Wednesday, March 12, 2025
spot_img

TUMERITHISHWA LUGALO, TWENDENI KABURI LA NYUNDO

This image has an empty alt attribute; its file name is makala-LOGO-4-1024x197.jpg

SHIRIKA LA Hifadhi za Taifa (TANAPA), limefungua milango ya Lugalo mkoani Irnga. Eneo la kihistoria lilipo kaburi ya Nyundo, alikozikwa Kamanda wa Majeshi ya Kijerumani, Emil Von Zelewisk na wanajeshi wake zaidi ya 300 waliouawa na wapiganaji wa Chifu Mtwa Mkwawa katika uwanja wa mapambano wa Lugalo.

TANAPA limefungua milango ya Lugalo ili watalii wa ndani na nje ya nchi waweze kwenda kutalii eneo hilo ambalo ndilo pekee katika Bara la Afrika lililohifadhi urithi wa ujasiri na maarifa ya kivita ya wapiganaji wa Kiafrika katika medani za vita.

Lugalo ni eneo ambalo kila mtu duniani anapaswa kulitembelea. Kwa wanajeshi, polisi na wapiganaji wengine, mbali ya kwenda kutalii, Lugalo kwao ni eneo la kuhiji na kujifunza maarifa ya kivita na kwa watalii wengine; kama Diaspora, waandishi, wanahistoria, wanafunzi wa ndani na nje na makundi mengine; Lugalo, ndilo eneo ambalo wakilitembelea, linabaki likiishi katika kumbukumbu zao.  

Watalii wanapata fursa ya kufika uwanja wa vita wa Lugalo na kaburi la Nyundo, wakifika kwanza Makumbusho ya Chifu Mkwawa iliyopo Kalenga, Iringa. Wakiwa hapo wanapewa fursa ya kufika eneo hilo kwa gharama nafuu sana.

Ukifika Lugalo utafahamu kuwa tangu miaka ya 1800, Afrika ilikuwa na maafisa mawasiliano na wapelelezi; na aidha utafahamu kwamba Jeshi la Chifu Mkwawa ndilo kielelezo cha kuwepo kwa teknolojia ya hali ya juu ya kijeshi duniani hivi sasa.

Kamanda wa majeshi ya Ujerumani aliyeuawa katika Uwanja wa Vita wa Lugalo na wapiganaji wa Chifu Mkwawa mwaka 1891, Emil Von Zelewisk. Picha hii imehifadhiwa Makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa iliyopo Kalenga, Iringa.

Kuifahamu kwa ufasaha Lugalo na Kaburi la Nyundo, Mwanahistoria Zuberi Suleimani Witala, aliyepo Lugalo, Iringa anaeleza kuwa mwaka 1891 maafisa mawasiliano wa Chifu Mkwawa walimpelekea taarifa kuwa wanajeshi wa Kijerumani wameonekana Kilosa, Morogoro wakielekea kwenye himaya yake Iringa.

Watalii wa ndani wakielekea eneo la uwanja wa vita la Lugalo.

Witala anasema kikosi cha mawasiliano cha Chifu Mkwawa kiliitwa Vanyigendo.

Kikosi hicho kilikuwa kikifanya kazi pamoja na kikosi cha wapelelezi kilichoitwa Vanyamapelela.

Vanyigendo walitoka Kilosa, Morogoro wakikimbia mbio za kupokezana kijiti. Maafisa mawasiliano wa Chifu Mkwawa walikuwa na vituo karibu kila kijiji kutoka himaya moja hadi nyingine na mpango huo wa mawasiliano ulibuniwa na Chifu Mkwawa.

Anasema taarifa kutoka Kilosa zilipelekwa kwa Chifu Mkwawa kwa kukimbia mbio, kutoka kijiji kimoja hadi kingine ambako zilipokelewa na afisa mawasiliano aliyekuwa hapo naye akatoka mbio hadi kijiji kinachofuata kukabidhi taarifa kwa mwenzake, naye alianza mbio kupeleka taarifa kijiji  alicho mwenzake wa mbele hadi kumfikishia Chifu Mkwawa.

Chifu Mkwawa baada ya kufikishiwa taarifa hizo, aliviandaa vikosi viwili vya makomandoo wake vilivyoitwa Vamalavanu na Vanyakilando. Waliondoka kutoka Ngome ya Lipuli iliyopo Kalenga hadi Lugalo, hapo wakaweka kambi na kuanza kujiandaa kwa vita.

Uwanja wa Vita wa Lugalo, mahali lilipo Kaburi la Nyundo

Chifu Mkwawa ambaye alikuwa ‘bwana mipango wa vita,’ aliwaamuru makamandoo wake kufyeka eneo la msitu liwe kama njia, kazi hiyo ilifanyika haraka kisha alitoa mchoro wa vita  kuwa makomandoo hao walale pembeni ya njia iliyofyeka na wafunikwe kwa majani.  

Komandoo mmoja akapewa Gobole, akaelekezwa apande juu kabisa ya mti awe anawaangalia wanajeshi wa Kijerumani wanavyokuja, akiona wote wameingia kwenye uwanja wa mapambano ampige risasi wa mwisho na hiyo ndiyo ishara kwa makomandoo waliofunikwa majani kuibuka kuanza kupambana na Wajerumani ana kwa ana.

Mwanahistoria huyo anasema kikosi cha kwanza cha wanajeshi wa Kijerumani kiliingia chote kwenye eneo lililofyekwa ambalo ndilo liliandaliwa na Chifu Mkwawa kwa ajili ya vita.

Kikosi pili kabla hakijaingia, Kamanda wa Jeshi la Wajerumani, Von Zelewesk ambaye alikuwa kwenye kikosi cha kwanza, aliona bata akinywa maji, akampiga risasi ili awe kitoweo chake.

Risasi ile iliwaibua makomandoo wa Chifu Mkwawa kutoka kwenye nyasi walizokuwa wamejificha wakidhani kuwa imepigwa na komandoo mwenzao na hapo vita kali ikaanza.

Kikosi cha wanajeshi wa Ujerumani kilikuwa na wapiganaji zaidi ya 300, wote walikuwa watu wa miraba minne hivyo mapambano yalikuwa makali. 

Kaburi la Nyundo.

Kamanda Zelewisk aliuawa baada ya kupigwa mkuki wa kwenye makalio ambao aliukalia ukaingia moja kwa moja hadi tumboni, akafa hapo hapo.

Baada ya kikosi hicho cha wanajeshi zaidi ya 300 kuteketezwa na makomandoo wa Chifu Mkwawa, Komandoo aliyekuwa juu ya mti aliwaeleza wenzake kuwa kuna kikosi kingine kinakuja na kwamba risasi ile hakuifyatua yeye bali kamanda wa wanajeshi wa Ujerumani.

Chifu Mkwawa na jeshi lake walisonga mbele kwenda kukabiliana na kikosi cha pili cha wanajeshi wa Kijerumani ambacho kilikuwa na mabomu na mizinga.

Katika mapambano hayo makomandoo wengi wa Chifu Mkwawa waliuawa.

Chifu Mkwawa baada ya kuona mwenendo wa vita si mzuri kwa jeshi lake, aliagiza kikosi chake kingine cha makomandoo waliokuwa wanakunywa dawa iitwayo Lyambambalo waende uwanja wa mapambano..

Hicho kilikuwa kikosi maalumu cha makomandoo wa Chifu Mkwawa na ndiyo pekee  walikuwa wakinywa dawa ya Lyambambalo; dawa ambayo hukwepesha shabaha ya risasi.

Majina ya Makamanda wa Jeshi la Kijerumani yaliyo kwenye kaburi la Nyundo. Makamanda hao waliuawa na wapiganaji wa Chifu Mkwawa katika vita ya Lugalo iliyopiganwa mwaka 1891.

Anasema makomandoo hao walipofika na kuingia kwenye uwanja wa mapambano, Wajerumani walishangaa kila wakiwalenga kwa risasi zinapita pembeni, wanasonga mbele kuwashambulia. Wanajeshi wengi wa Kijerumani wakauawa.

Ikatolewa amri na kamanda wa Kijerumani aliyekuwapo baada ya Zelewisk kufa kuwa, kikosi cha Chifu Mkwawa kilichokuja ni cha majini, siyo watu wa kawaida, kitawaangamiza hivyo wakimbie kusalimisha roho zao. Wajerumani wakakimbia wakiacha nyuma mizinga, mabomu na bunduki zao.

Katika mapambano hayo, Makomandoo wa Chifu Mkwawa  waliua wanajeshi wengine wa Kijerumani zaidi ya 190 na kukamata mateka 10 waliokuwa wamejeruhiwa vibaya.

Mateka hao wa Kijerumani walichukuliwa hadi uwanja wa mapambano ilipopiganwa vita ya kwanza eneo la Lugalo lakini  walipoona wenzao walivyouwa kwa risasi na mabomu ya Wajerumani, hasira ziliwapanda, wakawaua mateka wote wa Kijerumani.

Mizinga 10 ya Wajerumani ilitekwa pamoja na bunduki na risasi, silaha hizo zilipelekwa mbele ya Chifu Mkwawa aliyekuwapo eneo la uwanja wa mapambano Lugalo; akawauliza walipo mateka wakamjibu wamewaua wote.

Chifu Mtwa Mkwawa.

Chifu Mkwawa akawaambia makomandoo wake kuwa wamefanya kosa kubwa kuwaua kwa sababu mateka hao ndiyo wangewafundisha kutumia silaha walizoziteka.

Chifu Mkwawa akawaamuru wapiganaji wake kupeleka silaha hizo kwenye ngome ya Lipuli, huko Kalenga.

Baadaye; baada ya Chifu Mkwawa kujiua mwaka 1898 akiwa msituni, Wajerumani walikwenda uwanja wa mapambano Lugalo kuokota mifupa ya wenzao waliokufa katika mapambano ya awali.

 Witala anasema zaidi ya mabaki ya mifupa ya Wajerumani 500 iliokotwa na kuzikwa kwenye kaburi la Nyundo lakini pia ilizikwa mifupa mingine zaidi ya 4500 ya wapiganaji kutoka Sudan na sehemu nyingine za Afrika waliokuwa wakipigana bega kwa bega na Wajerumani.

Kwa mujibu wa Witala, Kamanda  Zelewisk alifahamika kama kamanda katili ambaye alikuwa akiua watu kwa kuwapiga  nyundo kichwani na hiyo ndiyo sababu kaburi alilozikwa pamoja na wanajeshi wake likaitwa kaburi ya Nyundo.

TWENDENI KABURI LA NYUNDO LILILOPO LUGALO, IRINGA TUKAJIONEE MAAJABU YA MASHUJAA WA KITANZANIA.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya