Friday, March 14, 2025
spot_img

VIGOGO TANESCO ‘WALIMWA’ WARAKA

RIPOTA PANORAMA

VIONGOZI waandamizi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) wameandikiwa waraka wenye maelekezo 11 wanayotakiwa kuyasimamia katika maeneo yao ya kazi.

Waraka huo ambao Tanzania PANORAMA Blog imeuona ukiwa na kumbukumbu namba UB. 161/541/10/10; umeandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga, (pichani hapo juu) Februari 3, 2025 kwenda kwa Naibu Mkurugenzi Usambazaji Umeme, wakurugenzi wa kanda, mameneja wa mikoa, mameneja wa wilaya na maafisa huduma kwa wateja.

Mhandisi Nyamo – Hanga ameandika kuwaelekeza vigogo hao kuwa, wao kama wasimamizi wa wafanyakazi wa shirika hilo kwenye maeneo yao wahakikishe maelekezo yake ya kuboresha utoaji huduma kwa wateja yanawafikia na wanazingatia kufanya kazi kwa weledi na kufuata utaratibu wanapotekeleza majukumu yao.

Katika waraka huo, Mhandisi Nyamo – Hanga ameelekeza kuwa hairuhusiwi kwa namna yoyote kufunga tiketi kabla mteja hajapatiwa huduma stahiki na tiketi zinazoruhusiwa kuunganishwa ni zenye taarifa au matatizo yanayofanana na kwamba zisifutwe mpaka huduma inaporejea na iwapo tatizo litachukua muda mrefu, wateja wajulishwe mapema ili wasiendelee kupiga simu kuuliza.

Mhandisi Nyamo – Hanga ameelekeza pia kuwa tiketi ambazo taarifa na au matatizo yake hayafanani, haziruhusiwi kuunganishwa bali kila mteja ahudumiwe kulingana na tatizo alilolitolea taarifa.

“Tiketi zinazotakiwa/zinazopaswa kwenda idara nyingine (reffal tickets) zifanyike kwa usahihi na zisifungwe mpaka mteja akapohudumiwa na baada ya kumuhudumia, fundi ajaze tatizo alilolikuta (problem found) na aandike kwa usahihi utatuzi alioufanya kutatua changamoto ya mteja,” yanasomeka maagizo namba nne na tano katika waraka wa Mhandisi Nyamo-Hanga.

Pia mteja kufungiwa mita katika eneo lake kabla ya kujaza mfumo wa ‘nikonekt’, na baada ya kufungiwa mita mpya au kubadilishiwa asajiliwe siku hiyo hiyo kuepusha usumbufu wa kukosa huduma na maafisa huduma kujulisha wateja sababu za kuchelewa kuunganishiwa huduma ili kupunguza upigaji simu wa wateja ambao maombi yao yanashikiliwa kwenye mfumo wa ‘nikonekt’ bila taarifa.

Maagizo mengine ya Mhandisi Nyamo – Hanga kwa maafisa hao ni kutoa taarifa kwa wateja ya kukatika umeme mara kwa mara, maafisa uhusiano na huduma kwa wateja wa mikoa kushirikiana na kurugenzi ya mawasiliano kuratibu mikutano baina ya shirika na wananchi ili kuwafahamisha mikakati inayotekelezwa kuwahudumia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dkt. Dotto Biteko akikagua utendaji kazi wa kituo cha miito kwa simu cha Tanesco hivi karibuni.

Mwisho Mhandisi Nyamo – Hanga anaagiza kurugenzi ya Tehema ya Tanesco kushughulika na changamoto za kimifumo za mara kwa mara katika kituo cha miito ya simu na anaonya kuwa watendaji watakaobainika kufanya udanganyifu wanapowahudumia wateja watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Haya yanajiri wakati kituo cha miito ya simu cha Tanesco kikiandamwa na madai ya ufisadi mkubwa wa fedha za shirika hilo, madai ambayo Mhandisi Nyamo – Hanga licha ya kuulizwa ukweli wake ameshindwa kuyatolea majibu kwa takribani wiki moja sasa.

Tanzania PANORAMA Blog itaanza kuripoti kwa kina skandali inayokikabili kituo cha miito ya simu cha Tanesco, wiki ijayo.

    

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya