Thursday, April 10, 2025
spot_img

KITANDA CHA JIWE CHA CHIFU MKWAWA HIKI HAPA

CHIFU Mtwa Mkwawa alilala kwenye jiwe kwa muda wa miaka minne, wakati akipigana vita vya msituni na wakoloni wa Kijerumani.

Jiwe hilo lipo kijiji cha Mlambalasi mkoani Iringa, karibu na lilipo kaburi kilimozikwa kiwiliwili chake, baada ya kujiua kwa kujipiga risasi.

Yeyote anayetaka kuliona jiwe hilo ambalo lilikuwa kitanda cha Chifu Mkwawa kwa muda wa miaka minne anapaswa kutembelea Makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa, iliyopo Kalenga, mkoani Iringa.

Chifu Mkwawa kichwa chake kilikatwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1898, baada tu ya kujiua na kupelekwa Ujerumani na baadaye mwaka 1954, fuvu la kichwa chake lilirudishwa na kuhifadhiwa kwenye makumbnushi yake hiyo iliyopo Kijiji cha Kalenga mkoani Iringa.

Chifu Mkwawa alianza kulala kwenye jiwe mwaka 1894 alipokimbilia msituni baada ya kushambuliwa na wakoloni wa Kijerumani wakisaidiwa na wapiganaji wa machifu waliokuwa jirani na himaya yake, aliopigana vita nao na kuwashinda.

Kaburi hili hapo juu ndipo kimezikwa kiwiliwili cha Chifu Mtwa Mkwawa aliyejiua kwa kujipiga risasi kisha kichwa chake kikakatwa na wakoloni wa Kijerumani. Kaburi hili lipo Kijiji cha Mlambalasi mkoani Iringa.

Himaya ya Chifu Mkwawa ilivamiwa na Wajrumani kutokea milima ya Sao Hill. Wajerumani  walionyesha njia hiyo ya milimani na machifu waliokuwa wakiwasaidia kupigana na Chifu Mkwawa.

Wajerumani waliiendea ngome ya Chifu Mkwawa kwa kivizia, wakitembea milimani usiku ili wapiganaji wa Chifu Mkwawa wasiwaone.

Mwanahistoria Zuberi Witala anaeleza kuwa Wajerumani waliambiwa na machifu hao kuwa hawawezi kupigana na Chifu Mkwawa wakamshinda iwapo atajua anakaribia kuvamiwa naye akapata muda wa kujiandaa na majeshi yake kwani alikuwa na mbinu nyingi za kivita, hivyo ili kumshinda ni lazima kumshambulia kwa kumshtukiza.

Mwanahistoria Zuberi WItala.

Wajerumani na wapiganaji wa machifu hao walipofika Mlima wa Tosamaganga waliweka kambi na kuandaa zana zao za kivita hasa mizinga ambayo ilielekezwa kambi ya Lipuli.

Witala anasema kambi ya Lipuli ilianza kushambuliwa kwa mizinga na mabomu ya kutupa kwa mkono Oktoba 28, 1894.

Wapiganaji wa Chifu Mkwawa na wahehe walikufa wengi kwa sababu walidhani mabomu ya kutupa kwa mkono ni mawe hivyo hawakuwa na tahadhari nayo na wengine waliyachukua wakitaka kuyarusha uelekeo wa Wajerumani wakidhani kuwa ni mawe lakini yaliwalipukia na kuwaua.

Wajerumani waliishambulia ngome ya Lipuli kwa siku mbili mfululizo na ilipofika Oktoba 30, 1894, Chifu Mkwawa alibaini kuwa hali ya vita kwa upande wake siyo nzuri.

Witala anasema, Chifu Mkwawa alilipua silaha alizoteka kwa Wajerumani katika vita ya 1891 ili wasiweze kuzitumia tena, kisha akaondoka kwenye ngome yake na kukimbilia msituni.

Silaha zilizolipuwa na Chifu Mkwawa ziliwashtua Wajerumani wakadhani Mkwawa naye ameanza kuwashambuliwa kwa  mizinga na wakati wakiwa kwenye mshangao huo huku wengine wakikimbia kurudi nyuma, ndipo yeye na wapiganaji wake aliokuwa nao ndani ya ngome ya Lipuli walifanikiwa kutoka na kukimbia hadi Mto Ruaha ambako walivuka na kuelekea Mlambalasi

Mwanahistoria Witala anasema Chifu Mkwawa baada tu ya kuvuka Mto Ruaha, alikutana na mwanajeshi wa Kijerumani aliyekuwa na cheo cha Luteni na kumtaka ajisalimishe ili amchukue akiwa hai ampeleke kwa kamanda wake aliyekuwa amempa kumkamata akiwa hai.

Eneo la Mto Ruaha ambalo Luteni wa Kijerumani alishambuliwa kwa mkuki na kuuawa papo hapo na Chifu Mtwa Mkwawa baada ya kujaribu kumuweka chini ya ulinzi. Mwanajeshi huyo wa kikoloni alizikwa pembeni ya njia ya maji ya Mto Ruaha.

Anasema kosa alilofanya Luteni huyo wa Kijerumani ni kumtaka Chifu Mkwawa anyooshe mikono juu bila kumuamuru kutupa mkuki wake kwani wakati akinyoosha mikono juu aliimrushia mkuki kwa mkono wake uliokuwa na misuli imara na kumuua papo hapo. Luteni huyo wa Kijerumani alizikwa ng’ambo ya Mto Ruaha, mahali alipouawa.

Chifu Mkwawa akawa amekimbilia msituni ambako alianza upya kupigana vita na wakoloni wa Kijerumani.

Witala anasema, Chifu Mkwawa akiwa msituni, alichimba mashimo, akategesha mikuki yenye sumu na kuifunika kwa majani, mbinu ambayo Wajerumani hawakuijua hivyo walipokuwa wakipita kwenye njia zenye mitego yake, wengi walikufa.

Baada ya Wajerumani kuona  wanakufa kwa wingi katika vita ya msituni walisitisha kumsaka msituni na kurudi kwa machifu waliowasaidia kuishambulia ngome ya Lipuli kuwaomba msaada.

Kitanda cha jiwe kilicho chini ya pango ambacho Chifu Mtwa Mkwawa alilala kwa muda wa miaka minne wakati akipigana vita vya msituni na Wajerumani kilikuwa na njia ya kutoroka na kutokea upande wa pili wa mlimani iwapo angeshambuliwa ghafla na maadui.

Mwaka 1896, Wajerumani waliingia makubaliano na machifu hao ambao mwanahistoria Witala anawataja kuwa ni Chifu Melele, Chifu Begele wa Kilosa na Chifu Lupembe ambao waliingiza msituni vikosi vya wapiganaji wao kuwasaidia Wajerumani kupambana na Chifu Mkwawa lakini bado walishindwa huku wengi wakiuawa.

Kushindwa vita ya msituni kwa Wajerumani na muungano wa machifu maadui wa Chifu Mkwawa kuliwafedhehesha Wajerumani wakaanza kuwaua ndugu zake wakiwalazimisha wasema mahali alipokuwa amefijicha na siri za mbinu zake za kivita.

Baada ya Mkwawa kupata taarifa za kuwepo kwa muungano wa majeshi ya machifu na Wajerumani dhidi yake, aliandika barua kwa Lugha ya Kiarabu kwenda kwa mwakilishi wa wakoloni kutoka Ulaya aliyekuwepo Tanganyika wakati huo kutathimini mwenendo wa utawala wa Wajerumani.

Ramani ya ngome ya Chifu Mkwawa ya Lipuli.

Barua iliyoandikwa na Chifu Mtwa Mkwawa kwa Lugha ya Kiarabu.

Katika barua hiyo, Chifu Mkwawa alikuwa akimuomba mkoloni huyo awaelekeze wakoloni wenzake wasitishe vita naye kwa muda ili apambane kwanza na majeshi ya machifu waliokuwa wakiwasaidia Wajerumani na akishamalizana nao, ndipo vita yake na Wajerumani iendelee.

Barua hiyo haikumfikia mkoloni huyo hivyo Chifu Mkwawa aliendeleza vita vya msituni hadi 1898 alipopata taarifa kuwa mdogo wake, alikamatwa na kunyongwa na Wajerumani baada ya kukataa kutoa siri za mbinu zake za kivita.

Mawe haya yaliyozungukwa na msitu wa miti ambamo chini yake kuna pango kubwa yapo Kijiji cha Mlambasi, Iringa mahali alipokuwa akilala Chifu Mkwawa kwenye kitanda cha jiwe, walinzi wake walikaa juu ya mawe hayo kumlinda akiwa amelala.

Chifu Mkwawa akajua kuwa hawezi tena kupambana na kuwashinda Wajerumani wakati ndugu zake wakiuawa kikatili.

Mnara huu ulijengwa wakati wa kumbukumbu ya kutimia miaka 100 tangu Chifu Mtwa Mkwawa alipojiua kwa kujipiga risasi. Umejengwa pembeni ya kaburi kilimozikwa kiwiliwili chake katika kijiji cha Mlambalasi mkoani Iringa.

Witala anasema Chifu Mkwawa aliumizwa sana na kuuawa kwa mdogo wake, akaamua na yeye kujiua. Kwamba alikoka moto mkubwa, akaanza kuvua mavazi ya kichifu na kuyachoma moto, akampiga risasi mlinzi wake mwaminifu akamuua, kisha akakaa pembeni ya moto aliokuwa amekoka, naye akajipiga risasi, akafa.

HISTORIA HII UNAWEZA KUIPATA VIZURI UKITEMBELEA MAKUMBUSHO YA CHIFU MTWA MKWAWA, ILIYOPO KALENGA MKOANI IRINGA.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya