatawawezesha washiriki kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, kupambana na masuala ya moto pamoja na uanzishaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori.

Aidha, Chana amesema ili kutatua changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za utatuzi ikiwemo kuendesha doria za ushirikiano wa taasisi za TAWA, TANAPA na Wilaya ya MAKETE; kutumia teknolojia katika udhibiti wa wanyamapori ikiwemo ndege nyuki, mikanda maalumu ya mawasiliano (GPS Satellite Collars), mabomu baridi na kutoa semina ya kujenga uelewa kwa maafisa wanyamapori 122 kutoka halmashauri za wilaya.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Maliasili), Benedict Wakulyamba amewahamasisha wananchi wa Makete kuanzisha eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori kutokana na uwepo wa Ushoroba wa Ndukunduku katika wilaya  hiyo.

Amesema mwaka wa fedha 2024/2025, wizara imepanga kuendelea kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali nchini kuhusu usimamizi wa WMA, Shoroba na mikakati ya kudhibiti migongano baina ya binadamu wa wanyamapori.

Mafunzo hayo yanawahusisha Makamishna Wasaidizi wa Kanda kutoka TAWA, TANAPA na TFS, wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, wadau wa uhifadhi wa kata za wilaya ya Makete, viongozi wa dini na serikali wa Wilaya ya Makete.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya