
ILI kumjua Chifu Mtwa Mkwava Mkwavinyika Mnyigumba Mwamuyinga Kilonge wa Himaya ya Wahehe, unapaswa kutembelea Makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa iliyopo Kalenga, Iringa.
Anafahamika zaidi kwa jina la Chifu Mkwawa. Chifu aliyekuwa na misuli yenye nguvu na akili nyingi. Alikuwa na mbinu nyingi bora za kivita zilizomuwezesha kuangamiza mamia ya wanajeshi wa Kijerumani na pia alikuwa mfanyabiashara hodari.
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambalo linasimamia Makumbusho ya Chifu Mkwawa limerahisisha ufikaji kwenye makumbuko hiyo na limeitunza vema historia yake ambayo ni simulizi ya kuvutia kwa mtalii anayefika mahali hapo na darasa tosha la historia kwa wanafunzi wa Tanzania, Afrika na duniani nzima.
Dunia inamtambua Chifu Mkwawa kama kiongozi wa Kabila la Wahehe lililopo Tanzania. Kamanda wa Jeshi la Lipuli mwenye mbinu nyingi za kivita katika uwanja wa mapambano; na hilo linathibitishwa na uamuzi wa wakoloni wa Kijerumani kuchukua kichwa chake na kukipelekea Ujerumani kwa ajili ya kuchunguza ubongo wake baada ya kujiua yeye mwenyewe.
Chifu Mkwawa alizaliwa mwaka 1855; akaishi maisha yenye mafanikio makubwa kwa muda miaka 43, kisha akajiua yeye mwenyewe mwaka 1898 akiwa msituni katika Kijiji cha Mlambalasi kwa sababu hakuwa tayari kutekwa na majeshi ya kikoloni ya Wajerumani.
Chifu Mkwawa ndiye anayeshikilia historia ya Kabila la Wahehe. Hiyo ni kwa mujibu wa historia iliyo kwenye makumbusho yake eneo la Kalenga alikoishi enzi za uhai wake.
Maana ya neno Kalenga ni eneo lenye maji mengi. Awali kabla ya ujio wa wakoloni, wenyeji wa eneo hilo, Wahehe waliliita Kwilenga lakini wakoloni walishindwa kulitamka, wakawa wanatamka Kalenga na kuanzia hapo neno Kwilenga lilifutika na badala yake Kalenga ndiyo likawa linatumika.
Jina la kwanza Chifu Mkwawa, Mtwa; maana yake ni kiongozi wa Kabila la Wahehe na Mkwawa maana yake ni mtekaji au mpokonyaji. Ili kuyajua yote haya kwa undani ni muhimu kutembelea Makumbusho ya Chifu Mkwawa huko Kalenga, Iringa.
Akiwa Chifu wa Kabila la Wahehe, Chifu Mkwawa alijenge kambi ya jeshi lake eneo la Kalenga mahali alipokuwa akiishi. Kambi hiyo aliiita Lipuli.
Kambi ya Lipuli ambayo ipo ndani ya eneo la Makumbusho ya Chifu Mkwawa ilijengwa kwa muda wa miaka minne, kuanzia mwaka 1887 hadi 1891.

Masalia ya mawe yaliyojenga ukuta wa kambi la Lipuli yanayoonekana kwenye majani.
Ukuta wa Kambi ya Lipuli ulikuwa na urefu wa futi 12, upana wa ukuta ulikuwa mita 3 na ukubwa wa ndani ya ngome ulikuwa kilomita 16.
Chifu Mkwawa alipigana vita na himaya za machifu wa Morogoro, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Dodoma na Singida na kuzishinda.

Masalia ya Mlima wa udongo uliochotwa na Chifu Mkwawa kutoka himaya mbalimbali za kichifu alizopigana nazo na kuzishinda kisha kuchota udongo wa ardhi yake kwenda kuuweka kwenye ngome yake ya kijeshi ya Lipuli.
Alikuwa na utaratibu wa kipekee. Utaratibu wake huo ulikuwa akipigana vita na kushida alichukua udongo wa himaya aliyoipiga na kwenda kuurundika kwenye sehemu maalumu ndani ya ngome yake ya kijeshi ya Lipuli.
Chifu Mkwawa alishinda vita dhidi ya himaya za machifu wengi hivyo eneo alilokuwa akirundika udongo wa himaya alizozipiga, lilijitengeneza kilima cha udongo na mahali hapo alipafanya kuwa sehemu yake ya kuhutubia watu wake.
Kilima hicho cha udongo kiliitwa Liringa. Maana na neno Liringa kwa Kihehe ni kuringa au kutamba.
Historia iliyo ndani ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa inaonyesha kuwa alikuwa chifu mwenye maringo na hasa alipokuwa akitoka vitani na ushindi. Kwamba kila alipokuwa akirejea kutoka vitani na ushindi, alikuwa akipanda kwenye kilima hicho cha udongo kwa madaha na kutoa hotuba akiwatambia machifu wenzake aliowashinda vitani kisha kuwafanya mateka wake.
Udongo wa baadhi ya maeneo ya Tanzania ambayo Chifu Mkwawa aliuchukua baada ya kuyapiga majeshi ya machifu wenzake ni wa himaya za kichifu za Morogoro, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Dodoma na Singida.
Kwa sababu ya kushinda vita nyingi, Chifu Mkwawa alikuwa mtawala wa eneo lenye ardhi kubwa hivyo alitambulika kama chifu tajiri kwa sababu wakati huo, utajiri ulikuwa ukipimwa kwa ukubwa wa ardhi unayoimiliki.
Chifu Mkwawa, pia alikuwa mfanyabiashara mahiri. Alifanya biashara na Waarabu na alijenga nao urafiki. Biashara aliyokuwa akiifanya ni ya kubadilishana bidhaa.
Alifahamika kama mtawala mjanja sana na mwepesi sana wa kujifunza. Wakati akifanya biashara na waarabu alijifunza kusoma na kuandika kiarabu kwa muda mfupi; akaweza kuzungumza, kusoma na kuandika kiarabu.
ILI KUJUA MENGI KUHUSU CHIFU MTWA MKWAVA MKWAVINYIKA MNYIGUMBA MWAMUYINGA KILONGE WA IRINGA, TEMBELEA MAKUMBUSHO YA CHIFU MTWA MKWAWA ILIYOPO KALENGA IRINGA.