TERESIA MHAGAMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko ameziagiza taasisi zilizo chini ya wizara yake kuupa kipaumbele mpango mahususi wa nishati.
Agizo hilo alilitoa alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha tatu cha tathimini ya utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha miezi mitatu, Oktoba hadi Disemba 2024, kilichofanyika hivi karibuni.
Dkt. Biteko alisema mpango huo uliosainiwa wakati wa mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika uliofanyika nchini mwezi uliopita, pamoja na mambo mengine unalenga kusambaza umeme kwa watanzania milioni 8.3 ifikapo 2030.
“Kila mmoja kwa nafasi yake ajipange atatekeleza vipi hii energy compact. Fedha hizi mlizosikia zimetolewa na wadau wa maendeleo kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika zinahusu Bara lote la Afrika.
“Hazitakuja Tanzania pekee hivyo lazima tujipange jinsi ya kuzipata ili kutekeleza miradi tuliyopanga kuifanya,” alisema.
Aidha, Dkt. Biteko ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusambaza nishati safi ya kupikia vijijini sambamba na kufanya tathmini ya idadi ya watu wanaohama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi.

Alisema REA ihakikishe ifikapo 2030, asilimia 75 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Katika kikao hicho, taasisi zilizotekeleza majukumu yake ipasavyo zilipewa zawadi. Taasisi hizo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Kikao cha tatu cha tathmini ya utendaji kazi wa wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kilizikutanisha Tanesco, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), EWURA, PURA, REA, Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC).