
HISTORIA iliyosahaulika ya mwisho wa maisha ya mama mzazi wa Chifu Mtwa Mkwawa wa Kabila la Wahehe, imerejeshwa.
Hivi sasa, mtalii anayetembelea Makumbusho ya Chifu Mkwawa iliyopo Kijiji cha Kalenga, mkoani Iringa anaweza pia kulitembelea eneo ambalo mama mzazi wa Chifu Mkwawa alipotelea, mwaka 1889.
Mama mzazi wa Chifu Mkwawa hakufa kifo cha kawaida, bali alipotelea kwenye kijito cha maji alikojitumbukiza na mwili au sehemu za mabaki ya mwili wala mifupa yake havikupatikana hivyo kijito hicho ndicho kinachotambulika kama kaburi lake.
Kijito hicho kipo eneo la Kikongoma, pembeni ya Daraja la Mungu ambalo maji ya Mto Ruaha hupita chini yake. Eneo hilo linasimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Jenerali Mstaafu, George Waitara. Katika kipindi alichoongoza Bodi ya Wakurugenzi ya TANAPA, shirika hilo limepata mafanikio makubwa.
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linalosimamia Makumbusho ya Chifu Mkwawa, sasa linatoa fursa kwa watalii wanaotembelea makumbusho hiyo, pia kwenda kulitembelea eneo la Kikongoma alikopotelea mama yake Chifu Mkwawa ambaye chanzo cha kupotea kwake ni kuficha siri za uchifu wa Kabila la Wahehe.
TANAPA inawawezesha watalii wa ndani na nje kufika Kikongoma wakiongozwa na waongoza watalii wa shirika ambako hulipa ada ya kiingilio; Shilingi 2,000 tu.
Mhifadhi wa Malikale Daraja la Pili Makumbusho ya Mtwa Mkwawa, Paulo Mathias Mduma ambaye amezungumzia kurejeshwa kwa historia ya mwisho wa maisha ya mama mzazi wa Chifu Mkwawa katika kitita cha utalii kwenye makumbusho ya Chifu Mkwawa anasema, uamuzi huo wa TANAPA umeongeza kwa kiasi kikubwa watalii wanaotembelea makumbusho hiyo.

Paulo Mduma, Mhifadhi Malikale Daraja la Pili, Makumbusho ya Mtwa Mkwawa.
“Uongozi wa sasa wa TANAPA unajua namna ya kuvutia watalii, unafanya kazi nzuri sana. Hapo mwanzo hatukuwa na watalii wengi lakini hivi sasa kitita cha utalii kwenye makumbusho hii kimeongezwa, watalii wanamiminika kwa wingi na tumekuwa busy na wageni.
“Mtalii anayetembelea makumbusho hii, anapata fursa ya kujua mambo mengi ya Chifu Mkwawa lakini zaidi ya hapo, anapewa pia fursa ya kwenda eneo la Kikongoma ambako mama yake mzazi na Chifu Mkwawa alipotelea.
“Historia ya mama huyo inasisimua na kuvutia sana hivyo watalii wengi wamekuwa na hamu ya kuisikia na kuona eneo alikopotelea. Hilo eneo lipo chini ya Halmashauri lakini TANAPA imejenga ushirikiano mzuri sana na wadau wengine wa utalii hivyo huwa inatoa maafisa wake, wanawapeleka watalii huko Kikongoma ambako hulipia ada ya Shilingi 2,000 tu kama kiingilio kwenye eneo hilo.
“Maafisa wa TANAPA huwapitisha watalii hatua kwa hatua kwenye historia ya mwisho wa maisha ya mama mzazi wa Chifu Mkwawa,” anasema Mduma.
Historia ya mwisho wa maisha ya mama mzazi wa Chifu Mkwawa iliyotolewa na mwongoza watalii wa Makumbusho ya Chifu Mkwawa, Aneth Kibitanyi inaonyesha kuwa mama huyo alikuwa mtaalamu wa tiba za jadi na alikuwa na siri za uchifu wa Wahehe.

Aneth Kibitanyi, mwongoza watalii katika Makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa iliyopo Kalenga, Mkoa wa Iringa akitoa maelezo kwa watalii waliotembelea eneo la Kongomela, alikopotelea mama mzazi wa Chifu Mkwawa.

Kibitanyi anasema neno Kikongoma maana yake ni kutokomea au kupotea. Eneo hilo lina chemchem inayotoa maji ya moto yanayoweza kuchemsha yai likaiva na hatua chache kutoka eneo lililo na maji moto, kuna maji baridi.
Ni eneo lililo chini ya njia ya maji yanayopita chini ya mawe makubwa yaliyojipangwa vizuri juu ya ardhi na yanatumiwa na wenyeji kama daraja na kuvuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Daraja hilo linaitwa Daraja la Mungu kwa sababu lilikuwepo tangu enzi na enzi na linaendelea kuwepo. Halikujengwa na binadamu.

Sehemu ya Mto Ruaha inayopita katika eneo la Kongomela
Maji moto ya Mto Kikongoma yanaaminiwa na wengi kuwa yana uwezo wa kuondoa mikosi na watalii wengi wa ndani na nje wanaofika eneo hilo wamekuwa wakiyachota na kuondoka nayo na wengine hunawa usoni.

Maji ya moto yanayotoka kwenye Chemchem iliyopo Kongomela. Maji haya yalikuwa yakitumiwa na mama yake Chifu Mkwawa kuchemsha dawa.
Kibitanyi anasema maji moto kutoka kwenye chemchem hiyo ndiyo ambayo mama yake Chifu Mkwawa alikuwa akiyatumia kuchemsha dawa zake kwa ajili ya tiba za machifu na watu wengine.
Anasema, safari ya mwisho wa maisha ya mama yake Chifu Mkwawa ilianzia nyumbani kwake baada ya kutekwa na kijana aliyemlea kama mtoto wake anayemtaja kwa jina la Mwambambe.
Kwamba Mwambambe, kijana wa Kinyamwezi aliyeokotwa na baba yake Chifu Mkwawa, Chifu Mnyigumba alilelewa na mama yake Chifu Mkwawa na kuozeshwa dada yake Mkwawa.
Mwambambe alikuwa na tamaa ya kuwa Chifu wa Kabila la Wahehe na alijua hilo atalifanikisha iwapo atapata dawa kutoka kwa mama yake Chifu Mkwawa.
Kibitanyi anaeleza kuwa Mwambambe alikuwa kijana mwenye miraba minne na alimzidi umri Chifu Mkwawa, lakini walikuwa marafiki wakiishi kama mtu na mdogo wake. Alipendwa sana na Chifu Mnyigumba kwa sababu alikuwa hodari wa kupigana vita.
Mwambambe alikuwa na uwezo wa kudaka kwa mikono yake mikuki au mishale 10 kwa wakati mmoja aliyoshambuliwa nayo na adui zake na kuitumia kuwashambulia. Chifu Mnyigumba alimuozesha Mwambambe binti yake ambaye ni dada yake Chifu Mkwawa.
Akiwa sehemu ya familia ya Chifu Mnyigumba, Mwambambe alijua siri nyingi za familia ya kichifu ikiwemo ya mrithi wa kiti cha uchifu kuwa ni lazima awe mtoto wa kwanza wa kiume wa Chifu na kwa sababu alijawa na tamaa ya kuwa Chifu alianza kupanga mipango ya kumuua Chifu Mkwawa.
Wazee wa Kihehe walibaini mipango miovu ya Mwambambe ya kutaka kumuua Mkwawa lakini hawakumwambia Chifu Mnyigumba kwa sababu alikuwa akimpenda sana Mwambambe. Walichokifanya, walimtorosha Mkwawa wakampeleka Nzuguni, Dodoma kulelewa huko na mjomba wake.
Chifu Mnyigumba alipofariki dunia, Mwambambe alimteka mama yake Mkwawa akamlazimisha ampeleke mahali ambako huwa anachimba dawa wanazopewa machifu ili zimsaidie yeye kutawazwa kuwa Chifu wa Kabila la Wahehe badala ya Mkwawa.

Jiwe ambalo mama yake Chifu Mkwawa alivua nguo zake zote na kuziweka juu yake kabla ya kujirusha kwenye kijito kilicho chini ya mawe na kutoweka moja kwa moja.
Mama yake Mkwawa akiwa mateka alijaribu kutafuta njia za kujinasua bila mafanikio kwa sababu Mwambambe alikuwa jitu la miraba minne hivyo alikubali kwenda kumuonyesha dawa hizo.
Walianza safari hiyo wakiwa na wasaidizi wachache wa mama yake Mkwawa na moja kwa moja walielekea Kikongoma, walipofika eneo la chemchem ya maji moto alimuonyesha na kumwambia kuwa hapo ndipo dawa za kichifu zinachemshwa.
Kibitanyi anasema, Mwambambe akiwa na matumaini makubwa ya kupata dawa za kichifu kutoka kwa mama yake Mkwawa, aliombwa na kukubali na mama huyo abaki mahali hapo kwa sababu sehemu anayokwenda kuchukua dawa hizo anapaswa kwenda akiwa mtupu, bila nguo hata moja hivyo Mwambambe ambaye ni mwanaye aliyemlea na pia mkwewe, hapaswi kumuona akiwa mtupu.

Mlango wa kuingia kwenye mto alijitumbukiza mama yake Chifu Mkwawa
Mama yake Mkwawa aliongozana na wasaidizi wake wachache aliokuwa nao kwenda umbali mdogo kutoka chemchem ya maji moto kisha akawaaga kuwa anakwenda zake, anatokomea kwa sababu hawezi kutoa siri ya uchifu wa Wahehe kwa mgeni wa kabila la Wanyamwezi.

Mto ulio chini ya mawe katika eneo la Kongomela ambao mama yake Chifu Mkwawa alijirusha na kutokemea.
Alivua nguo zake zote akaziweka juu ya jiwe, kisha akajirusha kwenye mto wa maji unaopitisha maji chini ya mawe ya Daraja la Mungu, akatoweka au kwa Lugha ya Kihehe akakongomela.
Hakuonekana tena, wala mabaki ya mwili wake au mifupa yake haijapata kuonekana hadi leo na hivi sasa eneo hilo linatumiwa na Wahehe kama sehemu ya kufanyia matambiko.
Jiwe ambalo mama yake Chifu Mkwawa aliweka nguo zake baada ya kuzivua ili “akongomele” limehifadhiwa vema na imewekwa amri kuwa ukifika kwenye jiwe hilo kabla ya kwenda eneo alilopotelea mama yake Mkwawa ni lazima uchume jana na kuliweka kwenye jiwe hilo ikiwa ishara ya heshima kwa mama huyo.

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji.
Baada ya TANAPA kuwezesha watalii wengi wa ndani na nje kuanza kufika eneo hilo na kujifunza historia, Kibitanyi anasema wapo waandishi na wanahistoria kutoka mataifa ya Ulaya waliofika kwa ajili ya kukusanya taarifa za mama huyo.
Anasema waandishi wamefika kukusanya taarifa kwa ajili ya kuandika habari na vitabu na wanahistoria wamekuwa wakifanya utafiti wa kupotelea mtoni kwa mama yake Chifu Mkwawa kisha mabaki ya mwili wake au mifupa yake vizipatikane huku wengine wakieleza kuwa matukio kama hayo wa watu kupotea kimiujiza yalitokea kwa manabii waliokuwa wakizungumza moja kwa moja na Mungu.
Hata hivyo, kumekuwepo na utata kuhusu mwaka aliopotea mama yake Mkwawa kwani wapo wanaosema alipotea mwaka 1889 na wengine mwaka 1879.
TEMBELEA MAKUMBUSHO YA CHIFU MTWA MKWAWA ILIYOPO KIJIJI CHA KALENGA, MKOA WA IRINGA KUJIONEA URITHI WA HISTORIA YA KUSISIMUA NA KUVUTIA YA MAMA MZAZI WA CHIFU MKWAWA.