Friday, May 30, 2025
spot_img

IFAHAMU NJIA KUU YA WATUMWA ILIYOPO UJIJI, KIGOMA

NJIA kuu waliyopita watumwa mwishoni mwa karne ya 18 na mwanzoni mwa karne ya 19, bado ipo.

Njia hiyo ipo Manispaa ya Ujiji – Kigoma mkoani Kigoma ikianzia hapo Ujiji hadi Bagamoyo mkoani Pwani; na ndiyo njia pekee iliyopo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Njia kuu ya watumwa ya Ujiji hadi Bagamoyo ni urithi wa utamaduni wa Tanzania na imehifadhiwa na inatunzwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Miriam Mkonya, Mhifadhi Mkuu wa Malikale Makumbusho ya Dkt. Livingstone iliyopo Ujiji, Kigoma.

Miriam Mkonya, Mhifadhi Mkuu wa Malikale Makumbusho ya Dkt. Livingstone iliyopo Ujiji, Mkoa wa Kigoma anaizungumzia njia hiyo akieleza kuwa ilitumiwa na watumwa kusafiri pamoja na kusafirisha pembe za ndovu, mwishoni mwa karne ya 18 na mwanzoni mwa karne 19.

Mkonya anasema njia hiyo ilitengenezwa na wafanyabiashara wa kiarabu waliokuwa wakijihusisha na biashara ya utumwa na pembe za ndovu kuanzia mwaka 1847 hadi 1848 kwa kupanda miti ya miembe iliyokusudiwa kuonyesha njia ya kupita, kivuli na chakula cha watumwa wanapotoka Ujiji kuelekea Bagamoyo.

Hapa ndipo mahali inapoanzia njia kuu ya watumwa ya kutoka Mji wa Ujiji mkoani Kigoma hadi Bagamoyo mkoani Pwani.

Anasema watumwa waliotumia njia hiyo ni kutoka mataifa ya Tanganyika, Rwanda, Burundi na Umanyema, sasa inajulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

ā€œMji wa Ujiji ulikuwa kituo cha watumwa waliokusanywa kutoka ndani ya Tanganyika, umanyema, Rwanda na Burundi kabla ya kuanza safari ya kuelekea kituo cha mwisho cha Bagamoyo kwa upande wa Tanganyika ambako walipakizwa kwenye majahazi kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya kuuzwa.

ā€œZanzibar, watumwa walinunuliwa na wafanyabiashara kutoka mataifa ya Asia na Mashariki ya mbali.

ā€œNjia hii ndiyo pekee iliyopo hadi sasa katika nchi zote za ukanda wetu huu na ni urithi wa utamaduni wa Taifa. Inatuzwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na wadau wengine.

ā€œPamoja na njia hii, TANAPA pia inatunza na kuhifadhi kambi za watumwa za Kwihala iliyopo Mkoa wa Tabora, Kilimatinde mkoani Singida, Mpwapwa mkoani Dodoma, Mamboya iliyopo Mkoa wa Morogoro na Bagamoyo,ā€ anasema.

Mkonya anaeleza zaidi kuwa wafanyabiashara ya utumwa waliitengeneza njia hiyo ili waweze kukumbuka sehemu ya kupita kutoka Mji wa Ujiji hadi Bagamoyo na ilipandwa miti ya miembe kwa ajili ya chakula cha watumwa na kutengeneza kivuli wakati wa safari ya kutembea kwa miguu iliyochukua muda miezi mitatu kutoka Ujiji hadi kufika Bagamayo.

Mwongoza watalii katika Makumbusho ya Dkt. Livingstone, Kassim Govola yeye anasema mwaka 2014, akiwa ameambatana na watalii kutoka mataifa ya Ulaya,Ā alitembea kwa miguu katika njia hiyo kutoka Ujiji hadi Bagamoyo,Ā wakitumiaĀ Ā muda waĀ mwezi mmoja na siku sita.

Kabla yao, anasema mwaka 1990, mjukuu wa Dkt. Livingstone, Robert Livingstone alifika Ujiji na kuanza safari ya kutembea kwa miguu kwenye njia hiyo akianzia Ujiji hadi Bagamoyo.

Njia kuu wa watumwa ambayo imetengenezwa kwa kupanda miti pembeni. Watumwa walipita katikati ya miti hiyo kama barabara yao lakini pia matunda ya miti hiyo ambayo ni maembe waliyatumia kwa chakuila na majani yake kama kivuli.

ā€œHii ndiyo njia pekee ya watumwa iliyopo hadi sasa katika eneo lote la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Serikali na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wamefanya jambo zuri sana kuihifadhi na kuitunza njia hii.

ā€œHuu niĀ urithi wa utamaduni wa Taifa. Hakuna sehemu nyingine katika nchi hizo za Afrika ambako kuna njia waliyotumia watumwa kusafiri kwenda kuuzwa. Na pia njia hii ilitumiwa na wafanyabiashara wa wakati huo wa meno ya ndovu,Ā kuyasafirisha hadi Bagamoyo kabla ya kuyapakia kwenye majahazi kwa ajili ya kuyapeleka sehemu mbalimbali duniani.

ā€œTanzania pekee ndiyo inao urithi huu wa kitamaduni ukiwa halisi kama ulivyotengenezwa wakati huo na babu na bibi zetu wakisafirishwa kama watumwa,ā€ anasema Govola.

Anasema watalii kutoka Marekani na Uingereza ndiyo hufika kwa wingi kutalii kwenye njia hiyo na hasa wanafunzi ambao hutaka kuiona njia halisi iliyotumiwa na watumwa.

ā€œIpo haja kwa shule zetu hapa nchini kuwaleta wanafunzi kufanya utalii wa kimasomo katika njia hii, kwani badala ya kusoma tu darasani wakifika hapa wataiona njia halisi wanayojifunza darasani.

ā€œKama mjukuu wa Dkt Livingstone alifika Tanzania na kuja Ujiji ili kuona njia ambayo babu yake alipita wakati wa uhai wake akiwa katika harakati zake za kuokoa watumwa kutoka kwenye minyororo ya utumwa, kwanini watoto wetu tusiwalete kujifunza hapa kwa kuiona njia waliyopita babu na bibi zao?ā€ anasema.

HII NI FUSRA KWA WANAFUNZI NA WALIMU KOTE NCHINI KWENDA UJIJI, KIGOMA KUFANYA UTALII WA KIMASOMO.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya