ZERUBABEL CHUMA
MRADI wa bwawa la kuzalisha umeme, megawati 2,115 wa Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika.
Hayo yamesemwa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni, Dodoma.
Alisema kukamilika kwa mradi huo uliogharimu Sh. trilioni 6.6 kumeongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kumechochea kasi ya maendeleo.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hadi Machi 2025, megawati 2,115 zimeunganishwa kwenye gridi ya Taifa ambazo zimeongeza kiwango cha upatikanaji umeme katika gridi hiyo hadi kufikia megawati 4,031.7.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni, Dodoma, jana.
Alisema kati ya Novemba, 2020 na Februari, 2025 serikali iliunganisha umeme katika vijiji 4,071 kwa gharama ya Sh. bilioni 1,593 na hivyo kuwezesha vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kuunganishiwa umeme.
Majaliwa alisema hatua inayofuata baada ya kukamilisha mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote ni kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo jumla ya vitongoji 33,657 kati ya 64,359, sawa na asilimia 52.3 vimeunganishiwa huduma ya umeme.
Kwamba usambazaji wa umeme katika vijiji na vitongoji utawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zinazohitaji Nishati ya Umeme, zikiwemo kuchomelea vyuma, useremala, kuchakata nafaka na kuchenjua madini.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Dotto Biteko (aliyeketi mbele) akisikiliza hotuba na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ilisomwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni, Dodoma, jana.