RIPOTA PANORAMA
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba imetoa hukumu kuwa, kufanya mapenzi na mwanafunzi siyo kosa kisheria.
Hukumu hiyo ilitolewa mahakamani hapo Oktoba 28, 2024 na Jaji Gabriel Malata baada ya kusikiliza hoja za Wakili Mwandamizi Msomi wa Serikali, aliyekuwa akiwakilisha upande wa Jamhuri, Alice Mutungi aliyeeleza kuwa kisheria hakuna kosa la kufanya mapenzi na mwanafunzi.
Kesi hiyo ya jinai namba 27046 ya mwaka 2024, mshtakiwa alikuwa Thadeo Pastory na mlalamikaji alikuwa Jamhuri ambayo wakili wake, Mutungi aliiambia mahakama kuwa kufanya mapenzi na mwanafunzi si kosa kisheria hivyo mahakama ikatoa uamuzi wa kumuachia huru mshtakiwa.
Jaji Malata ambaye alikuwa akisikiliza rufaa iliyokatwa na Pastory kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera ambayo ilisikiliza kwanza kesi hiyo na kumkuta mshtakiwa hana hatia ya kosa la kubaka lakini ikamfunga kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kosa la kufanya mapenzi na mwanafunzi.
Kwa mujibu wa hukumu ya Jaji Malata iliyoko kwenye mtandao wa mahakama, TanzLii, Pastory alishtakiwa na Jamhuri katika Mahakama ya Wilaya ya Missenyi kwa kosa la kubaka mwanafunzi.
Kwenye kesi hiyo ya jinai namba 137 ya mwaka 2023, iliyosikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Missenyi, upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mahakamani kwamba Pastory alibaka mwanafunzi hivyo akakutwa hana kosa la kubaka.
Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya ya Misenyi ilimuhukumu Pastory kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kosa la kufanya mapenzi na mwanafunzi wa shule ya sekondari.
Kwamba, kwa mujibu wa kifungu cha 60A cha Sheria ya Elimu, kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, kufanya mapenzi na mwanafunzi ni kufanya mapenzi kulikokatazwa, hivyo Pastory alihukumu kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani.
Hukumu ya Jaji Malata inaeleza kuwa Pastory hakuridhishwa na uamuzi huo hivyo aliamua kukata rufaa Mahakama Kuu, Bukoba ambako upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mwandamizi Msomi Mutungi ulieleza mahakakani hapo kuwa kosa alilohukumiwa nalo Pastory halipo kisheria.
Wakili Mutungi aliieleza mahakama kuwa vifungu vilivyotajwa na kutumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Missenyi kumfunga gerezani Pastory, vinakataza kumpa mimba na au kumuoa mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari lakini hakuna sehemu katika vifungu hivyo vya sheria inayoharamisha kufanya mapenzi na mwanafunzi hivyo ni kosa ambalo halipo.
Hukumu ya Jaji Malata inaeleza zaidi kuwa Wakili Mwandamizi Msomi Mutungi aliieleza mahakama kuwa Pastory alitiwa hatiani kwa kosa ambalo halipo kisheria hivyo Jaji Malata alihitimisha hukumu yake kwa kumwachia huru mshtakiwa isipokuwa kama atashikiliwa tena, iwe kwa kosa jingine.