TERESEA MHAGAMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga kumchukulia hatua mtumishi wa shirika hilo aliyemfokea mteja.
Amesema iwapo Mhandisi Nyamo – Hanga hatatekeleza agizo hilo, yeye mwenyewe atachukua hatua kwa mtumishi huyo.
Agizo hilo amelitoa hivi karibuni kwenye kikao cha tatu cha tathmini ya utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha miezi mitatu, Oktoba hadi Disemba 2024.
Dkt. Biteko ameanzisha utaratibu wa kufanya vikao vya tathmini ya utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kujipima na kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo.
Alisema haridhishwi na mwenendo wa kituo cha huduma kwa wateja cha Tanesco ambacho kinalalamikiwa na wateja.
“Pamoja na kazi nzuri mnazozifanya lakini eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni utoaji wa huduma kwa wateja. Juzi nilitembelea kituo hiki nikawaambia sifurahishwi na utendaji kazi wa kituo.
“Mimi nafahamu changamoto za kituo hiki si kwa kuota bali wananchi wananipa mrejesho pamoja na viongozi wanaonisimamia. Hivi tumefanya kazi yote
hii ya kuwa na umeme wa ziada, tunajenga laini za umeme lakini mtu mmoja ambaye kazi yake ni kumsikiliza mteja na kumpa majibu sahihi anatupainti wote vibaya tunaonekana hatufai.
“Majibu yapo lakini wataalamu wanageuka kuwa wababe kwa wateja, hii haikubaliki,” alisema Dkt. Biteko.
Alilitaja lalamiko la mwananchi aliyepiga simu Tanesco kisha akapewa tiketi namba ya lalamiko lakini baada ya muda ilifutwa kwa madai kwamba lalamiko husika limeshashughulikiwa wakati halijashughulikiwa.
Alisema mteja huyo alipouliza kwanini lalamiko lake lake limefutwa alifokewa na mtumishi wa Tanesco.