RIPOTA MAALUMU
WANASAYANSI duniani wamegundua wanyamapori wa ajabu kwenye Bonde la Kongo.
Pia wamegundua aina mbalimbali za mimea zilizostawi kwenye bonde hilo katika kipindi cha miaka 10 waliyofanya utafiti kwenye eneo hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) iliyotolewa Disemba 3, 2024, zaidi ya wanyamapori wa ajabu na mimea 700 vimegunduliwa na wanasayansi hao kwenye Bonde la Kongo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ugunduzi huo unahusisha ndege aina ya Bundi wa ajabu anayetoa mlio unaofanana na sauti ya paka.
Bundi huyo aligunduliwa mwaka 2022 na kupewa jina la Otus Bikegila au bundi wa principle na kwamba masikio yake yana muundo wa tawi la mti.
Ripoti hiyo inataja kugunduliwa kwa nyoka wa kutisha, mwenye sumu kali, mjanja na ambaye hubadilika rangi kulingana na mazingira anayekuwepo. Nyoka huyu amepewa jina la Mongo au Atheris Mongoensis.
Atheris Mongoensis.
“Nyoka huyu aligunduliwa mwaka 2020 na mbali na kuwa ana sumu kali pia ana nywele. Ana uwezo wa kujibadilisha rangi na kuwa kijani, njano na nyeusi anapokuwa kwenye mawindo ya kutafuta chakula, hali inayomruhusu kutogundulika kirahisi akiwa msituni.
Ripoti inamtaja pia chura mwenye uwezo wa kutoa ishara ambaye amepewa jina la Chura wa Kongo au Congolius Robustus.
Chura huyu anapatikana kwenye maeneo kadhaa kusini mwa Mto Kongo ulioko Bonde la Kongo na ana urefu wa chini ya sentimita nne.
Congolius Robustus, chura mwenye uwezo wa kutoa ishara.
Ripoti inataja pia kugunduliwa kwa mbuni na mamba mwenye umbo dogo pamoja na mimea ya aina mbalimbali.
Bonde la Kongo ambalo linajulikana kama lungs of Africa au mapafu ya Afrika ni msitu wa pili kwa ukubwa duniani na unaopata mvua nyingi kwa mwaka ukitanguliwa na msitu wa Amazon.
Bonde la Kongo lina mfumo wa ikolojia unaofyonza hewa ya ukaa kiliko inayotolewa lakini inaelezwa kuwa watu wengi duniani hawajui umuhimu wake.
Mkuu wa Uhifadhi wa Bonde la Kongo, Jaap Van der Waarde amekaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingerexa (BBC) akieleza kuwa mbali na kuwa na viumbe hai wengi wa kipekee duniani, bonde hilo ndilo pekee duniani kwa sasa ambalo lina mvua nyingi katika kipindi chote cha mwaka na linalofyonza kwa wingi hewa ya kaboni kuliko inayotolewa.
Kwamba Bonde la Kongo limeupiku Msitu wa Amazon ambao ulikuwa ukiongoza duniani kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kufyonza hewa ya kaboni lakini hivi sasa uwezo huo umepungua.
Mwezi uliopita, WWF ilitoa ripoti iliyoeleza kuwa utafiti uliofanywa na mamia ya wanasayansi kutoka sehemu mbalimbali duniani na wale wa shirika hilo, uligundua kuwa idadi ya wanyamapori duniani imepungua kwa asilimia 73.
Wanasayansi hao sasa wanatafiti uwepo wa bioanua za ajabu katika Bonde la Kongo na mahitaji ya haraka ya uhifadhi wa maisha ya viumbe hai hao katika eneo hilo.