MAKALA YA MTANGAZAJI
MWENENDO wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) sasa ni wa mchakamchaka, idadi ya watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa imeongezeka kwa asilimia 11 na mapato liliyokusanya shirika kwa mwaka 2023/2024 yamevuka malengo kwa asilimia 21.
TANAPA limetekeleza kwa ufanisi mkubwa malengo makuu nane liliyopanga kuyatekeleza mwaka 2023/2024; sambamba na utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema, utatuzi wa migogoro kati ya binadamu na wanyama wakali na waharibifu pamoja na ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya shughuli za utalii hifadhini.
Haya yanaelezwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA,) Musa Kuji katika taarifa yake kwa mwaka 2023/2024 kuhusu mwenendo wa shirika hilo analoliongoza inayoonyesha jinsi alivyolichechemua kutekeleza kwa ufanisi mipango yake.
Kamishna Kuji anasema kwa muda wa mwaka mmoja, 2023/2024 alioshika hatamu za kuliongaza TANAPA, idadi ya walitalii waliotembelea Hifadhi za Taifa ilizidi kwa watalii 33,028 ya matarajio; na makusanyo ya mapato yalivuka lengo kwa ziada ya Shilingi bil. 29 zilizotarajiwa kukusanywa.
Watalii wakiwa wamepumzika kwemye eneo maalumu lilitengenezwa kwa ajili ya mapumziko ya watalii wawapo kwenye hifadhi.
Kwa maneno yake mwenyewe, Kamishana Kuji anasema; “kwa kipindi cha kuanzia Julai mosi, 2023 hadi Juni 30, 2024 shirika lilitarajia kupokea jumla ya wageni 1,830,080 lakini tulipambana kweli kweli tukavuka hilo lengo. Wageni walioingia katika kipindi hicho ni 1,863,108.
“Kwenye mapato ni hivyo hivyo, tulivuka lengo. Katika kipindi hicho cha kuanzia Julai mosi, 2023 hadi Juni 30, 2024 shirika lilitarajia kukusanya mapato ya Shilingi 382,307,977,497.07 lakini tulikusanya jumla ya Shilingi 410,902,998132.31. Makusanyo hayo yana ziada ya Shilingi 28,595,020,635.24. Hivyo naweza kusema TANAPA tumetekeleza malengo yetu kwa mwaka 2023/2024 kwa zaidi ya asilimia 100.
“Tumefanikiwa hivi kwa sababu tunaye Rais ambaye ana nia ya dhati kabisa ya kuinua sekta ya utalii katika nchi yetu. Juhudi zake na kujitoa kwake kwa nchi yetu ni kukubwa mno. Umma unajua hili jinsi alivyotenga muda wake kutengeneza filamu ya The Royal Tour.
“Tunamshukuru na tunampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia ipasavyo sekta ya utalii kwa sababu ameuhakikishia ulimwengu kuwa Tanzania ni mahali salama pa kutembelea na yenye fursa lukuki za uwekezaji katika sekta ya utalii.”
Rais Samia Suluhu Hassan.
Kamishna Kuji anataja malengo makuu ya TANAPA yaliyokuwa kwenye mipango ya utekelezaji katika kipindi hicho kuwa ni shughuli za ulinzi na usalama katika hifadhi, udhibiti wa uingizaji mifugo ndani ya Hifadhi za Taifa, Ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za hifadhi na utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema.
Anataja malengo mengine kuwa ni kushughulikia migogoro kati ya binadamu na wanyama wakali, ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya shughuli za utalii na uhifadhi, utekelezaji wa shughuli za utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Hapo anafafanua kuwa; “Kuhusu utekelezaji wa malengo ya shirika kwa mwaka jana, nianze na shughuli za ulinzi na usalama. Kuanzia Julai mosi, 2023 hadi Juni 30, 2024 shirika lilipanga kufanya doria 61,765 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa rasilimali mbalimbali zilizopo kwenye hifadhi zetu.
Askari wa TANAPA akiwa kwenye doria hifadhini.
“Doria tulizofanya ni 58,016, hivyo utekelezaji wa jukumu letu la kulinda rasilimali mbalimbali zilizopo kwenye hifadhi zetu za Taifa tulilitekeleza kwa asilimia 93.93; na kwa upande mwingine niseme jukumu la udhibiti wa uingizwaji mifugo ndani ya Hifadhi za Taifa, sisi kama shirika tulikabiliana na changamoto hiyo kwa kutumia vikosi maalumu vya doria.
“Katika hilo, jumla ya mifugo 27,598 ilikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria na chanzo cha tatizo hili la mifugo kuingizwa hifadhini ni idadi kubwa ya mifugo iliyo karibu na mipaka ya hifadhi zetu. Kwa hiyo kwa kweli tatizo ni kubwa lakini tulikabiliana nalo kwa uzito kwa sababu ulinzi wa hifadhi hizi ni jukumu letu.”
Mifugo iliyokamatwa na askari wa TANAPA baada ya kuingizwa hifadhini kinyume cha sheria ikiwa chini ya uangalizi wa askari hao.
Kamishna Kuji anazungumzia pia ushirikishwaji jamii katika shughuli za uhifadhi. Anasema TANAPA kupitia mpango wake wa ujirani mwema lilifika kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi zote linazozisimamia. Anasema Hifadhi za Taifa zipo 21 na anataja mikoa zilipo kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Lindi, Morogoro, Iringa, Ruvuma, Dodoma, Mbeya, Njombe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora, Geita, Mwanza, Kagera, Simiyu na Mara.
“Tumefika kwenye vijiji na mitaa iliyo kwenye mikoa hiyo ambako shughuli mbalimbali za kimazingira zinafanyika. Shughuli hizo ni zinazojumuisha misitu ya vijiji, kuandaa vitalu vya miti na upandaji miti kila mwaka, uhifadhi wa vyanzo vya maji, miradi ya mkaa endelevu, biashara ya hewa ya ukaa (Carbon trading), ufugaji nyuki na usimamizi wa fukwe (Beach management units).
“Tumehakikisha tunaimarisha uhusiano na jamii zinazoishi kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi za Taifa kwa kutoa elimu ya uhifadhi na kuchangia shughuli za maendeleo katika vijiji hivyo kupitia miradi ya ujirani mwema ya support for community initiated projects – SCIP na TANAPA income generating project – TIGP.
Twiga wanapatikana kwenye hifadhi nyingi zinazosimamiwa na TANAPA
“Utekelezaji wa miradi hii una lengo la kutatua changamoto za kiuhifadhi sambamba na kutatua changamoto za kijamii kwa wananchi. Sasa hadi Juni 2024 kuna miradi 19 iliyokamilika katika Hifadhi za Taifa za Kilimanjaro ambako kuna miradi mitatu, Kitulo miwili, Mahale mmoja, Mikumi miwili, Mkomazi mitatu, Ruaha miwili na Serengeti ambako ipo sita.
“Kuna vijiji 97 ambavyo vina shughuli za utalii zinazojumuisha utalii wa kitamaduni kama nyimbo na vyakula vya asili na pia kuna mapango ya kizamani na utalii wa kimazingira unaohusisha chemichemi za maji moto na pia maporomoko ya maji (water falls); shughuli zote hizi zinaratibiwa na TANAPA.”
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakiwa kwenye maporomoka ya maji.
Kamishna Kuji anaeleza zaidi kuwa utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema ilitekelezwa kupitia program ya shirika ya ujirani mwema na kwamba miradi 43 ilitekelezwa kwenye Hifadhi za Taifa.
Anataja hifadhi zilizo na miradi hiyo na idadi kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuna mradi mmoja, Mikumi mmoja, Ibanda – Kyerwa mmoja, Kitulo mmoja, Mahale Mountains mmoja, Ziwa Manyara mmoja, Saadan mmoja, Ruaha mmoja, Rumanyika – Karagwe mmoja, Tarangire mmoja, Kigosi mmoja, Burigi – Chato mmoja, Ugalla River miwili, Nyerere minne, Kilimanjaro mitano, Mkomazi sita na Serengeti 14.
Anasema hadi Juni 30, 2024 miradi 15 ilikuwa imekamilika na kukabidhiwa, miradi 10 ipo kwenye hatua za mwisho za utekelezaji na 18 ipo katika hatua za awali za utekelezaji.
Kisha anazungumzia migogoro ya binadamu na wanyama wakali na waharibifu kuwa nayo TANAPA lilishughulika nayo kwa mafanikio makubwa.
Anasema kuanzia Julai Mosi, 2023 hadi Juni 30, 2024 matukio yaliyoripotiwa ni 1,962 na yalitokea katika vijiji 291 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa ambako vikosi vya doria vya TANAPA vilifika kwa wakati.
Watalii wakiangalia Simba hifadhini.
“Katika kipindi hicho tumefika katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi za Taifa 14 ambako tulifanya mikutano ya uhamasishaji kuhusu mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na migogoro baina ya binadamu. Hifadhi hizo ni Arusha, Burigi – Chato, Ibanda – Kyerwa, Ziwa Manyara, Mahale, Mkomazi, Nyerere, Serengeti, Ruaha, Kisiwa cha Rubondo, Rumanyika – Karagwe na Saadan.”
Kuhusu miundombinu, Kamishna Kuji anasema; “Tumefanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya utalii kwenye vituo vya kutolea huduma elekezi (VIC) hifadhini, tumeboresha viwanja vya ndege na barabara za utalii kwa ajili ya kukidhi huduma bora kwa watalii wanaotembelea hifadhi zetu za Taifa.
“Kwa mwaka mmoja huo ulioishia Juni, 2024 kilometa za barabara zilizolimwa na kukabaratiwa ni 10,733 lakini pia kazi ya kuweka mitandao yote ya barabara (road segiments) kwa majina yake kwenye mfumo wa kidijitali imeanza kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Vile vile tumefanya kazi ya uwekaji wa alama elekezi (sign posts) za kutosha katika maeneo yote ili kurahisisha uelekeo na pia kurahisisha shughuli za kuona vivutio wakati watalii wanapokuwa katika safari zao, tumeboresha maeneo ya kupumzikia (picnic sites) ndani ya hifadhi kwa kuweka vivuli na huduma muhimu kama choo yenye kujali uoto na mazingira yasiharibike na kutosababisha usumbufu kwa wanyamapori.”
Watalii wakiangaliaa wanyama hifadhini.
Kamishna Kuji anazungumzia pia utekelezaji wa shughuli za utalii akieleza kuwa TANAPA limehakikisha huduma zinazotolewa ni za viwango vya ubora unaokidhi matarajio ya watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa na kwamba TANAPA limeendelea kushiriki mikutano, maonyesho na misafara ya kutangaza utalii duniani kote.
Anasema; “Tumeshiriki kwenye tourism expo Japan katika Jiji la Tokyo, World travel markert (WTM) katika Jiji la London Uingereza na kwa kushirikiana na wadau wa utalii, TANAPA tulikuwepo kwenye msafara wa kutangaza utalii katika Bara la Asia. Msafara huo ulizifikia nchi za Finland, Denmark, Sweden na Estonia na ulijulikana kwa jina la My Tanzania Road Show.
“Wizara yetu, Wizara ya Maliasili na Utalii ina viongozi wazuri sana sana kwa sababu wako karibu sana na shirika kiutendaji. Wanatusaidia sana na TANAPA linawashukuru sana. Lakini pia Bodi ya Wadhamini, tuna bodi safi mno. Ipo na shirika bega kwa bega wakati wote.
“Wafanyakazi wana michango chanya sana kwenye shughuli za shirika. Mimi kama kiongozi wao ninajua na ninatambua kazi zao maana hata mafanikio tuliyoyapa kwenye kutangaza utalii kimataifa, kuna mchango mkubwa wa juhudi zao sambamba na wadau wetu wa uhifadhi na utalii.
Hapo anaongeza kuwa TANAPA lilishiriki mkutano wa World tourism travel council (WTTC 2023) uliondaliwa na baraza la ushauri la usafiri na utalii duniani na kufanyika Kigali, Rwanda.
Mandhari yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.
Baada ya maelezo hayo marefu, Kamishna Kuji anageuki malengo ambayo hayakutekelezwa na TANAPA katika kipindi cha mwaka 2023/24 kwa kueleza kuwa kulingana na mpango kazi lililokuwa limejiwekea, baadhi ya miradi ya ujirani mwema na maendeleo hasa ya kimkakati haikutekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa.
“Hadi Juni 30, 2024 mipango yetu TANAPA ya matumizi ya kawaida tuliyokuwa tumejiwekea tuliitekeleza yote isipokuwa baadhi ya miradi ya ujirani mwema na ile ya maendeleo hasa ya kimkakati kama ujenzi wa hotel ya nyota tatu ya Burigi Chato na ujenzi wa uwanja wa golf katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ndiyo ambayo haikutekelezwa kwa kiwango tulichotarajia.
“Na sababu zipo ambazo baadhi ni kuchelewa kupata fedha za miradi ya maendeleo, kukwama kwa baadhi ya wakandarasi kutekeleza miradi kwa wakati kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa rasilimali za kuendesha maeneo ya uhifadhi hasa hasa hifadhi za kusini, magharibi na mashariki ambazo uzalishaji haukidhi mahitaji ya uendeshaji.”
Anapofika hapo anaweka tuo na kushika glass ya maji kulegeza koo kutokana na maelezo marefu aliyoyatoa, na mimi naweka kalamu chini kupisha nafasi ya mapumziko.