MCHOKONOZI
MSALABA wa mema na mabaya katika Taifa letu kwa sasa upo mabegani mwa Raisi Samia Suluhu Hassan bila kujali mema na mabaya hayo yalipandikizwa lini, yakamea na kustawi lini hadi sasa yamekomaa.
Taifa letu liko kwenye taharuki. Ni taharuki ya utekaji, utesaji na mauaji ya raia. Katikati ya taharuki hiyo, vyombo vya ulinzi na usalama hususan polisi, vinatajwa kuhusika.
Raisi Samia ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, mzigo wa tuhuma na lawama dhidi ya vyombo hivi upo mabegani kwake. Hata hivyo, Raisi Samia anapoubeba mzigo huu, watanzania hatuna budi kujiuliza ni wapi tulipokosea hadi kufika hapa tulipo sasa.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba watanzania wengi tuna tabia ya usahaulifu; na binafsi ninaamini watanzania wengi siyo wapole wala wavumilivu bali wana tatizo la malezi na ukosefu wa lishe bora inayojenga utimamu wa ubongo tangu mtu akiwa mtoto mdogo.
Mwandishi Manyerere Jackton amepata kusema kuwa mtoto ambaye hapati lishe bora utotoni, akili yake haiwezi kuwa na akili akiwa mtu mzima.
Kama Taifa, tupo katika mtanziko wa uhuru wa kuishi. Nashawishika kuamini kuwa mtanziko huu chanzo chake ni polisi kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao na hapo hapo malezi mabaya na lishe duni vikionekana dhahiri kuwa kichocheo cha hali hiyo.
Tumezingatia kujaza matumbo ya watoto wetu vyakula vinavyodumaza ubongo, vyakula vilivyosindikwa na tumewapa uhuru wa kujifunza ujambazi, ukatili, muaji, kukata viuno na kila baya badala ya kuzingatia maadili mema.
Matokeo yake ndiyo haya. Tumeumba jamii ya watu wasiokuwa na utu, adabu, wanaowaza kuishi maisha ya kwenye sinema za kuuana, kupigana na kupata pesa kwa njia yoyote ile.
Dawa ya kutibu tatizo; kwanza ni kulitambua na kulikubali kwamba ni tatizo, halafu unalishughulikia kwa njia sahihi na mwisho unaangalia tatizo lililo kwa mwenzako unamsaidia kulitatua ili nyote muwe salama.
Malezi mabovu na liche duni utotoni vimetufanya tuwe watu wa ajabu bila kujua kuwa sisi ni wa ajabu. Kudhihirisha hili, angalia lishe ya watoto wetu kuanzia mkate wa siagi ya kudunduliza hadi chips yai badala ya chai na mihoga hadi ugali na mboga za majini. Lishe duni imetupatia chawa wengi sana katika Taifa letu.
Walimu wetu wenye jukumu la malezi na kuwasomesha wanetu, wanapotualika kwenye mahafali ya kuhitimu kwao wanawapandisha majukwaani watuonyeshe jinsi walivyowafundisha kukata viuno midundo ya muziki wa akina Diamond na Zuchu badala ya umahiri wa stadi za kazi na uwezo walioupata kitaaluma. Ni makosa makubwa.
Kikombe cha babu wa Loliondo
Angalia maelfu kwa maelfu ya watanzania wanavyomiminika kununua udongo, maji na mafuta kwa wachungaji wakiaminishwa kuwa yatawatakasa au kuwafikisha mbinguni badala ya kwenda kwenye nyumba za ibada kuomba toba.
Angalia watanzania wanaoamka asubuhi kuwahi sunagogi, wakashinda huko wakiomba Mungu awashushie pesa na utajiri badala ya kwenda kufanya kazi.
Mtu mzima aliyepata lishe bora na malezi mazuri tangu utotoni hawezi kufikiria wala kukimbilia Loliondo kwenda kunywa maji ya kikombe cha babu ili kupona maradhi yanayomsibu badala ya kwenda hospitali.
Kijana wa kike au wa kiume aliyelelewa vema na kula lishe bora utotoni hawezi kushinda akicheza kamari badala ya kusoma au kufanya kazi na wanaume na wanawake wanaotumia muda wao mwingi kushabikia mchezo wa soka na dansi za utupu badala ya kuutumia muda huo kupanga mipango ya maisha yao, lazima kuna mahali hawako sawa.
Tena; mtoto anayetoka shule akafika nyumbani kuangalia televisheni akisubiri apikiwe ubwabwa na dada wa kazi, ale ashibe kisha arudi kuweka miguu juu ya kochi kuangalia televisheni huku baba na mama yake wakimuangalia bila kumwambia atoe vyombo mezani akaoshe, hawezi kuwa na akili ya kujitegemea bali atawaza anasa, spider man, mapigano, kuuana na kupata pesa ya chap chap kama anavyoona magenge ya wahalifu wanavyopata fedha kihalifu kwenye sinema.
Haya ndiyo makosa makubwa yaliyotufikisha hapa tulipo sasa. Malezi mabaya na ukosefu wa lishe bora ndiyo kiini cha tatizo linalotukabili kama Taifa. Ukatili, roho mbaya, unafiki, tamaa, umbea na mengine mengi ya hovyo yaliyojengwa vichwani mwa watanzania, kiini chake ni hiki.
Vijana watuhumiwa wa kundi la panya road
Tumezalisha kizazi cha panya road, vijana katili waotembea na mapanga, visu, nyundo, nondo, nyembe, misumali na midenge kwa ajili ya kuwashambulia wazazi, kaka na dada zao ili wawapore pesa.
Wapo wazazi wanaofurahia ukatili wa matendo ya panya road na wanapokea pesa zinazonuka damu wanazopelekewa. Polisi wanapowasaka nyumba kwa nyumba kuwadhibiti, wanawaficha au wanawatorosha wasikamatwe.
Wazazi tunaficha na kutorosha wezi, vibaka, wauaji ambao ni watoto wetu. Taifa la leo tulilolijenga ndiyo hili. Hapa ndipo tulipokosea. Tunatafunwa na makosa yetu wenyewe. Busara ituongoze kujitazama ndani ya nafsi zetu, tukubali tumekosea. Tujisahihishe, kisha tusonge mbele.
Sitaki kurejea matendo mabaya ya kutishana kwa silaha za moto, kuumizana na hata kuuana tunayofanyiana raia kwa sababu ni mengi mno. Lakini ili kulipa uzito andiko langu nataja tukio la mwanamume aliyemjeruhi kwa bastola mwanamume mwenzake wakati wakigombania mwanamke kwenye klabu ya usiku jijini Dar es Salaam.
Nataja pia tukio lililotokea Mkoa wa Kagera ambako baba alishiriki kumchinja mwanaye kwa sababu ya tamaa ya pesa. Alitajwa Padre pia katika tukio hilo. Haya na mengine mengi ya kikatili ni kielelezo cha ukatili tulionao watanzania. Ni kielelezo cha aina ya kizazi chetu cha sasa.
Ni vizuri kuitazamana kwa macho matatu historia iliyotufikisha hapa na ili kuitendea haki ni wajibu kuiandika kwa kuweka rejea ili inakapokuwa ikihukumu; kwa sababu historia ina tabia ya kuhukumu kwa wakati inaoona unafaa, wakati ukifika ihukumu kwa haki.
Kinachoendelea sasa nchini ni matunda ya tulichokipanda. Polisi kuwa mabubu kutoa taarifa za uhalifu mkubwa walioahidi kuuchunguza na au ambao wana wajibu wa kuuchunguza na kuutolea taarifa hawajaanza leo, ni tabia yao kwa muda mrefu.
Tangu alipouawa mwandishi wa habari Stan Katabaro hadi leo sijapata kusoma mahali popote ripoti ya uchunguzi wa kifo chake. Kama ipo naomba niisome, nitafuta andiko langu hili.
Katabaro alikufa mwaka 1993, alikutwa tu amekufa. Akiandikia gazeti la Mfanyakazi aliripoti habari ya uchunguzi kuhusu serikali ya wakati huo kutoa Pori la Akiba la Loliondo kwa kampuni moja kutoka uarabuni. Kwa sababu ya ukimya wa polisi wengi wanaamini hicho ndicho kilichosababisha kifo chake.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka akiwa hospitalini kwa matibabu baada ya kutekwa na kusulubiwa kiasi cha kufa.
Utekaji, utesaji na uuaji watu upo miaka mingi lakini tunaweza kuuelezea kwa rejea nzuri zaidi kuanzia kwenye urais wa Jakaya Kikwete.
Wakati wa utawala wa Kikwete, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, yeye na wenzake wakiwa katika msuguano na Serikali alitekwa, akasulubiwa kiasi cha kufa, akaenda kutupwa katika msitu wa mabwepande. Ya Mungu mengi, Dk. Ulimboka hakufa lakini simulizi ya tukio lake hilo ni ya kusikitisha.
Baadhi ya vyombo vya habari huru viliandika tukio hilo huku vikiwataja kwa majina waliohusika. Waliotajwa ni watumishi wa taasisi za ulinzi na usalama.
Serikali ya Kikwete iliahidi kuchunguza tukio hilo, tume za kuchunguzi zikaundwa ikiwa ni pamoja na polisi lakini mpaka leo matokeo ya uchunguzi wa tume hizo hayajapata kutolewa. Polisi wapo kimya.
Si jambo jema kutonesha vidonda lakini nadhani na kwa sababu nadhani kudhani si kosa, kuirejea historia inayoumiza ili kuponya majeraha ni busara zaidi.
Raisi Mstaafu Jakaya Kikwete akimjulia hali aliyekuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Absalom Kibanda alipokuwa akitibiwa Afrika Kusini baada ya kushambuliwa na kuumizwa vibaya na wasiojulikana.
Wakati wa utawala wa Kikwete, aliyekuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Absalom Kibanda alivamiwa, naye akasulubiwa kiasi cha kufa, akatupwa nje ya nyumba yake.
Tukio lake lilitikisa Taifa kwa sababu Kibanda alifahamika kwa misimamo yake isiyoyumba katika mambo ya msingi ya kitaifa na alikuwa na uthubutu wa kuandika akikosoa na kuonya viongozi waliopewa dhamana za juu za uongozi wa Taifa letu kwenye mambo waliyokengeuka.
Ziliundwa tume za kuchunguza tukio hilo. Polisi walikwenda mpaka Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu lakini ripoti ya uchunguzi wao mpaka leo haijapata kutolewa. Labda walishindwa kuchunguza au labda uchunguzi huo unachukua muda kiasi. Ukweli ni kwamba mpaka leo polisi hawajatoa taarifa ya uchunguzi huo.
Wakati wa utawala wa Hayati John Pombe Magufuli, matukio ya utekaji, mauaji na utawala wa mabavu uliokuwa ukitekelezwa na baadhi ya wasaidizi wake yaliongezeka sana.
Ben Saanane
Ni wakati huo ndipo alipopotea Ben Saanane, ni wakati wa utawala wa Magufuli, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi, tena muda wa mchana akiwa katika maeneo wanayoishi viongozi wa kitaifa ambayo yana ulinzi wa vyombo vya dola.
Eneo alilotekwa Mohamedi Dewji
Na kipindi cha utawala wa Magufuli , mfanyabiashara Mohamedi Dewji alitekwa kwa siku kadhaa kabla ya kuachiwa na kurejea uraiani. Dewji ni mfanyabiashara anayetambulika kimataifa na pia raia wa Tanzania. Yupo mtaani lakini yeye mwenyewe hajapata kuzungumzia kwa undani tukio hilo na wala polisi hawajapata kutoa taarifa ya uchunguzi wao kuhusu nani alimteka na kwanini.
Mohamedi Dewji
Hadi leo ripoti ya uchunguzi ya shambulio la Lissu na kupotezwa kwa Saanane na wengine wengi waliopotea kipindi cha Magufuli hazijapata kutolewa na polisi. Wapo kimya.
Baadhi ya wasaidizi wa Magufuli waligeuka miungu watu wakivamia hata ofisi za vyombo vya habari wakiwa na wanausalama wenye silaha nzito nzito.
Matukio ya aina hii ndiyo yamejenga taswira kuwa baadhi ya wanausalama wanatumika vibaya na waliopewa dhamana za uongozi kunyanyasa, kuumiza na au kuua raia.
Na tukumbuke aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati wa urais wa Magufuli, Nape Nnauye alipojaribu kufurukuta, kwanza Magufuli alimfuta kazi kisha akapata kashikashi ya hao hao wanaodaiwa wanausalama, bila woga walimtishia kwa bastola mbele ya kadamnasi ya watu. Video mitandaoni zilimuonyesha aliyetishia. Sijui kama polisi walijihangaisha walau kumuhoji tu.
Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Katika kipindi tulicho nacho sasa cha uraisi wa Samia, utekaji, utesaji na mauaji ya raia vinaendelea kwa sababu ilishakuwa kama desturi. Tangu wakati wa utalawa wa Kikwete, akaja Magufuli kutekwa, kuteswa na kupotezwa raia imekuwa kawaida.
Sina sababu ya kuyarejea hapa matukio ya hivi karibuni kwani bado mabichi mno. Watu bado wana vidonda vibichi mioyoni mwao. Lakini tukubali kwamba matendo haya mabaya tumeishi nayo kwa miaka mingi na hakuna hatua za makusudi za kuyakomesha.
Tukiwa katikati ya hali hii tete tuliyoishi nayo kwa miaka mingi inatupasa kutambua kuwa jamii iliyojijengea utaratibu wa maisha yake kwa kipindi kirefu, kubadilisha utaratibu huo ndani ya mfupi ni jambo gumu.
Utamaduni wa kutekana, kutesana na kuuana ulianza kuchomoza tangu enzi za utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili lakini haukutafutiwa ufumbuzi, ulistawi vizuri tu wakati wa Kikwete na baadaye Magufuli na sasa wakati wa Samia umekomaa. Inahitaji uamuzi mgumu kuukomesha.
Tunapopaza sauti sasa tukitaka kukomeshwa kwa maovu haya, tutambue kuwa kiongozi aliyedhamiria kupambana na uovu huu lakini watu wake hawamuheshimu. Amewapa uhuru wa kusema walioukosa kwa miaka mingi lakini baada ya kuupata wanautumia uhuru huo kumtukana mitandaoni, anaweza kuvunjika moyo na kujutia maamuzi yake mema.
Pamoja na makosa yetu ya malezi mabaya na lishe duni, tukubali kuwa sisi wenyewe na watoto wetu tunafantya makosa makubwa huko mitandaoni kutukana na kudhalilisha viongozi wetu. Tunautumia vibaya uhuru wa kujieleza tulionao sasa ambao tulioukosa kwa zaidi ya miaka mitano. Tukubali kuwa tunakosea na tujisahihishe.
Polisi wenye tabia za kuumiza wenzao ni watoto wetu. Matendo yao haya yanatokana na sisi na pengine mafunzo yao ya upolisi.
Tulirithi mfumo wa Jeshi la Polisi la kikoloni ambalo kazi yake mahususi ilikuwa kulinda watawala badala ya raia na mali zao. Tuachane na mfumo huo sasa, polisi wetu wafundishwe kuwa watumishi wa raia.
Niwakumbushe simulizi ya Rais Samia kuhusu vituko vya polisi kuwa hata yeye walipata kumuhenyesha walipomdaka taa moja ya gari yake ikiwa haiwaki.
Alikuwa akitoka harusini usiku, wakamkamata taa ya gari lake haiwaki, akawasihi wamuachie atatengeneza asubuhi kwa sababu alikuwa hajui kama haiwaki; kwani walimsikiliza? Walimuhenya mpaka walipojua ni Samia, wakagwaya, wakamuachia.
Vyovyote iwavyo Jeshi la Polisi limechafuka na ili kulisafisha ni muhimu kulivunja na kuliunda upya likiwa jeshi la kuwatumikia raia.
Ni muhimu kulivunja sasa kwa sababu imani ya raia kwa jeshi hilo imepungua sana na hasa baada ya tukio lililoshindikana la kumnyakua Wakili Alphonce Lusako hivi karibuni.
Aliyekuwa akimkimbiza kumkamata anadaiwa kuwa ni polisi na ametambuliwa kwa jina. Picha za video zimesambaa, kukanusha kwamba aliyekuwa akitafutwa ni mtu mwingine ni sawa na kituko. Labda polisi wakanushe kuwa aliyekuwa akimkimbiza Wakili Lusako siyo polisi.
Sisemi Jeshi la Polisi livunjwe kwa nia mbaya au kuwakomoa. Hapana, kinachopaswa kufanywa ni kufumua muundo, utekelezaji wa majukumu yao na kuboresha mitaala ya kozi za upolisi kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye elimu na kwingineko.
Tunapotamani haya kutokea, tutambue kuwa kupambana na polisi kwa kutweza utu wao mitandaoni hakuna afya yoyote kwetu kama jamii ya watanzania wastaarabu na wala hakutawabadili bali kutazidi kuchochea hasira zao. Tujiepusha na aibu hii ya kuchafuana mitandaoni tukitambua msingi wa tatizo lililotufikisha hapa.
Niwaume sikio kuwa mimi pia ni muhanga wa ukatili wa polisi. Kuteswa, kunyimwa dhamana, kwenda kusachiwa nyumbani kama jambazi na polisi wasiokuwa na sare waliobeba bunduki nzito nzito na kunyang’anywa vifaa vya kazi kwa tuhuma za kuandika habari za kweli, zenye kila uthibitisho ambao polisi wanao. Vidonda vya ukatili wa polisi ninavyo moyoni.
Nikiwa nasubiri utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya haki jinai nimeamua kumwandikia Mwenyezi Mungu barua ya wazi yenye maombi maalumu badala ya kuaibishana mitandaoni.
Mungu hafichwi kitu hivyo katika barua hiyo nitawataja kwa majina polisi wa Kituo Kikuu cha Dar es Salaam walionikamata na walichonifanyia, nitawataja kwa majina Polisi wa Kituo cha Bandari walichonifanyia nami nikawadokeza Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURI) kuhusu polisi hao na pia nitawataja kwa majina maafisa wa TAKUKURU wa Makao Makuu Dodoma na Dar es Salaam niliowadokeza na kuwaonyesha kilichofanywa na Polisi wa Bandari.
Nitaandika kwa furaha kumsihi Mwenyezi Mungu aliyewatoa kwetu, awatwae kwake polisi wote walionitesa na kutweza utu wangu, akakae nao huko kwake kwa amani.