MAKALA YA MTANGAZAJI
UFINYU wa Bajeti, uingizwaji wa mifugo kwenye Hifadhi za Taifa kinyumwe cha sheria, mabadiliko ya tabianchi, kuchelewa kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ni mambo yaliyotikisa mwenendo wa utekelezaji wa mipango ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa mwaka 2023/2024.
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Musa Kuji hapa anazungumzia changamoto hizo na jinsi TANAPA lilivyokabiliana nazo hadi kufanikiwa kuvuka malengo ya utekelezaji wa mipango yake kwa mwaka 2023/2024; pamoja na mipango ya muda mfupi na muda mrefu lililojiwekea shirika hilo ili kufikia lengo la kuhudumia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025 ambayo pia ni azma iliyowekwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Watalii wakiwa wamepumzika kwenye eneo maalumu la kupumzika watalii hifadhini.
Kamishna Kuji anaanza kwa kutaja changamoto ya ufinyu wa bajeti ya uendeshaji. Anasema; āUfinyu wa bajeti ya uendeshaji ni changamoto kubwa iliyotutikisa mwaka 2023/2024. Napenda ifahamike kuwa bajeti ya hifadhi 16 ndiyo inatumika kuendesha hifadhi 21 tulizonazo nchini pamoja na kanda nne, vituo vitano vya Malikale na ofisi mbili kiunganishi zilizopo Dar es Salaam na Dodoma.
āLakini tulifunga mkanda, tukakabiliana na hali hiyo. mimi na wenzangu kwenye menejimenti tulikubaliana kila senti tunayopokea kwa ajili ya uendeshaji shughuli za shirika ni lazima thamani yake ionekane. Tulifanikiwa.
āMimi na wenzangu tunaendelea na jitihada za kuiomba Serikali iongeze ukomo wa bajeti (ceiling) ya uendeshaji wa shirika.
āHatua hii italiwezesha shirika kujiendesha kwa ufanisi zaidi ikiwemo kuongeza uwezo wa kudhibiti vitendo vya ujangili na kukusanya mapato zaidi. Na hilo likifanyika, litawezesha shirika kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa kwa sababu shirika litakuwa na misuli ya kutosha ya utekelezaji wa mipango tuliyojiwekea.ā
Changamoto ya pili anayoitaja ni uingizwaji wa mifugo katika Hifadhi za Taifa kinyume cha sheria jambo lililoilazimu TANAPA kuimarisha doria na utoaji elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka Hifadhi za Taifa.
Mifugo iliyokamatwa kwa kuingizwa hifadhini kinyume cha sheria.
Nyumbu wakiruka kuvuka mto ulio hifadhini
Anasema; āKatika kukabiliana na changamoto hii tuliendelea kuimarisha doria na kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka Hifadhi za Taifa kuhusu athari za uingizwaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi.
āLakini tulienda mbali zaidi ya hapo kwa kuwaalika wadau wengine ambao tulishirikiana nao kuandaa na kutekeleza mpango wa matumizi ya ardhi (village land use pkans) katika maeneo ya vijiji vinavyopakana na Hifadhi za Taifa.ā
Kamishna Kuji anataja changamoto ya tatu kuwa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo athari zake zilisababisha kuongezeka kwa mimea vamizi, migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Anasema; āChangamoto hii tulikabiliana nayo kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Askari wa TANAPA.
āAidha, tuliendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kukabiliana na mimea vamizi, tulichimba mabwawa na visima vya maji kwa ajili ya upatikanaji wa maji kwa wanyamapori na tulifanya kazi ya kupanda miti ya asili na rafiki kwa mazingira katika maeneo ya vyanzo vya maji.
āKazi nyingine tuliyofanya ili kukabiliana na changamoto hii ni kubainisha mipaka ya hifadhi kwa kuweka alama (beacons) ili kuzuia wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na tulihamasisha uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.ā
Changamoto ya tano ya kuchelewa kupata fedha za miradi ya maendeleo, anasema hiyo bado inaendelea kufanyiwa kazi kwa kuendelea kujenga hoja kwa Serikali kuiomba ilipatie TANAPA fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa miradi iliyopangwa.
Changamoto ya mwisho inayotajwa na Kamishna Kuji ni ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu; anasema, āHapa sasa kuna kazi kubwa imefanyika, tulitumia askari wetu wa wanyamapori wa vijiji na Jeshi la Akiba hasa katika vijiji vyenye changamoto kubwa ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ili kuongeza mwitikio wa haraka.
āLakini pia kwa muda wote ambapo matukio hayo yalitokea, tulishirikiana na wadau wa uhifadhi na wananchi kudhibiti na tuliweka nguvu kubwa kwenye matumizi ya teknolojia ikiwemo kufunga visukuma mawimbi kwa makundi ya tembo kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji.
Kundi la wanyama mbalimbali wanaopatikana katika Hifadhi za Taifa.
āVisukuma mawimbi vinaunganishwa na mifumo ikiwemo uzio wa kielektroniki, kwa lugha ya kitaalamu wanasema Geo ā fencing na Earth range inayotoa taarifa kwa wakati zinazowezesha askari wetu kuwadhibiti wanyamapori wasivuke maeneo ya mipaka kwenda maeneo ya vijiji.
āMara zote katika kipindi cha mwaka huo mzima, tuliimarisha doria katika vituo vya askari wa mwitikio wa haraka. Ninaamini wadau wa utalii na wananchi watakuwa wamepata picha ya namna gani tulivyokabiliana na changamoto zilizokuwa mbele yetu kwa mwaka 2023/2024.ā
Kando ya changamoto hizo na utatuzi wake, Kamishna Kuji anazungumzia mipango inayotekelezwa na TANAPA kwa mwaka 2024/2025, anasema; āSasa mipango ya muda mfupi ya shirika ni kuendelea kuhifadhi maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa na rasilimali zilizomo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
āNdani ya maeneo hayo, kuna wanyamapori, Bioanuai na makazi ya wanyamapori. Sasa uhifadhi wake unafanyika kwa kuimarisha ulinzi ili kuiishi kauli mbiu ya Wizara ya Maliasili na Utalii isemayo TUMERITHISHWA ā TUWARISISHE.
āPia katika mipango yetu mwaka 2024/2025 tunapambana kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii katika Hifadhi za Taifa kwa kuboresha miundombinu na utoaji huduma kwa wageni wanaotembelea Hifadhi za Taifa.ā
Kamishna Kuji anaendelea kwa kueleza mipango ya muda mrefu ya TANAPA kuwa kwanza ni kujiunga na biashara ya hewa ya ukaa duniani.
āHili nilieleze vizuri ili umma ulielewe kwa ufasaha. TANAPA lina jumla ya hekta takriban milioni tatu za misitu ya asili zilizohifadhiwa katika hifadhi mbalimbali. Na lengo la kuhifadhi misitu hii ni kupambana na mabadiliko ya tabianchi duniani.
āMwelekeo wa uhifadhi duniani ni kulinda maeneo ya misitu iliyohifadhiwa kwa kuwalipa fedha taasisi, jamii na watu binafsi waliohifadhi misitu ya asili katika maeneo wanayoyasimamia na kuyamiliki.
Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Kuji (kulia) Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk Richard Matolo (katikati) na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano, Catherine Mbena wakikagua matengenezo ya barabara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
āNa ifahamike kuwa biashara ya hewa ya ukaa ni endelevu na tayari baadhi ya taasisi na watu binafsi hapa nchini zimejiunga na kuanza kufaidika na biashara hiyo.
āTANAPA tumewasiliana na Kituo cha Biashara ya Hewa ya Ukaa hapa nchini ili kupata taratibu za kujiunga na faida zake na tunatarajia kuanza na hifadhi zilizo katika ukanda wa magharibi, kusini na mashariki ambazo zina misitu mikubwa.ā
Kamishna Kuji anamalizia taarifa yake kwa kueleza kuwa katika mipango ya muda mrefu ya shirika pia kuna kuimarisha utendaji kazi wa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji inayofahamika kwa jina TANAPA Investment Limited.
Anasema TANAPA limeanzisha kampuni hiyo ambayo miongoni mwa majukumu yake ni kufanya kazi kibiashara. Anasema kampuni hiyo imekwishasajiliwa na kupata leseni ya daraja la kwanza (class one contractors in building and civil works.)
Kamishna Kuji anasema kampuni hiyo imeanzishwa ili kufanya kazi za ujenzi za ndani ya shirika na za nje ya shirika kibiashara na pia inafanya kazi za ushauri elekezi (consultancy) na mapato yanayotokana na uwekezaji huo yatatumika kuendeleza shughuli za utalii na uhifadhi.