
KAMA unataka kujua dawa mujarabu ya kumtambua mwanamke anayechepuka kwenye ndoa yake, tembelea makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa iliyopo Kijiji cha Kalenga, mkoani Iringa.
Ukiwa ndani ya makumbusho hiyo, pia utavijua vifaa vya sayansi ya Kiafrika viliyotumiwa na Chifu Mkwawa kutambua eneo walipo maadui zake viliyoitwa Luhemelo na utaona na kujifunza kuhusu Vinyantilo na Utuli na Mtwango.
Ni mambo ya kuvutia sana ambayo hayapatikani sehemu nyingine yoyote duniani isipokuwa Kalenga, Iringa mahali lilipohifadhiwa fuvu la kichwa cha Chifu Mkwawa, Kamanda wa Jeshi la Lipuli aliyeteketeza majeshi ya Kijerumani na kuteke zana zake za kivita.
Iko hivi; Chifu Mkwawa wa Himaya ya Uhehe alioa wake 62 na kabla ya kufanya tendo la ndoa na mke wake aliyemuhitaji, alimpima kwa kutumia vyungu vinne vidogo vilivyounganishwa ili ajue kama amechepuka. Vyungu hivyo (vilivyo juu kwenye picha kubwa) viliitwa Lifugo.
Vyungu Lifugo vilikuwa vinatoa majibu sahihi ya vipimo kwa kila mke wa Chifu Mkwawa aliyepimwa na upimaji ulifanywa na wanasayansi wa Sayansi ya Kiafrika waliobobea kwenye tiba za wanawake.

Kezia Felix Sanga, mwongoza watalii katika Makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa iliyopo Kijiji cha Kalenga, Mkoa wa Iringa ambaye ametoa simulizi iliyoandikwa kwenya makala haya.
Vyungu vitatu vilikuwa vinawekewa maji na kimoja cha katikati kiliweka dawa. Upimaji ulifanyika kwa kuwaita wanawake watatu, kila mmoja alisimama pembeni ya chungu kimoja kilichowekwa maji safi kisha mwanasayansi bingwa wa mambo ya wanawake aliweka dawa kwenye chungu cha katikati.
Baada ya mwanasayansi kuweka dawa kwenye chungu cha katikati, alitembea akiwazunguka wanawake hao huku akiongea maneno ya kisayansi ya kabila la Kihehe.
Akiwa anatembea kuwazunguka wanawake hao huku akitamka maneno ya Sayansi ya Kihehe, chungu chenye maji alichosimama mwanamke aliyechupuka, maji yake yalibadilika na kuwa na rangi nyekundu kama damu, kisha maji hayo yalitoa mapovu. Baada ya matokeo hayo kazi ya vipimo inakuwa imekamilika.
Kwa mujibu wa taratibu za Kabila la Wahehe wakati huo, mwanamke aliyepimwa na kubainika kuchepuka nje ya ndoa yake alikuwa akipewa adhabu ya kukatwa masikio yake yote mawili.
Adhabu hiyo iliwekwa ili kumtambulisha mwanamke huyo kwa jamii kuwa siyo mwaminifu kwenye ndoa yake na pili kama fundisho kwa wanawake wengine wasithubutu kuchepuka nje ya ndoa zao.
Kati ya wake 62 wa Chifu Mkwawa, aliyebainika kuchepuka baada ya kupimwa na kipimo vya Lifugo alikuwa mke wa tisa ambaye jina lake ni Sechalamila. Mama huyo aliadhibiwa adhabu ya kukatwa masikio yake yote mawili na adhabu hiyo ilitekelezwa na Chifu Mkwawa mwenyewe.

UTULI NA MTWANGO
Utuli na Mtwango (pichani hapo juu) ni kinu na mchi ambavyo vilitumika kutengeneza dawa za Chifu Mkwawa na vilitengezwa kwa mti wa mpingo. Mbali na kutumika kwa ajili ya ketengeneza dawa za Chifu Mkwawa, Utuli na Mtwango vilitumika pia kuponda nafaka kwa ajili ya chakula cha Chifu Mkwawa.

VINYANTILO
Vinyantilo (pichani hapo juu) ni vyungu vilivyotumika kuhifadhi maziwa, asali na maji.

LUHEMELO
Chungu Luhemelo (pichani hapo juu) kilitumika kama Dira. Kilitumika kujua pande nne za dunia ambazo ni Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini na pia kilikuwa mahususi kwa ajili ya kutambua eneo walipo maadui.
Luhemelo vilikuwa vyungu vitano vidogo vilivyounganishwa sehemu moja. Ili vifanye kazi, chungu cha katikati kiliwekewa dawa, halafu viwili vya upande mmoja vilifunikwa juu na viwili vilivyosalia viliachwa wazi.
Ili kujua sehemu walipo maadui, mwanasayansi wa Sayansi za Kiafrika alipaswa kusema maneno ya kisayansi akiwa amesimama mbele ya vyungu hivyo na akiwa anasema maneno hayo, chungu kilicho mwelekeo wa upande walipo maadui kilifuka moshi.
Baada ya matokeo hayo, Chifu Mkwawa na majeshi yake walijipanga kwa ajili ya mapambano na mara nyingi walishinda vita kwa sababu Dira Luhemelo iliwasaidia kutambua eneo walipo maadui hivyo walikwenda kukabiliana nao wakiwa hawajafika kwenye himaya yao.